Kisa Kaze, Mabosi Yanga Wavamia Kambi

KATIKA kurejeshwa morali na kuwapa nguvu ya ubingwa wa Ligi Kuu Bara, mabosi wa Yanga juzi Jumatano walivamia kambi ya timu hiyo na kufanya kikao kizito.Hiyo ikiwa ni siku moja tangu uongozi wa timu hiyo utangaze kumsitishia mkataba wa miaka miwili ambao kocha huyo aliusaini kukinoa kikosi hicho.

 

Timu hiyo iliingia kambini Kijiji cha Avic Town, Kimbiji huko Kigamboni nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam juzi Jumatatu kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mchezo wao wa ligi dhidi ya KMC FC Aprili 7, mwaka huu utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, mabosi hao waliovamia kambi hiyo ni Mwenyekiti wa timu hiyo, Dk Mshindo Msolla na makamu wake Frederick Mwakalebela na viongozi wengine wa kamati ya utendaji.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa kikao kilianza kufanyika saa moja kamili usiku na kumalizika saa tatu kamili na kikubwa viongozi hao walimpa maneno ya kuwaongezea nguvu na morali ya kufanya vizuri katika michezo inayofuatia ya ligi ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.

 

Aliongeza kuwa viongozi hao waliwataka wachezaji kutokata tamaa baada ya kipigo dhidi ya Coastal Union cha mabao 2-1 na sare ya bao 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania na badala yake kuongeza hali ya kujituma ili watimize malengo yao ya ubingwa katika msimu huu.

 

“Mara baada ya kocha Kaze kuwaaga wachezaji kuwa anaondoka nchini baada ya mkataba wake kusitishwa, wachezaji walionekana kuwa na majonzi makubwa.“Hivyo katika kurejesha morali na hali yao ya kujituma, viongozi haraka walivamia kambini usiku na kufanya kikao na wachezaji wote pamoja na Kaimu Kocha Mkuu, Mwambusi (Juma).“

Kikubwa tunashukuru kikao kilifanikiwa ambacho kiliendana na chakula cha jioni na wachezaji wamejiwekea malengo yao ya kupambana ili kuhakikisha wanauchukua ubingwa wa ligi na uongozi kwa upande wao watatimiza kila mahitaji yao ikiwemo bonasi yao kila wanapopata matokeo mazuri ya ushindi,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa Mwakalebela kuzungumzia hilo alikiri na kusema: “Ni kweli kabisa tulikutana na wachezaji wetu na kuzungumza mengi na kati ya hayo ni kuwapa morali ya kujituma katika michezo yetu ijayo ya ligi na kikubwa kupata ushindi.

 

“Wachezaji walitusikiliza na kutuahidi kufanya vizuri ili kutimiza malengo yetu ambayo ni kuchukua ubingwa wa ligi na Kombe la FA, tunafahamu wachezaji wapo katika kipindi kigumu ambacho kocha wao amesitishiwa mkataba.”

STORI: WILBERT MOLANDI,Dar es Salaam


Toa comment