The House of Favourite Newspapers

Kuzimu Na Duniani-18

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
“Hutakiwi kuweka wazi huu mkakati. Zingatia hilo kwa ajili ya usalama wa uhai wake. Na hii ni amri, wala si maoni yetu,” alisema akafutika.

Nilibaki namwangalia mke wangu, naye akasema:
“Kuanzia leo nimeamua kufunga na kuomba. Itakuwa kwa muda wa siku tatu.”
SASA ENDELEA…

Nilishangaa sana. Sikujua ni kitu gani kilimfanya mke wangu asubuhi hiyo aamke na kusema anaamua kufunga na kuomba tena akiwa anajiandaa kwenda kuchota maji bombani.
“We hufungi?” aliniuliza.

Nikamkatalia kwa kutingisha kichwa. Lakini kabla hajaondoka kwenda kuchota maji, alipiga magoti pembeni ya kitanda na kuanza kusali. Nilimsikia akimwomba Mungu ampe neema ya kuweza kufunga na kuomba kwani kwa nguvu zake kama binadamu hawezi.

Pia alisema ameamua kufunga na kuomba ili magumu yaondoke katika familia maana ahadi ya Mungu inasema mambo magumu hayawezi kutoka isipokuwa kwa kufunga na kuomba.
Baada ya hapo, alibeba ndoo yake na kuondoka huku akiimba nyimbo za Injili. Huku nyuma, wakatokea majini wanawake watatu mbele yangu, wakasimama kisha mmoja wao akasema:

“Ee! Tumesikia mkakati wa mke wako. Tunajua amepewa maono. Lakini hayatamsaidia kitu maana sisi tuna wewe. Tumekuja hapa ili kukupa maelekezo na lazima uyafuate.

“Hakikisha kabla mkeo hajarudi kutoka kwenye maji unafunga mlango ili akija asiingie moja kwa moja mpaka abishe hodi. Kitendo cha kubisha hodi kitamuondolea nguvu ya funga hivyo kwetu atakuwa mwepesi tu kumtendea tulichokwambia,” alisema mmoja wao.

Nilikubali kwa kutingisha kichwa, wakafutika palepale ghafla. Nilibaki natetemeka.
Nilisimama kwenda kufunga mlango kwa lengo la kumfanya mke wangu akija ashindwe kuingia mpaka agonge mlango au abishe hodi kama nilivyoagizwa na wale majini.

Baada ya kufunga mlango nikarudi chumbani, kitandani na kujilaza. Nilijua siku ya mke wangu kufariki dunia ilishafika. Ni dakika tu zilikuwa zikisubiriwa.
Mara, nilimsikia mke wangu akiimba nyimbo zake za Injili huku akiwa ameshaingia ndani. Nilitoka mbio ili kumuuliza amewezaje kuingia wakati nilifunga mlango.

“He! Ulipotoka tu nilifunga mlango, we umeingiaje?” nilimuuliza.
“Sijakuta mlango umefungwa, nimeukuta kama nilivyouacha,” alisema mke wangu huku akionekana kunishangaa sana.

Sikuwa na la kusema. Sasa ningesema nini wakati mtu ameshaingia. Nilijihakikishia mimi mwenyewe kwamba, mlango niliufunga bila wasiwasi wowote ule. Lakini aliingiaje?

Nikasikia sauti ndani ya moyo wangu ikisema: “Unacheza na nguvu za Mungu siyo? Unaulizaje mkeo aliingiaje ndani wakati ulifunga mlango huku ukijua amekutangazia ameanza kufunga?”
Niliogopa, nikazidi kuogopa. Nilichoamini ni kwamba, wale majini wangekuja wakati wowote ule na kunipa maelekezo mengine.

Mke wangu baada ya kutua ndoo ya maji tu, akaingia chumbani. Akaanza kuomba sana huku akipaza sauti. Palepale nilianza kusikia nachomwa moto mwili mzima, kuanzia kichwani hadi kwenye nyayo! Nikajua kumekucha.

Nilikimbilia sebuleni huku nikijishikashika sehemu mbalimbali za mwili kwa kuamini naweza kupunguza ile hali ya kuungua moto! Kweli, kiasi fulani nilijisikia nafuu kuliko nilivyokuwa chumbani.
Nilikaa sebuleni kwa matumaini kwamba, lazima wale majini wangetokea kunipa msaada au kutoa maelekezo mengine lakini wapi! Mke wangu alimaliza kusali, akatoka, akachukua ndoo na kwenda tena kwenye maji.

Sasa nilikuwa najiuliza wale majini watakujaje maana hakuna hata siku moja mimi nikawa na shida halafu nikawafuata huwa wanakuja wenyewe.

Nilisimama na kuingia chumbani, roho ikawa hainipi, nikarudi sebuleni, pia nikaona hakufai nikatoka nje kabisa. Nje nilisimama kama ninayeshangaa jambo lakini ghafla nikasikia sauti za wanawake ndani wakiniita, nikajua wamekuja sasa, nikaenda ndani haraka sana.

Niliwakuta sebuleni watatu, walisimama wakiwa wamechukia sana tena sana. Walinikazia macho pima. Nikajua mimi nimefanya kosa katika maelekezo yao ya awali kuhusu kufunga mlango. Mmoja wao akasema:

“Mke wako anajifanya ana uwezo mkubwa sana kuliko sisi! Ametendewa haki na kuukuta mlango uko wazi. Lakini sisi tunakuhakikishia mpaka inafika saa sita mchana wa leo, hatakuwa hai tena.”
“Sawa,” nilijibu kwa mkato. Mwingine akasema:

“Tunafuatilia hatua kwa hatua kuhusu mke wako. Usije ukaungana naye na wewe ukawa safari moja ya kuiaga dunia. Kuwa mvumilivu kwa litakalotokea. Hatukutaka kumfanyia hivyo mke wako lakini ameonekana kuwa kikwazo kwenye kazi zetu.”

Nilikubali kwa kutingisha kichwa kwamba nimewaelewa vizuri sana. Mara, mlangoni tukasikia sauti ya mke wangu akiendelea kuimba zile nyimbo za Injili, wale wanawake majini wakafutika haraka sana mbele ya macho yangu na kuniacha mimi natetemeka kwa wasiwasi na woga.

Je, wewe msomaji unajua kilichotokea? Usikose kusoma wiki ijayo kwenye gazeti hili.

Leave A Reply