Kartra

Kisa Simba, Senzo Avamia Kambi

Senzo Mazingisa, raia wa Afrika Kusini.

KATIKA kuongeza morali na mzuka wa ushindi, Mshauri wa Yanga, Senzo Mazingisa, raia wa Afrika Kusini, juzi jioni alivamia kwenye kambi ya timu hiyo na kufanya kikao na wachezaji, benchi la ufundi.

 

Hiyo ni katika kuelekea mchezo wao wa leo Jumamosi wa Kombe la FA dhidi ya Kengold FC ya mkoani Mbeya utakaopigwa saa kumi kamili kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

 

Yanga yenye pointi 49, ikiongoza kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, imepanga kubeba mataji yote katika msimu huu ikiwemo huo wa ligi na Kombe la FA ambayo yote yanawaniwa na wapinzani wao Simba wenye muendelezo mzuri wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, Senzo alifanya ziara hiyo ya kushtukiza katika kambi ya timu hiyo iliyopo Kijiji cha Avic Town, Kigamboni na kufanya kikao cha pamoja na wachezaji, benchi la ufundi kabla ya kuanza mazoezi.Mtoa taarifa huyo alisema kikao hicho kilitumia dakika 15 ambacho kilifanyika katikati ya uwanja na kikubwa mshauri aliwasisitiza ushindi katika kuelekea mechi ya leo.

 

Aliongez kuwa mshauri amemtaka kila mchezaji kupambana katika nafasi yake kuhakikisha wanaendelea kupata matokeo mazuri baada ya kutoka kupata ushindi wa ligi dhidi ya Mtibwa Sugar.

 

“Juzi (Alhamisi) jioni tulipata ugeni wa ghafla kutoka kwa mshauri wa klabu, Senzo ambaye alifika kambini na kufanya kikao cha pamoja na wachezaji, benchi lote la ufundi

“Na kikubwa katika kikao hicho amezungumzia kuhusu majukumu ya wachezaji uwanjani na kuhakikisha wanapambana kufikia malengo ya kubeba makombe yote kwa kuanzia ligi na FA.

 

“Unajua ile kasi ya wapinzani ambao ni Simba ya kupata matokeo mazuri kwenye ,echi zao za ligi kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutoka kuzifunga klabu kubwa Afrika za AS Vita na Al Ahly inatisha,” alisema mtoa taarifa huyo.

Senzo juzi (Alhamisi) jioni alitupia picha mtandaoni akiwa kambini huko pamoja na wachezaji, benchi la ufundi akizungumza nao na kuandika: “Mazoezini jioni, Daima Mbele, Nyuma Mwiko.

 

”Katika hatua nyingine, uongozi wa Yanga umempa kocha faili la wapinzani wao Kengold wataocheza nao leo na lengo ni kuwajua vizuri wapinzani wao hao wa FA.

 

Kengold inashiriki Ligi Daraja la Kwanza na katika msimamo wao wa Kundi A iko nafasi ya tatu baada ya kucheza mechi 10 ambapo imeshinda michezo mitano, sare moja na kufungwa minne.

 


Toa comment