The House of Favourite Newspapers

Kiongera avuna mamilioni Simba

0

kiongeraWilbert Molandi, Dar es Salaam
KAMA siyo dola 10,000 (sawa na shilingi milioni 20), basi mshambuliaji Mkenya, Paul Kiongera, asingerejea tena kuichezea Simba.

Mshambuliaji huyo, tayari amejiunga na wenzake huko Unguja, Zanzibar kwenye kambi ya pamoja kujiandaa na Ligi Kuu Bara na mechi ya kwanza atakayokabiliana nayo ni dhidi ya Azam FC Jumamosi ijayo.

Mkenya huyo, amerejea Simba akitokea KCB ya ambako ameongezwa kwenye usajili wa dirisha dogo baada ya Kocha Mkuu, Muingereza, Dylan Kerr kupendekeza. Alikuwa akicheza huko kwa mkopo.

Kwa mujibu chanzo cha habari kutoka ndani ya Kamati ya Usajili ya Simba, awali walipomfuata mshambuliaji huyo, aligoma kujiunga na kikosi hicho akitaka kwanza amaliziwe fedha zake za usajili anazoidai ambazo ni dola 10,000.

Chanzo hicho kilisema, wakati wanaendelea na mazungumzo hayo, mshambuliaji huyo aligoma kuja kukabidhiwa fedha hizo Dar es Salaam, akiomba atumiwe nyumbani kwao Kenya.

Kiliongeza kuwa, mshambuliaji huyo mara baada ya kutoa sharti hilo, uongozi ulifanya jitihada za kutosha na kumtumia, ndipo alipotua Zanzibar.

“Wakati tunamsajili Kiongera, hatukuwa tumempatia fedha zote za usajili, hivyo tulimpatia fedha nusu na nyingine tukipanga kummalizia baada ya muda fulani.

“Lakini mara baada ya kuumia, tukashindwa kummalizia fedha hizo ambazo ni dola 10,000 ambazo tumempatia hivi karibuni, siku moja kabla ya kujiunga na wenzake Zanzibar.

“Kiukweli kabisa aligoma kabisa kurejea kuichezea Simba katika usajili huu wa dirisha dogo akiomba kwanza amaliziwe fedha hizo, lakini tunashukuru tayari tumempatia,” kilisema chanzo hicho.

Aidha alipotafutwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hans Poppe, kuzungumzia suala hilo simu yake ya mkononi haikuwa inapatikana huku ikielezwa kuwa yupo nje ya nchi.

Leave A Reply