Kutokwa na vinyama sehemu za siri (Genital warts) kwa wanawake

imagesKutokwa na vinyama, mafindofindo yanayoota kwenye ngozi au utando laini unaozunguka maeneo ya siri (Genital warts) huwa ni ugonjwa unaoenezwa kwa njia ya kujamiiana na kitaalam huitwa Sexually Transmitted Infection kifupi, kifupi STI.

Ugonjwa huu unaweza kutokea kwenye uke, mrija wa mkojo (Urethra), shingo ya kizazi (Cervix) au maeneo ya kuzunguka njia ya haja kubwa au ndani yake.
Ugonjwa huu husababishwa na jamii ya virusi wanaoitwa kitaalam Human Papilloma Virus (HPV) ambavyo vipo zaidi ya aina 70 tofauti ingawa si wote wanaosababisha maradhi haya ya maeneo ya siri.

Aina nyingine za HPV husababisha kutokwa na vinyama kwenye ngozi inayozunguka sehemu nyingine za mwili kama vile kwenye mikono au miguu.
Baadhi ya aina za virusi wa HPV pia husababisha saratani ya shingo ya kizazi kitaalam huitwa Carcinoma of the cervix kwa wanawake au saratani ya njia ya haja kubwa, kwa jinsia zote mbili.

Ugonjwa huu wa kuota vinyama sehemu nyeti umejitokeza kwa kasi kubwa na watu wengi waliopatwa na ugonjwa huu huwa hawaoneshi dalili zozote zile.

Kwa upande wa wanawake, virusi wa HPV wana uwezo wa kusambaa mpaka maeneo ya ndani kabisa ya kuta za uke au shingo ya kizazi (Cervics) bila dalili kujitokeza.

Kama tulivyoeleza, maambukizi ya HPV husambaa kutoka kwa mtu mmoja mpaka mwingine kwa njia ya kujamiiana kunakohusisha njia ya haja kubwa, uke au ngono ya mdomoni.

Mara baada ya kuambukizwa, huweza kuchukua mpaka muda wa wiki sita hadi miezi sita kwa ugonjwa wa kuota vinyama kujitokeza wazi, ingawa baadhi ya wagonjwa wanaweza kukaa hata miaka kadhaa bila kuwa na dalili yoyote ile.

Watu ambao wanaweza kukumbwa na maambukizi ya ugonjwa huu ni wale wenye wapenzi wengi wanaofanya ngono isiyo salama, kufanya ngono katika umri mdogo na na walio na maambukizi ya virusi wa Herpes na wakati huohuo kuwa na msongo mkali wa mawazo.

Walio na upungufu katika mfumo wa kinga mwilini kwa sababu ya magonjwa mbalimbali au kwa sababu ya matumizi ya dawa fulani wanaweza kupata maradhi haya.

Dalili
Kuota vinyama vidogo au Genital warts huonekana kama vioteo laini vinavyojitokeza juu ya ngozi ingawa wakati mwingine vinaweza kuwa vidogo mno kiasi cha kutoweza kuonekana vizuri kwa macho ya kawaida.

Dalili nyingine ni mgonjwa kuwa na ganzi maeneo yaliyozungukwa ugonjwa na kwa wanawake, uchafu unaotoka sehemu za siri huongezeka na atakuwa anawashwa sana maeneo ya siri na wakati mwingine kutokwa na damu ukeni mara baada ya tendo la ngono, hata hivyo ni kwa baadhi tu ya wanawake.

Kwa upande wa wanawake pia ugonjwa huu hujitokeza ndani ya uke au njia ya haja kubwa, nje ya uke au ngozi ya nje kuzunguka njia ya haja kubwa, au ndani ya uke kuzunguka eneo la shingo ya kizazi.

Uchunguzi wa ugonjwa huu kwa wanawake hujumuisha maeneo ya nyonga (Pelvic Examination) ambapo daktari huchunguza eneo hilo kwa kutumia vifaa maalum vinavyomuwezesha kuona uwepo wa maradhi haya na wapi vilipo.

Wakati mwingine daktari anaweza pia kufanya kipimo cha Pap Smear kwa ajili ya uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi. Kwa wanaume, huchunguzwa maeneo ya siri ili kuona kama kuna vinyama hivi vimejitokeza.

Itaendelea wiki ijayo.


Loading...

Toa comment