Kongamano la Katiba! Mbowe, Wenzake Wakamatwa Mwanza

KIONGOZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake zaidi ya 10, wanadaiwa kukamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza usiku wa kuamkia leo Jumatano, Julai 21, 2021, katika Hotel ya Kingdom jijini humo.

 

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema;  “Polisi walifika hotelini hapo na kuwakamata Mbowe na wengine 11 majira ya saa nane usiku. Wamepelekwa Central Polisi ila Mbowe pekee ndio hatujui amepelekwa wapi. Tunaendelea kufuatilia kujua yupo wapi,” amesema Mrema.

 

Mrema amewataja baadhi ya waliokamataa ni, Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, John Heche, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha), John Pambalu na Mhadhiri mwandamizi wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Azaveri Lwaitama.

 

Mbowe na wenzake, wamekamatwa ikiwa ni saa chache zilikuwa zimesalia kabla ya kuongoza kongamano la Katiba mkoani humo. Kongamano hilo lililozuiwa na polisi Jumamosi iliyopita, lilielezwa na Mbowe kwamba litafanyika leo Jumatano huku Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel akipiga marufuku mikusanyiko isiyokuwa na kubali maalum.

 

RC Gabriel alitoa zuio hilo jana Jumanne akidai ni jitihada za kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona ambayo mkoani humo vimeshamili. Hata hivyo, Chadema kupitia kwa Mrema walisema, kongomano hilo litafanyika kwani limezingatia tahadhari ya corona ikiwemo kila mshiriki kuvaa barakoa na kunawa na maji tiririka.

 

Jitihada za kumpaka Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza zinaendelea ili kujua chanzo cha kukamatwa kwa viongozi hao. Endelea kufutilia mitandao yetu ya kijamii kupata taarifa na habari mbalimbali.


Toa comment