The House of Favourite Newspapers

Kukosa Hamu ya Tendo la Ndoa

0

Sababu Za Wanaume

Natumai muwazima wa afya. Leo katika mada yangu hii, nataka kuzungumzia zaidi sababu za wanaume wengi kukosa hamu ya tendo la ndoa.

Kama ilivyo matatizo mengine, tatizo la kukosa hamu ya kushiriki tendo la ndoa huwakumba na wanaume vilevile ila siyo kwa kiwango kikubwa kama ilivyo kwa wanawake.

Katika makala haya, tutaangalia kwa kina sababu za tatizo hili kwa wanaume na athari zake.

Mwili wa mwanadamu uliumbwa na matamanio na si mabaya kama mwenye mwili atakuwa na uwezo wa kujitawala. Wanaume wengi huvutiwa zaidi na hisia za kushiriki tendo la ndoa kwa kuona baadhi ya maungo kwa wanawake, kusikia sauti na hata migusano.

SIYO KUUTAWALA MWILI

Kuna wanaume ambao wapo tu, ilimradi siku zinakwenda, hawapati hamu ya kushiriki tendo la ndoa na wanajiona kama ndiyo wamefanikiwa kujitawala, kumbe ni wagonjwa.

Habari njema ni kwamba, licha ya tatizo hilo kuwasumbua wengi, kuna mambo unayoweza kuyafanya kupunguza ukubwa wa tatizo hili au kuliondoa kabisa kwa kutumia mimea tiba na matunda tiba.

Unachotakiwa kufanya, kama umejaribu kutumia njia mbalimbali  kuondoa tatizo hili bila mafanikio, basi wahi mapema kwa wataalamu ukafanyiwe uchunguzi.

Baadhi ya wanaume wanamini kuwa, hamu ya kufanya tendo la ndoa inapungua kadiri umri wa mwanaume unavyoongezeka. Kuna idadi kubwa ya wanaume ambao hamu yao ya kufanya tendo la ndoa imebaki vilevile hata umri wao kuwa mkubwa.

UKUBWA WA TATIZO KATIKA JAMII

Kwanza tuanze kwa kutazama ukubwa wa tatizo hili. Idadi ya wanaume wanaoridhika kuishi na tatizo hili ni ndogo sana ukilinganisha na ile ya wanawake.

Hata hivyo, tatizo la wanaume kukosa hamu ya kushiriki tendo la ndoa limekuwa ni chanzo kikubwa katika kuleta migogoro katika familia.

Wanaume kwa kawaida ni wabishi na huwa hawapendi kuaibika hivyo mtu anaweza akawa na tatizo lakini asipende mwenza wake ajue kama analo ambapo kumbe kama angeliweka bayana angepata ushauri wa namna ya kulitatua.

Pamoja na kwamba tatizo hili halijitokezi sana kwa wanaume ukilinganisha na wanawake, inakadiriwa kuwa asilimia 15 hadi 16 ya wanaume wana tatizo hili. Ni sawa na uwiano wa mwanaume mmoja mwenye tatizo hili katika kila wanaume sita au saba. Idadi ya wanawake wenye tatizo hili ni mara mbili ya wanaume.

WANAUME WANAKEREKA ZAIDI

Tatizo hili huwakera zaidi wanaume kuliko wanawake kwa sababu wanaume huchukulia urijali kama sehemu ya ukamilifu wa mwanaume na wanakosa raha wanapoona wana upungufu kuhusu mambo ya mapenzi tofauti na wanawake.

SABABU AU CHANZO CHA TATIZO

Tatizo la kukosa hamu ya kufanya tendo la ndoa kwa wanaume linaweza kusababishwa na vitu vingi.

Sababu hizo zinaweza kuwa za kimaumbile, kisaikolojia au za mchanganyiko wa vitu hivyo viwili. Hebu tuone baadhi ya vyanzo vya tatizo hili.

UHUSIANO BAINA YA MWANAUME NA MWANAMKE

Uhusiano kati ya mwanaume na mwanamke ambao ni wanandoa una mchango mkubwa katika kujenga au kubomoa matamanio ya mwanaume.

Kama kutakuwa na matatizo ya uhusiano kama vile ugomvi kati ya wawili hao, kuna mchango mkubwa katika kusababisha tatizo la mwanaume kukosa hamu ya tendo la ndoa.

Ni vyema ukajihoji kama uhusiano wako na mwenza wako upo sawasawa.

MAZOEA

Mara nyingine mwanaume anaweza akawa katika uhusiano kwa muda mrefu kiasi ambacho amemzoea mwanamke hali inayosababisha mwanaume huyo kukosa hamu ya kushiriki tendo la ndoa. Hili nalo hutokea mara nyingi.

MATUMIZI YA MADAWA YA KULEVYA

Matumizi ya baadhi ya madawa na unywaji wa pombe wa kupindukia huweza kuleta tatizo hili la mwanaume kukosa hamu ya kufanya tendo la ndoa. Madawa yanayochangia tatizo hili ni ya High blood pressure, ya kuondoa msongo wa mawazo, yote yanayozuia ufanyaji kazi au uzalishaji wa Testosterone. Mfano, Cimetidine, Finasteride na Cyproterone.

MATATIZO KATIKA MFUMO WA HOMONI

Tumeshaona kuwa, upungufu wa homoni inayoitwa Testosterone inasababisha kukosa hamu ya kufanya tendo la ndoa. Matatizo mengine katika mfumo wa homoni huchangia tatizo hili.

Kama Thyroid haitoi homoni za kutosha, tatizo hili huweza kutokea ingawa mchango wa Thyroid katika tatizo hili ni mdogo sana. Thyroid ni tezi ya kuzalisha homoni iliyopo katika eneo la shingo.

UMRI MKUBWA

Kiwango cha Testosterone katika mwili wa mwanaume hupungua kwa asilimia 1-2 kila mwaka kadiri anavyozidi kuwa na umri mkubwa. Mara nyingi kuanzia miaka 50 na kuendelea. Homoni ya msingi sana kuhusiana na masuala ya mapenzi huitwa Testosterone. Kwa mwanaume homoni hii hutolewa kwa kiwango kikubwa na korodani na kwa mwanamke hutolewa na Ovari.

Homoni ikipungua katika mwili wa binadamu, humfanya apoteze hamu ya kufanya tendo la ndoa. Kiwango cha Testosterone kikishuka sana katika mwili wa mwanaume huyu humfanya asiwe na nguvu, ashindwe kutuliza mawazo kwenye jambo alifanyalo na apoteze hamu ya kufanya mapenzi.

UCHOVU

Wakati  mwingine uchovu husababisha  mwanaume kukosa hamu ya kushiriki tendo la ndoa. Na ikiwa mwanaume atasongwa na shughuli nyingi zinazochosha mwili, hamu ya kushiriki tendo la ndoa huanza kupungua na ikizidi, baadaye mwanaume atakosa kabisa hamu ya kushiriki tendo na atahitaji uangalizi mkubwa ili arejee katika hali ya kawaida.

Vilevile kukosa mpango mzuri wa shughuli zako za kila siku na kujaribu kulazimisha kufanya mapenzi katikati ya ratiba yako iliyojaa huchangia kukosa hamu ya kufanya tendo.

MSONGO

Msongo ni ugonjwa wa hali ya kuwa na mawazo makali ya muda mrefu ya kukukosesha raha hali inayosababisha kushindwa kuyafanya mambo yako ya kawaida kiufanisi.   Mawazo ya namna hii huathiri mwenendo wako wa maisha pamoja na matamanio yako ya kimapenzi. Itaendelea wiki ijayo.

Leave A Reply