The House of Favourite Newspapers

Kocha Mghana Afungasha Mabegi Yanga SC, Asepa

0

IMEFAHAMIKA kuwa, Kocha wa Viungo wa Yanga, Edem Mortotsi, amesitisha mkataba wake wa miezi sita wa kuendelea kukinoa kikosi hicho.

 

Kocha huyo raia wa Canada mwenye asili ya Ghana, alijiunga na Yanga Januari 27, mwaka huu baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mrundi, Cedric Kaze kumpendekeza kwa ajili ya kufanya naye kazi.Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, kocha huyo alianza vituko vya hapa na pale mara baada ya mkataba wa Kaze kusitishwa Machi 7, mwaka huu.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, vituko hivyo alivianza baada ya kuona anakosa amani na furaha katika timu hiyo, kituko cha kwanza alichoanza nacho ni kuomba apangiwe nyumba ya kuishi nje ya kambi iliyopo Avic Town, Kigamboni, Dar es Salaam.

 

Aliongeza kuwa, kabla ya kupewa nyumba hiyo, aliulizwa na mabosi wa timu hiyo achague sehemu atakayotaka kuishi ndani au nje ya Kigamboni, lakini akashindwa kutoa majibu.

 

 

Chanzo hicho kiliendelea kueleza kwamba, wakati viongozi wakisubiri majibu ya sehemu anayotaka kukaa, akaibuka na kuomba kulipwa pesa zake za kuvunja mkataba, baada ya siku mbili kabla ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC, akawaaga viongozi na kusema anarudi kwao.

 

“Hili la Edem kuomba kuondoka Yanga muda mrefu tulilijua mara baada ya kusitisha mkataba wa Kaze ambaye ndiye aliyempendekeza aje kufanya naye kazi.“Mara baada ya Kaze kuondolewa alianza vituko vingi kati ya hivyo tulishangaa kumsikia kuomba alipwe pesa zake za kuvunja mkataba wakati yeye yupo kwenye mkataba na bado tunamuhitaji.

 

 

“Hivyo Edem hayupo na timu hivi sasa na hata kwenye mchezo wetu wa ligi uliopita dhidi ya KMC hakuwepo katika benchi la ufundi, amerudi kwao Ghana na mabegi yake yote, hivyo hatarejea. Uongozi unafanya jitihada za kumleta kocha mwingine wa viungo,” alisema mtoa taarifa huyo kutoka ndani ya benchi la ufundi la timu hiyo.

 

 

Alipotafutwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Hassani Bumbuli kuzungumzia hilo, alisema: “Hilo suala siwezi kulizungumzia kwa hivi sasa, hivyo subiri hadi taarifa rasmi itakapotolewa na uongozi.”

Leave A Reply