The House of Favourite Newspapers

The angel of darkness – 35

0

Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.

Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna ambao kila mmoja anapitia maisha ya tofauti kabisa na mwenzake. Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anabakia kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.

Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Brianna, yeye analelewa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge baada ya Mashango kufariki dunia kwa kugongwa na gari.

Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.

Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kutaka kuyabadilisha maisha yake na sasa maandalizi ya ndoa yao yamepamba moto. Wanakubaliana wamdanganye mfanyabiashara huyo kwamba wawili hao ni ndugu wa damu wakati ukweli ni kwamba ni wapenzi.

Wawili hao wanahamia kwenye jumba la kifahari la Msuya na hatimaye, Arianna na Msuya wanafunga ndoa ya kifahari na kuacha gumzo kubwa jijini Arusha, wanasafiri mpaka kwenye Visiwa vya Hawaii kula fungate.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

“Usijali Arianna, kukupenda ni jukumu langu na naahidi kukutunza kama mboni ya jicho langu,” alisema Msuya, wakiwa ndani ya chumba kizuri cha hoteli ya Hilton Worldwide, kilichokuwa kimepambwa maalum kwa ajili ya maharusi hao, Arianna na Msuya wakakumbatiana kwa hisia nzito huku msichana huyo akiendelea kutokwa na machozi ya furaha.

Siku hiyo ya kwanza ilipita wawili hao wakiwa fungate, Arianna akawa bado haamini kama kweli hatimaye amekuwa mke halali wa Msuya. Kwake hiyo ilikuwa ni ndoto ambayo hatimaye ilikuwa imetimia, akawa anamshukuru Mungu wake kwa muujiza huo mkubwa aliomtendea.

“Kwa jinsi alivyoyabadilisha maisha yangu, Arianna alikuwa akijihisi kuwa na deni kubwa ndani ya moyo wake ambalo hakuwa akijua ni namna gani atalilipa.
“Mbona unaniangalia kama kuna kitu unachotaka kuniambia Arianna?”

“Sina cha kukwambia Msuya zaidi ya kusema nakupenda sana na nakushukuru kwa jinsi ulivyoyabadilisha maisha yangu,” alisema Arianna, Msuya akamsogelea na kumkumbatia, akambusu kwenye paji lake la uso na kumfanya Arianna asisimkwe sana na mwili wake.

Naye akamkumbatia Msuya kwa nguvu, akawa anahema kwa nguvu kama mtu aliyetoka kukimbia mbio za Marathon. Kila alipokuwa anafikiria dhambi kubwa aliyokuwa anamfanyia Msuya, ya kuendeleza uhusiano wa kimapenzi na Diego, tena ndani ya nyumba yake huku wakimdanganya kuwa ni ndugu, alijihisi kuwa na hatia kubwa ndani ya moyo wake.

Akajiapiza kutafuta suluhu ndani ya moyo wake ili kama ikiwezekana, aukabidhi moyo wake wote kwa Msuya na kumuonesha uaminifu na mapenzi ya hali ya juu. Akaweka nadhiri kwamba watakaporejea Arusha tu, hiyo ndiyo itakuwa kazi yake ya kwanza.

Wakiwa wanaendelea na fungate lao, Msuya alizidi kumuonesha Arianna mapenzi ambayo hakuwahi kuyapata sehemu yoyote, akawa anatamani muda wote amuone akiwa na furaha.

Muda wote wawili hao walikuwa wakigandana kama kumbikumbi, wakienda kuogelea kwenye mabwawa mazuri yaliyokuwa kwenye hoteli hiyo, kukaa ufukweni na kupunga upepo mzuri wa bahari na kukaa kwenye bustani nzuri za maua zilizokuwa hotelini hapo.

Ile hofu aliyokuwa nayo Arianna kwa Msuya, ikawa inazidi kupungua kadiri walivyokuwa wanazidi kukaa pamoja, wakazidi kuzoeana, huku muda mwingine wakitaniana na kucheka utafikiri marafiki waliokutana miaka mingi iliyopita.

Kwa jinsi Msuya alivyokuwa anaonesha kumjali na kumpenda, Arianna hakuwa na hiyana na mwili wake, muda mwingi wakawa wanautumia chumbani wakipeana haki zao za msingi. Hata hivyo, bado kuna tatizo lililokuwa linamsumbua Arianna ambalo hakuweza kuliweka wazi kwa Msuya, hata katika kipindi hicho ambacho tayari alikuwa mkewe.

Arosto ya kutumia madawa ya kulevya ikaanza kumtesa ndani ya moyo wake, siku mbili alizoshinda na Msuya tu bila kujidunga, zilimfanya ajisikie maumivu makali ya mifupa, viungo mbalimbali vya mwili wake na tumbo. Akaanza kuhaha huku na kule juu ya namna ya kupata hata kidogo ili atulize arosto yake.

Hali hiyo ilimfanya amzoee haraka mmoja wa wahudumu wa hoteli hiyo ya kitalii ambapo alipopata upenyo, alimueleza kuhusu alichokuwa anakihitaji. Mhudumu huyo akamwambia kama anaweza kumlipa fedha za kutosha kwa ajili ya kazi hiyo, yupo tayari kuwa anamletea madawa hayo kutoka mitaani kwa siku zote watakazokaa hotelini hapo.

Arianna akamsisitiza kuhakikisha mumewe hajui chochote kuhusu mpango huo. Kwa kuwa fedha hazikuwa tatizo kwa Arianna, alifanikiwa kumpa kiwango cha fedha alichokuwa anakihitaji kijana huyo, akamuahidi kwamba jioni ya siku hiyo atamletea alichokuwa anakihitaji.
Muda ulizidi kusonga mbele huku Arianna akijitahidi kadiri ya uwezo wake kuficha arosto iliyokuwa inamsumbua. Alipokuwa anazidiwa, alikuwa anasingizia kuzidiwa na homa kisha anaenda kulala, jambo lililofanya iwe vigumu kwa Msuya kuelewa nini kinachomsumbua.

Kama walivyokubaliana na mhudumu huyo wa hoteli kubwa ya Hilton Worldwide aitwaye Curtis, jioni alitoka na muda mfupi baadaye alirejea na kuanza kumtafuta Arianna.

Kwa kuwa Arianna naye alikuwa anaujua muda waliokubaliana kukutana, alimtoroka Msuya kwa dakika chache, akakutana na mhudumu yule kwenye korido ya kuelekea kwenye bustani za maua ambapo alimkabidhi mzigo wake kwa ujanja wa hali ya juu kiasi kwamba hata kama kungekuwa na mtu anawatazama, asingeelewa chochote zaidi ya kuwaona wakipishana kwa kasi.

Baada ya kupata madawa hayo, Arianna alirudi chumbani kwao na kwenda kuyaficha sehemu ambayo isingekuwa rahisi kwa Msuya kuyaona, akachukua kete moja na kuanza kutafuta uwezekano wa kujidunga.

“Nahisi tumbo linanisokota sana, ngoja niende msalani,” Arianna alianza kwa kujihami kwa sababu alijua akiingia chooni kwa ajili ya kwenda kujidunga, atachukua muda mrefu. Msuya akamkubalia na kumpa pole bila kujua mwenzake alikuwa na lake jambo.

Arianna akaingia kwenye choo cha ndani kwa ndani na kufunga mlango kwa komeo, akatoa bomba la sindano na yale madawa, akayachanganya kisha kuvuta kwenye bomba la sindano, akajifunga kwa kamba ngumu mkononi na kuanza kutafuta mshipa mkubwa wa damu. Alipoupata, alijichoma ile sindano na kusukumiza madawa yote kwenye mshipa wake wa damu kisha akashusha pumzi ndefu. Harakaharaka akachomoa lile bomba na kulificha juu ya sinki la choo pamoja na masalia ya madawa yaliyosalia.

Akamwaga maji mengi kila sehemu ili kufuta ushahidi kisha akafungulia maji ya ‘bomba la mvua’ na kuanza kujimwagia, madawa yakawa yanazidi kukolea mwilini na kumfanya aanze kubembea, hali iliyomfanya ajihisi kama yupo kwenye ulimwengu mwingine kabisa.

Msuya alishangaa muda unazidi kusonga mbele bila Arianna kutoka chooni, akapatwa na wasiwasi hasa kwa kuwa tayari alishamwambia kwamba anajihisi tumbo linamuuma. Harakaharaka akainuka pale kitandani na kwenda kugonga mlango wa chooni lakini hakuitikiwa, wasiwasi mkubwa ukatanda ndani ya moyo wake.

Alirudia kugonga kwa zaidi ya mara tatu lakini bado hali ilikuwa ileile, mbaya zaidi, mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani. Ikabidi apige simu mapokezi ambapo muda mfupi baadaye, wahudumu wawili walifika kumsaidia, mmoja akiwa na funguo ya akiba ya chooni.

Baada ya kuhangaika kwa dakika kadhaa, hatimaye walifanikiwa kuufungua mlango huo na kumtaka Msuya ndiyo atangulie kuingia ili ajue yupo kwenye hali gani. Akiwa na wasiwasi mkubwa, Msuya alifungua mlango na kuingia, akawa anaangaza macho huku na kule, ghafla macho yake yakatua kwa Arianna.

“Mungu wangu! Arianna! Arianna!” alisema Msuya huku akionesha kuwa na mshtuko mkubwa.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.

Leave A Reply