The House of Favourite Newspapers

Kuzimu Na Duniani-11

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
“Hiyo sasa si kazi yako kujua. Baada ya kuchukua vivuli kazi yako itakuwa imeisha mara moja. Wewe nenda.”
Niligeuka na kutembea kwa masikitiko sana. Nilijua nikishachukua vivuli, wahusika watakata roho palepale na ndiyo maana pia hawakutaka kuniambia.
SASA ENDELEA:

Niliingia hospitali huku nikikumbuka masharti yote, hivyo wakati naingia, nikageuka na kutembea kinyumenyume. Nilipishana na nesi mmoja akiwa amebeba mfuko wa rambo.
Nikapita hadi kwenye wodi moja ya wagonjwa wanawake wenye watoto. Pia nikaingia kinyumenyume. Nikasimama katikati ya wodi. Wagonjwa wote walikuwa vitandani, wengine macho, wengine usingizini. Waliokuwa macho, kuna waliokuwa wakiugulia kwa maumivu, wengine walikuwa macho tu.

Hakuna aliyeonesha dalili kwamba, ananiona mimi pale niliposimama. Nikatembea kumfuata mwanamke mmoja, yeye alikuwa macho lakini mtoto wake alikuwa amelala. Nilipofika karibu yake, nikamnyooshea mkono, nikauchezesha kisha nikaurudisha kwangu.

Nikaenda kwenye kitanda kingine ambacho mama alilala, lakini mtoto wake alikuwa macho na anachekacheka. Niliposogea karibu tu, yule mtoto akaniangalia na kuanza kulia sana. Alilia kwa ukali mpaka nikaogopa.

Kifupi yule mtoto aliniona lakini hakuwa na uwezo wa kusema kwamba anaona nini. Hapa labda niseme tu kwamba, watoto ambao hawajafikia uwezo wa kusema wana uwezo wa kuona viumbe au vitu visivyoonekana. Lakini wakishapewa uwezo wa kusema mama, pale, ile, nataka, ona, huyo anaondolewa uwezo wa kuona visivyoonekana.

Na ili kuwaelimisha kuhusu hili, napenda kuwakumbusha kwamba, mara nyingi mitaani tunakoishi, kuna tabia kwamba, mtoto akipenda kulia sana usiku, baadhi ya imani za watu zinasema hajapenda jina alilopewa.

Wengine wanafikia hatua ya kumbadilishia jina mtoto, watampa la babu yake au bibi kama ni mwanamke au lolote lenye asili ya kabila lake. Wapo wanaosema mtoto analia kwa sababu mizimu imechukia. Hakuna cha mizimu.

Mara nyingi mtoto kulia usiku, sababu kuu ni kuwaona wachawi au majini ndani ya chumba. Mwangalie mtoto anapolia anaangalia wapi. Akikimbiza kichwa ujue anashuhudia maajabu.

Na pia, ili uamini kuwa mtoto analia usiku kwa sababu ya kuona visivyoonekana, ukimbeba na uso wake kuuelekeza ukutani hunyamaza. Kama ataendelea kulia ujue kama ni mchawi amekwenda mpaka ukutani na kumwangalia huku akimtisha.

Jiulize ni kwa nini watoto wadogo kulia ni nyakati za usiku tu? Na ndiyo muda ambao wanga au majini yanazunguka sana.Ila sema majini ni mara chache sana kumliza mtoto kwani wao wana tabia ya kujigeuza na kuwa na sura ya upole na tabasamu laini.

Basi, nilichofanya, nilisimama, nikajishika kichwani, palepale nikawa kama mwanamke mzuri. Nilijiangalia sana. Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kujibadili kuwa mwanamke mrembo.

Yule mtoto akaacha kulia, akaanza kuniangalia na kutabasamu. Mama yake alishaamka wakati huo na alikuwa akimshangaa mwanaye kwa kulipuka na kilio.
Nilimsogezea mkono, nikavuta kivuli, nikageuka, nikaenda kwenye kitanda kingine. Ile nafika tu, mama wa mtoto akakurupuka na kuanza kufoka:

“Umefuata nini wewe? Umetumwa ee? Nesi, huyu mwanaume kaingia ndani ya wodi.”
Nilishtuka sana, nikawa natoka mbio huku nesi akija kwenye kile kitanda na kuuliza yuko wapi?

“Huyo unapishana naye hapo. Huyo anakupita.”
Nesi alisimama na kuangalia huku na kule. Lakini nilimpita kama basi liendalo kasi bila kuniona. Nilipofika nje, nilishtuka sana kuona nimebainika kwenye ile wodi. Tena wakati natoka na yule mwanamke anasema natoka nje, wenzake walikuwa wakinitafuta bila mafanikio.

Niliwakuta wale wamesimama palepale nilipowaacha. Nikiwa nahema kwa nguvu niliwaambia kidogo nikamatwe. Mmoja akasema:

“Tulikuona, tukakuacha. Nani alikwambia ujibadilishe kuwa mwanamke? Wewe huwezi kujibadili mpaka ruhusa yetu. Una bahati sana kwani ilikuwa uuawe palepale lakini tukakuacha. Ila tulikuondolea uwezo kwa sehemu, ndiyo maana aliyeweza kukuona ni yule mwanamke mmoja tu, wengine hawakukuona.”

Niliogopa, nikatetemeka sana. Yule aliyekuwa akiongea, akaniangalia sana kisha akaendelea kuniambia:
“Binadamu mwenye uwezo wa kujibadili ni mchawi tu. lakini kwa yule anayefanya kazi na sisi hana uwezo huo. Uwezo huo tunao sisi, tunaweza kuwa wanawake, wanaume, wazee, vijana, watoto, hata vyovyote vile.”

Niliomba msamaha sana, wakasema wamenisamehe kwa sababu sijaonesha jeuri, lakini walichoamua tangu mwanzo baada ya mimi kujigeuza ni kunisubiri nirudi kisha wanitoe roho nife moja kwa moja.

Lakini akilini nilijiuliza tabu yote ile, kutaka kote kuniua, kwani mimi nitafaidika na nini? Nilibaki kimya kwa muda, nikasema:

“Jamani nina swali muhimu sana kwenu ambalo limenijia baada ya kunisamehe.”
Yule msemaji wao wa tangu awali akaniambia kwa sauti yenye amri.
“Si unataka kuuliza kuhusu utakachopata kwa mambo yota haya?”

Je, wewe msomaji unajua kilichotokea? Usikose kusoma wiki ijayo kwenye gazeti hili.

Leave A Reply