The House of Favourite Newspapers

Kocha Simba, Global Wawakumbuka Mayatima Mwanza

0
Mwakilishi wa Global Publishers Shaban Ally akitoa misaada kwa Mama mlezi  Rehema Shaban wa kituo cha kulea watoto yatima cha Ngamia kilichopo Kangaye Wilayani Ilemela jijini Mwanza 

 

Kampuni ya Global Publishers chini ya Mkurugenzi Mtendaji, Eric Shigongo wakishirikiana na aliyekuwa kocha na mchezaji wa zamani wa Simba SC, Talib Bilali leo Jumamosi, Aprili 25, 2020, imefanikiwa kutoa msaada wa vitu mbalimbali kwa kituo cha kulelea watoto yatima cha Masjid – Ngamia kilichopo Kangaye- Wilayani Ilemela jijini Mwanza.

Global na Talib Bilali wamefanikiwa kutoa msaada wa vitu kama sukari, unga wa ngano, mafuta ya kupikia, maharage pamoja na ndoo za kutakasa mikono katika kipindi hiki cha kujikinga na virusi vya corona ambavyo vinazalisha ugonjwa wa Covid-19.

 

Akizungumza na Global Pulishers, Mama mlezi wa kituo hicho, Rehema Shaban amesema;” Kwanza napenda kuwapongeza sana Kampuni ya Global Publishers kwa kushirikiana na Talib Bilali kwa msaada huu waliotupatia, msaada huu utatusaidia kwa mambo mbalimbali kwani kama mlivyoona hatukuwa na ndoo ya kunawia mikono ila tumepata kutoka kwa Global hivyo tunawapongeza sana.”

Watoto yatima wanaolelewa katika kituo hicho wakiwa kituoni hapo.

 

“Tunaendesha kituo hiki katika mazingira magumu sana kwani hatupati misaada lakini kwakua ni wito kufanya hii kazi ya kulea hawa watoto yatima tunajikamua wenyewe mifukoni ilimradi siku ziende, hivyo misaada hii itatusaidia sana kipindi hiki cha mwezi Mtukufu wa Ramadhan ambapo sasa watoto hawa wanaweza kufunga kwakua uhakika wa kupata chakula kila siku upo kutokana na misada ambayo tumepata,” alisema Rehema.

Aidha, kwa upande wake Shaban Ally ambaye amekabidhi misaada hiyo kwa niaba ya Global Publishers amesema; “ Global imetoa msaada huu kwa kuzingatia kwamba hawa watoto wanaishi kwenye mazingira magumu, hivyo nawaomba wasimamizi wa kituo hiki watumie hii misaada kama ilivyokusudiwa,“ alisema.

 

Kwa sasa Talib ni kocha mkuu wa timu ya taifa ya soka la ufukweni la Oman na aliamua kufanya hivyo kwa kuwa lilikuwa lengo lake siku nyingi lakini hakuwa amepata wa kushirikiana naye kufikisha misaada yake.

 

 

 

“Nilipoona Global mnasaidia watu mitaani, nikaona ni watu ambao ninaweza kushirikiana nao kufikisha hiki nilichonacho  kupitia kampuni hii kwa ajili ya Watanzania na hasa sasa ambapo ni mwezi wa Ramadhani.  Nashukuru sana,” alisema Talib.

 

Kabla ya hapo, kwa kushirikiana na Global Group pia, Talib alitoa ndoo na sabuni kwa vituo vinne vya watoto yatima, lengo likiwa kuwasaidia kujikinga na maambukizi dhidi ya Corona.

 

Baada ya hapo, akatoa ndoo  na sabuni pia kwa madereva wa Bajaj na Bodaboda kwa kuwa wamekuwa wakitoa huduma kwa watu. Misaada yake yote imekuwa ikifikishwa na Global Group ambayo awali ilianza kusaidia watu mbalimbali katika jamii na kumvutia kocha huyo.

Habari na Johnson James/GPL

Leave A Reply