The House of Favourite Newspapers

Elimu haipo kwenye madaftari pekee

0

7.Wanafunzi-wa-Shule-ya-Msingi-Changanyikeni-na-mwalimu-wao-katikati-wakiwa-kwenye-moja-ya-mabanda-yaliyokuwepo-kwenye-maonesho-hayo-wakijisomea-vitabu..jpgWanafunzi wengi wamekuwa wakielekeza akili zao kwenye masomo wanayofundishwa darasani pekee huku wakijisomea kile tu ambacho wanakiandika kwenye madaftari huku wakitegemea kujibia mitihani yao ya mwisho na kufaulu.

Wanafunzi wanaotumia mfumo huo mara nyingi hufeli kwa kuwa hukutana na maswali mengi ambayo hawakujifunza kabisa kutoka kwa walimu wao na kuishia kulaumu walimu hao kwa kutowafundisha mada husika jambo ambalo siyo sawa kwa kuwa tangu mwanzo mwanafunzi anatakiwa afahamu kuwa elimu haipo kwenye madaftari pekee bali huanzia hapo na kuendelea.

Mwanafunzi anatakiwa afahamu kuwa mwalimu anatoa maelekezo tu darasani kama msaidizi (facilitator) wa safari ya mwanafunzi mwenyewe kujifunza zaidi kupitia vyanzo vingine kama mazingira yanayotuzunguka.

Hapo mwanafunzi mwenyewe anapaswa kuhusianisha elimu anayojifunza darasani na mazingira halisi ambayo kimantiki ndiyo humfanya mwanafunzi kuwa na uelewa mpana wa mambo kiasi kwamba anaweza kujibu maswali yake kwa upana zaidi kuliko mwanafunzi ambaye ataishia kusoma madaftari yake tu na kile alichofundisha mwalimu.

Ndiyo maana hata mitaala yetu japo kuwa hali ya uchumi inatuangusha, inaruhusu kwa kipindi fulani mwanafunzi  kujifunza kile alichojifunza kwa darasani kwa kujionea mwenyewe kwa macho yake mazingira husika ambapo zoezi hilo hufanywa kupitia ziara mbalimbali za wanafunzi, maarufu kama ‘Study Tour’.

Study Tour nyingi nchini hutegemea ukaribu wa eneo hilo na mahali wanafunzi walipo ambapo kwa wanafunzi wa Dar huweza kutembelea majengo ya zamani ya biashara ya utumwa yaliyopo Bagamoyo na kutakiwa kujifunza kwa ‘kuobserve’ mada ya Utumwa kwenye somo la Historia. Vivyo hivyo wanafunzi wa nje ya miji wanaweza wakajifunza somo la Jiografia kwa kuwa huwa karibu na mazingira hayo hivyo kutarajiwa kufanya vizuri zaidi katika masomo hayo lakini huwa ni kinyume chake.

Hata hivyo,   kwa mwanafunzi makini huweza kujifunza kwa kupitia mazingira yake siyo tu kwa kutembelea maeneo husika bali hata kwa kuangalia vipindi vya taarifa ya habari, makala za waandishi, documentary, video mbalimbali ambazo ndani yake huonesha mazingira na jinsi watu wanavyoishi.

Mbali na hayo mwanafunzi anaweza akageuza maeneo yoyote kuwa ‘study tour’ yake kwa somo lolote, mfano kutembelea mahakamani ambapo anaweza kujifunza jinsi mahakama zilivyogawanyika nchini kupitia mada ya Court Systems ya somo la Civics na sehemu nyinginezo ambazo kila moja hutoa nafasi ya kujifunza somo fulani.

Leave A Reply