The House of Favourite Newspapers

Kuna Watu Hawapendeki, Wasikuumize Kichwa!

0

KWA uwezo wake Mwenyezi Mungu tumeiona tena Jumatatu hii njema, Mola ametuwezesha tumeweza kukutana pamoja hapa kwenye kilinge chetu cha kupeana elimu ya uhusiano.

Kutokana na jinsi hali ilivyo, ni vyema wapendanao mkachukua hatua za kujilinda na janga hili la Corona.

 

Mlinde mpenzi wako ili naye akulinde wewe. Kumuacha akiwa hayupo salama, hakumaanishi wewe utakuwa salama, bali ni hatari kwako pia. Jukumu la kujilinda ni la kwenu wote wawili, chukueni hatua stahiki.

 

Tukirudi kwenye elimu yetu ya uhusiano, kama mada inavyojieleza hapo juu. Kwenye maisha ya uhusiano wa kimapenzi, kila mmoja anaitafuta amani ya moyo wake. Hakuna mtu ambaye anatamani kuishi kwenye shida za uhusiano.

 

Na katika hali ya kawaida, maisha ya uhusiano yanahitaji kuwa rafiki. Ili muweze kuwa na mafanikio, ni vizuri sana mkawa kwenye ulimwengu ule usiokuwa na makelele. Ulimwengu ambao kila mmoja wenu atafurahia uhusiano wenu.

 

Kinyume na hapo, maisha ya uhusiano wa kimapenzi yatakuwa magumu mno. Yatakuwa ni mateso. Kuishi kwenye mateso kunapunguza hata siku za kuishi. Kuishi kwenye ulimwengu huo ni sawa na kujipalia kaa la moto. Utateseka sana!

 

Bahati mbaya sana, licha ya kuwa kila mtu anakuwa na tabia zake, lakini kwa kweli kuna baadhi ya watu wao huwa ni kama wameumbwa kuwa sehemu ya kero kwa mwenzake. Kuna watu ambao unaweza kusema wao kuwa kwenye makelele au ugomvi ni sehemu ya furaha kwao.

 

anapokaa siku mbili au tatu bila kusababisha jambo ambalo litakutoa kwenye mstari na kukuondolea amani ya moyo, hajisikii raha. Mazungumzo yake siku zote siyo ya kujenga. Zaidi ni kukukera tu ilimradi akuondolee amani ya moyo. Hawa ndiyo watu ambao namaanisha kwamba hawapendeki, hata ufanye nini, huwezi kumbadilisha tabia.

 

Utafanya kila njia ili angalau kuweza kumbadilisha tabia, lakini mwenzako habadiliki chochote. Yeye ni kawaida yake kukukera. Sasa mtu wa aina hii wa nini kuendelea kuwa naye kwenye uhusiano wa kimapenzi? Mtu ambaye yeye hakupi furaha zaidi ya kero wa nini?

 

Watu wa aina hii tupo nao kwenye jamii zetu. Wakati mwingine ni vigumu kuwajua, lakini ni lazima tujifunze kuwabaini mapema. Tuwatambue na ikiwezekana kama hujaingia naye kwenye hatua kubwa kama uchumba na ndoa, basi uachane naye mapema.

 

Mtu ambaye anakuwa si msaada, anakuwa kero huyo ni shida. Unamueleza jambo jema, lakini yeye halimuingii akilini. Jambo ambalo analitamani ni kukupanikisha ili mgombane utadhani vile moyoni anafurahia ugomvi.

 

Ndugu zangu, maisha ya uhusiano yanahitaji utulivu. Kwa kawaida maisha yamejaa shida na changamoto za kila namna hivyo mahali pekee ambapo mtu anatengemea kupata faraja ni kwa mwenza wake.

 

Kama una mwenza ambaye hakupi faraja kila siku, huyo ujue kabisa hakufai. Hakuna sababu ya kuishi kwa kudundana au kutoana ngeu ndiyo maisha yaende, jaribuni sana kuepuka hilo mapema. Kama mtu unaona hakuelewi sera zako, analifanya penzi lenu kuwa uwanja wa vita, basi ujue huyo hafai.

 

Amepoteza sifa na ukimbaini mapema, muepuke. Usijipe presha za bure. Chagua kuwa na amani maishani mwako ili uweze kuishi miaka mingi kwa raha mustarehe.

 

Kwa leo naishia hapa, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri. Unaweza kunifuata kwenye kurasa zangu za mitandao ya kijamii, Instagram na Facebook: Erick Evarist, Twitter: ENangale.

Leave A Reply