The House of Favourite Newspapers

Kolabo ya Kiba na Mondi Yanukia

0

Kuna vitu ambavyo ni nadra mno kusikia na kuamini kama siku moja vitatokea hasa kwa wasanii wa Bongo Fleva ambao wanaaminika kuwa na uhasama wa kimuziki na kibiashara kama Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ na Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, lakini sasa kuna matumaini mapya ya kolabo kati yao, IJUMAA WIKIENDA limedokezwa.

 

 

Vyanzo vya karibu vya wawili hao vinadai kwamba, uwepo wa makundi (teams) mbili za wasanii hao wakubwa, Team Kiba ya King Kiba na ile ya Diamond au Mondi (Team Mondi), zimekuwa zikichangamsha mambo na kuongeza ushindani, lakini hivi uliwahi kuwaza siku moja zikiungana na kufanya kitu cha pamoja; yaani kolabo nini kitatokea kwenye ‘indastri’ ya Bongo Fleva?

 

 

Katika kile kinachoelezwa kwamba ni matumaini mapya ya uwezekano wa kutokea kwa jambo hilo, usiku wa kuamkia juzi Jumamosi, King Kiba alikuwa mubashara (live) kwenye ukurasa wake wa Instagram ambapo alifanya jambo linaloaminika kufungua milango mipya ya uelewano kati ya Team Kiba na Team Mondi na huwenda likashuhudiwa jambo kubwa la ushirikiano (kolabo) kati yao.

 

 

Kwenye vipande vya video vinavyomuonesha akiwa jikoni akipika, Kiba alikuwa kama DJ ambapo alikuwa akipiga listi ya nyimbo zake anazozipenda zaidi kisha kuziimba na kuzicheza huku akizifurahia kwa hisia kali.

 

 

Miongoni mwa nyimbo hizo ni zile za wasanii walio chini ya Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) ya Mondi wakiwemo Rayvanny, Mbosso, Lava Lava na Mondi mwenyewe.

 

 

Alichokifanya Kiba kimeweka tabasamu kwenye nyuso za mashabiki wao ambapo kwa mara ya kwanza wamejikuta wakizungumza lugha moja na kumuomba Mungu kolabo yao ikamilike siku moja kabla ya mmoja wao kuondoka duniani.

 

 

RAYVANNY

Kiba alianza kuucheza Wimbo wa Kwetu wa msanii Rayvanny kisha akaeleza namna ambavyo kwa muda mrefu wimbo huo umekuwa miongoni mwa nyimbo zake bora anazozisikiliza na kucheza.

 

 

LAVA LAVA

Baada ya hapo aliweka Wimbo wa Tattoo wa Lava Lava akieleza namna ambavyo anaupenda kuanzia mashairi hadi melodi zake kisha akauimba kwa hisia kali kuazia mwanzo hadi mwisho huku akicheza kwa kujiachia kwelikweli.

 

 

Baada ya Lava Lava, pia Kiba aliweka Wimbo wa Nadekezwa wa Mbosso na kusema nao ni mmoja wa nyimbo zake bora. Katika hali ya kuonesha kwamba ni kweli anaujua wimbo huo, Kiba aliuimba wote kwa hisia huku akiucheza kwa ‘vaibu’ kubwa.

 

 

MONDI MWENYEWE

Mwisho; Kiba aliibua shangwe la aina yake kwa wafuasi wake baada ya kusema kwamba kutoka kwa Mondi anauzimia mno wimbo wake wa African Beauty ambao amemshirikisha mwanamuziki wa Marekani, Omarion.

 

 

“Huu ni wimbo wangu bora kabisa wa wakati wote,” alisikika Kiba huku akicheza kwa vaibu kubwa na kuufurahia wimbo huo kupita kiasi. Baadhi ya mashabiki walioguswa na kitendo hicho cha Kiba wanasema kuwa, kuna kila dalili ya kuwepo kwa kolabo kati ya Kiba na Mondi na kwamba kuna siku bifu lao litakuwa ni historia.

 

 

“Ni upendo sana ameuonesha Kiba. Mungu awafanyie wepesi kwani bifu hazifai. “Maisha haya ni mafupi mno, kikubwa ni upendo ambao tayari Kiba ameuonesha.

 

 

“Hii ni ishara nzuri kwa sababu hata Diamond kuna siku aliimba Wimbo wa Hadithi wa Kiba. “Natamani siku moja Kiba na Mondi wafanye kolabo…” Ilisomeka sehemu ya maoni lukuki juu ya alichokifanya Kiba.

 

Kwa upande wake, msanii Baba Levo ambaye anajitambulisha kama ‘chawa’ wa Mondi anasema; “Diamond na Ali Kiba ni ndugu kwa sababu wote ni watoto wa Kigoma. Kiba kumsapoti Diamond ni sawa. Kiba ni msanii mkubwa hapa nchini na nje ya nchi.”

 

 

Kwa upande wake meneja wa Kiba aitwaye Aidan anasema kuwa, hawezi kusema kolabo ipo au haitakuwepo.

“Kuna kitu watu hawakijui. Wakati wa kampeni, kuna siku tulikuwa tunakwenda Katavi kwa kutumia ndege ndogo, kulikuwa na timu ya Diamond na timu ya Kiba kisha tukafikia hoteli moja, kwa hiyo hakuna vita labda kuna kutokukubaliana tu kwenye mtazamo.

 

“Kwa hiyo alichofanya Kiba ni kawaida yake kusapoti wenzake na kupenda nyimbo za wenzake kwa sababu ni mtu anayependa muziki mzuri,” anasema meneja huyo.

 

 

Kiba na Mondi wanatajwa kuwa kwenye bifu la muongo mmoja sasa, tangu Kiba alipomtuhumu Mondi kumfuta kwenye kolabo yao yapata miaka kumi iliyopita.

Stori; Mwandishi Wetu, Dar

Leave A Reply