The House of Favourite Newspapers

Penzi Kabla ya Kifo – 2

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA

Elizabeth Dickson Marcel alikuwa mwanamitindo aliyekuwa na jina kubwa barani Afrika, alifanikiwa zaidi, alibuni mavazi yake mwenyewe na kuyasambaza nchi mbalimbali duniani kiasi kwamba alitengeneza jina na kumfanya kuwa maarufu zaidi ya mwanamke yeyote yule barani Afrika.

SONGA NAYO…

Mara kwa mara alikuwa mtu wa kuonekana kwenye magazeti, maisha yake yaliyojaa vituko yaliwashangaza watu wengi kiasi kwamba hawakujua kitu alichokitafuta kwani kama jina kubwa, alikuwa nalo, kama ni fedha, alikuwa nazo na za kutosha kabisa na kumfanya kuwa bilionea.

Waandishi wa habari hawakumuacha, japokuwa kila siku alisema kwamba anachukia kufuatiliwa na waandishi hao lakini hawakuacha kumfuatilia, kila walipomuona baa akinywa na mwanaume, habari yake iliandikwa, walipomuona akiingia kwenye gari la mwanaume mwingine, pia habari hiyo iliandikwa.

Japokuwa hakuishiwa vituko, lakini Elizabeth alitokea kupendwa mno, watu walimheshimu kwa kuwa alikuwa mtafutaji sana, kichwa chake kilikuwa na akili ya kutafuta fedha, kila alipokaa, alifikiria fedha na hata wanaume alikuwa akitoka nao kimapenzi, ni wale waliokuwa na fedha tu ambao aliamini wangeweza kumpa njia nyingi za kutafuta za fedha hizo.

Kitu kilichowashangaza watu wengi ni kwamba Elizabeth hakuwa mtu wa kuvaa mavazi ya heshima, kila siku alivalia nguo fupi sana, mapaja yalikuwa wazi au kuvaa nguo alizozibuni ambazo zilionesha asilimia tisini ya mwili wake.

 “Huyu Elizabeth anakera sana, anavaa mavazi mafupi tu, yananikera lakini nashangaa nampenda sana na ukiniuliza nampendea nini, wala sijui, mimi nampenda tu,” alisema msichana mmoja, alikuwa shabiki mkubwa wa Elizabeth.

“Hata mimi nampenda sana! Sijali uvaaji wake, hata akitembea mtupu mitaani, wala sijali, mimi nampenda tu,” alisema msichana mwingine.

Kila siku watu mbalimbali waliokuwa na matatizo kiafya walifika nje ya nyumba yake ya kifahari iliyokuwa Mbezi Beach kwa ajili ya kuomba msaada wa fedha ili waweze kusaidiwa na kutibiwa magonjwa yao.

Kutokana na moyo wa huruma aliokuwa nao Elizabeth, hakuwa mbinafsi, kila aliyefika nyumbani kwake, alimsaidia pasipo kuangalia ngozi au tofauti za kidini, kwake, kila mtu alionekana kuwa sawa.

Baada ya kusaidia watu kwa kipindi kirefu, akaamua kuanzisha hospitali kwa ajili ya wagonjwa wa moyo tu. Alijua kwamba mamia ya Watanzania walikufa kutokana na magonjwa ya moyo, hivyo alivyotaka ni kuwa na hospitali ya magonjwa hayo ili wagonjwa watibiwe hapo na si kusafirishwa kwenda India kama ilivyokuwa.

Jina lake lilikua kila siku, wasichana wengi wakampenda na hivyo nao kutamani sana kuwa na umaarufu na akili ya kutafuta fedha kama aliyokuwa nayo Elizabeth. Hakuruhusu jina lake liingie kwenye bidhaa yoyote ile pasipo kupewa fedha, alijua kwamba jina lake lilikuwa biashara kubwa, hivyo akalitumia vilivyo.

Ingawa alikuwa na jina kubwa na utajiri mkubwa lakini mpaka kipindi hicho Elizabeth hakufanikiwa kupata mtoto. Hicho ndicho kilikuwa kilio chake cha kila siku, alijitahidi kuzianika hisia zake katika vyombo vya habari huku akilia lakini hakukuwa na kitu kilichobadilika kabisa.

Alijuta, kuna kipindi alimlaumu Mungu kwamba alimuonea lakini kila alipofikiria kwamba kulikuwa na wanawake waliopata watoto kisha watoto kufariki, akajikuta akibadilisha mawazo yake na kumshukuru Mungu.

Moyo wake uliteseka, usiku alipokuwa peke yake kitandani, muda mwingi alifikiria ni kwa namna gani angeweza kupata mtoto. Alitembea na wanaume wengi, wenye fedha lakini hakufanikiwa kupata mtoto.

Akatembea kwa waganga wengi, kila mtu aliyejitangaza kwamba angeweza kumtibu tatizo lake alimfuata lakini hakukuwa na matumaini yoyote yale. Akaamua kuachana na waganga wa jadi na hivyo kusafiri mpaka Ulaya, huko akafanyiwa uchunguzi, kila kitu kilionekana kuwa sawa, hata madaktari walipoona hashiki mimba walishindwa kufahamu tatizo lilikuwa nini, walishangaa lakini bado msichana Elizabeth hakuweza kupata mtoto.

Je, nini kiliendelea? Fuatilia wiki ijayo.

Leave A Reply