The House of Favourite Newspapers

Kuzimu Na Duniani-4

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

Muda wote huo hakukuwa na mtu aliyekuwa akishuka wala kupanda. Na si kawaida.

“Mimi pale ni kwangu, naishi na mke wangu na mabinti zangu watatu, sina mpangaji wala ndugu mwingine wa kiume. Sasa huyo unayemsema wewe ni yupi?” nilimuuliza kwa sauti yenye maswali kibao.

ENDELEA MWENYEWE…

Basi, labda nitakuwa nimechanganya habari. Kwaheri ya kuonana bwana,” aliniambia huku akiondoka kushuka.

Nilitembea kama hatua tano halafu nikageuka ili kumwangalia vizuri, sikumwona!

“He!” nilishtuka na kuanza kutembea haraka kupandisha kilima ili kuwahi kwenye nyumba.

Nilitokea sehemu ya Kitanzini na safari hii nilisema moyoni kwamba ni lazima niwaambie watu maajabu yale.

Nilisimama sehemu wanayouza matunda na mbogamboga, nikamwona mwanamke mmoja anakuja usawa wangu, moyoni nikasema huyuhuyu nitamwambia.

“Kamwene,” nilimsalimia Kihehe.

“Kamwene mnogage?” alinijibu.

Lakini kabla sijaendelea naye, palepale nikamwambia.

“Unakwenda chini Ipogoro?”

“Ee ndiyo.”

“Kuna mwanamke nimekutana naye hapo kati si wa kawaida.”

“Kakufanyaje?”

“Alikuwa akiongea na mimi lakini ghafla akanipotea machoni. Nadhani ni jini.”

“Sura yake ikoje?” aliniuliza.

“Mweupe hivi.”

“Kama mimi?”

Aliposema kama mimi akajifunua kidogo uso ambao aliuficha kwa kanga. Cha ajabu si kwamba alikuwa kama yeye bali ni yeye yule mwanamke. Nikatoka mbio huku watu wakinishangaa.

Kutokana na utu uzima wangu niliamini kuonekana nakimbia ni aibu, nikasimama na kumwangalia yule mwanamke, hakuwepo pale.

“Kwani we baba unakimbia nini?” muuzaji mmoja wa mboga aliniuliza.

“Kuna mwanamke nilikuwa naongea naye hapo amenitisha.”

“Ulikuwa unaongea na mwanamke hapa sasa hivi?”

“Ndiyo.”

“Kha! Mbona ulisimama peke yako na ukakimbia peke yako!”

Mwanamke mwingine naye akiwa amekaa kwenye kiti akacheka na kusema:

“Ulanzi wa saa hizi nao si mzuri. Mtu unaona unaongea na mtu kumbe upo mwenyewe.”

Nilianza kutembea bila kuwajibu. Nikaenda kutokea kwenye barabara ya Uhindini. Lakini kwa mbele niliwaona wanawake watatu wamesimama, nikaanza kuwaogopa kwa kupita mbali nao.

Mmoja akaninyooshea mkono kama anayeniita, nikamuuliza mimi? Akatingisha kichwa kukubali kwamba ni mimi.

Nilikataa, nikazidi kupita mbali lakini naye akakazana kuniita kwa mkono tena polepole. Ghafla nilijikuta nazidiwa nguvu na kuanza kutembea kama navutwa na sumaku kuwafuata pale walipo.

Nilitembea kwa mwendo wa haraka. Nilipowakaribia, wote waliinama kidogo, wakaweka mikono chini ya magoti yao na kuiunganisha, mimi  miguu yangu ikafikia kwenye mikono hiyo, wakanibeba.

Hawakutembea bali kufumba na kufumbua tulikuwa ndani ya nyumba moja ya kifahari. Tulikaa sebuleni. Lakini kwa haraka sana nikakumbuka kuwa, mahali pale nilikaa siku ile nilipoota ndoto. Nilishtuka sana, nikaogopa.

Wao walikaa kwenye kochi la mbali kidogo na nililokalia mimi. Mara mlango kutoka kwenye chumba kimoja jirani na sebule ukafunguliwa, akatoka mwanamke mwingine akiwa anatembea kuja sebuleni huku akiniangalia na kuachia tabasamu.

“Unanikumbuka?” aliniuliza akikaa.

Nilimkazia macho, nikambaini ni yule mwanamke niliyekutana naye katikati ya mlima akanipotea.

“Umeshanikumbuka sasa?” aliniuliza lakini sikumjibu.

Akajifuta usoni na kuniuliza tena: “Unanikumbuka tena?”

Safari hii sura yake ilikuwa ni ya yule mwanamke niliyekutana naye siku ya kwanza kabisa, tukapandisha wote akaenda kuishia kwenye kichaka akisema ndiyo makazi yake.

“Umenikumbuka sasa?” alisema tena kisha akajifuta tena uso, ghafla akageuka sura. Safari hii alikuwa ni yule mwanamke aliyekuja nyumbani akanichukua kwenye ndoto mpaka nikamwelezea mke wangu.

“Sisi tuna shida kubwa sana na wewe. Tumekuwa tukikufuatilia kwa muda mrefu ni namna gani tutakupata. Mshukuru sana mke wako kwa sababu anasali sana kwa hiyo anakukinga kwa muda mrefu.

“Kazi yetu kwako ni moja tu, tunaomba sana tushirikiane. Lakini ukikataa kwa kukuomba huku tutatumia nguvu yetu ambayo ni kubwa sana. Sawa?” aliniuliza kwa ukali.

“Si sawa,” nilijibu.

“Si sawa kwa nini?”

“Nataka kurudi nyumbani kwangu.”

Waliangaliana wakacheka sana. Mmoja akaniuliza:

“Unajua hapa upo wapi?”

“Si Iringa.”

Je, unajua nini kilitokea? Usikose kusoma wiki ijayo kwenye gazeti hilihili.

Leave A Reply