The House of Favourite Newspapers

Kocha wa Yanga Ampa Guede Mechi Mbili, Atoa Kauli ya Kibabe

0
Joseph Guede

KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amewaambia mabosi wa timu hiyo wafanye kila wanaloweza apate mchezo wa kimataifa wa kirafiki kabla ya kurejea katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya mapumziko ya kupisha michuano ya Afcon kumalizika.

Gamondi ametoa kauli hiyo kufuatia kuendelea na programu za mazoezi na wachezaji wake wote ambao hajaitwa kwenye timu za taifa zinazoshiriki Afcon.

Mbali na hapo Gamondi anataka kumpima straika wao mpya, Joseph Guede ambaye amesajili kwenye dirisha hili dogo na ndiye atakuwa straika kiongozi kwenye kikosi cha Yanga.

Championi linafahamu kuwa, kocha huyo ameomba michezo miwili ya kirafiki kwa ajili ya kuwapa mechi fitinesi nyota wake.

Akizungumza na Championi Jumatano, Gamondi alisema kuwa kuna kila sababu ya timu yake kupata michezo ya kimataifa ya kirafiki wakati huu wa mapumziko ili kujua ubora wa kikosi chake kwa kupata muunganiko ukiwemo wa wachezaji wapya kabla ya kurejea kwenye michuano ya kimataifa.

“Tunaendelea na mipango yetu kwa sababu bado kazi kubwa ipo mbele yetu na ukiangalia wachezaji baadhi walikuwa kwenye mapumziko mafupi hawakuwepo katika Kombe la Mapinduzi hivyo tumerejea mapema kuweza kujipanga kwa muda huu ambao upo kwa sasa lakini wapo wapya ambao wameingia wanahitaji kuzoea timu ili tufikie malengo.

“Lazima tucheze mechi za kirafiki hasa upande wa kimataifa wakati huu ligi imesimama na ikiwezekana na nyengine za ndani kwa sababu tunalenga kuboresha timu yetu kwa malengo ya kufanya vizuri kimataifa na wachezaji waliongia waweze kwenda sawa na waliokuwepo,” alisema Gamondi.

Stori na Ibrahim Mussa na Wilbert Moland

Leave A Reply