The House of Favourite Newspapers

Kuzimu Na Duniani -6

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

“Swali zuri sana umeuliza. Tunataka kumaliza utaratibu wa Kimungu huko duniani. Hatuko tayari dunia iwe sehemu salama ya kuishi, ikiwa hivyo watu watamsifu Mungu badala ya kutusifu sisi. Hilo hatuko tayari nalo.”
TAMBAA NAYO MWENYEWE SASA…

“Kwa hiyo?” niliwauliza.

“Unaijua vizuri Iringa?”
“Naijua.”
“Tunataka kukupa kata yako. Utakuwa unashughulikia maeneo ya kuanzia Sabasaba, Kihesa, Mtwivila mpaka Mkimbizi pamoja na maeneo yake ya ndani. Maeneo ambayo sijakutajia yana watu wake.

“Kazi yako kubwa itakuwa kuhakikisha unavuruga mfumo wa dawa za binadamu. Lengo letu kubwa zisifanye kazi kwenye mwili kama ilivyokusudiwa. Lakini pia utatakiwa kuhakikisha unatibua mfumo wa amani uliopo.
“Wewe ndiye utakayesimamia ulaji hovyo wa chakula kwa lengo la kuiharibu miili. Yaani binadamu wa maeneo hayo wawe na mfumo mbovu wa ulaji.”

Nahisi walishaniteka kiakili kwani hapo sasa na mimi nilikuwa nakwenda tu bila kukataa wala kuuliza itakuaje mpaka alipomaliza kusema ndiyo akaniuliza kama nina maswali.
“Sina. Labda tu nataka kujua namna nitakavyofanya hiyo kazi nitakuwa naishi wapi?”
“Nyumbani kwako palepale Mlandege.”

“Kwa nini msinipange Kata ya Mlandege?”
“Ina mtu kama nilivyokwambia.”
Nilifurahi sana kusikia nitakuwa nakaa nyumbani kwangu. Kama wangeniambia nitakuwa nakaa kwao katika makazi yale ambayo niliamini ni ujinini.

Jambo moja ambalo kama naliamini ni kwamba, mpaka nafikia hatua ya kuwa mtulivu na kuwasikiliza hata mimi sikuwa mimi. Tayari nilikuwa na tabia kama zao.
“Haya sasa simama ili uingie ndani kwenye chumba maalum kwa ajili ya kusimikwa ili kufanya kazi na sisi,” alisema yuleyule mmoja kati ya wale watatu.

“Nina swali lingine,” nilisema nikiwa sijasimama. Wao walishasimama, hivyo wakakaa kama wanyenyekevu.
“Mimi nitafaidika na nini?”
“Unataka ufaidike na nini?”
“Mimi nataka kujengewa nyumba kubwa nzuri ya kuishi na familia yangu. pia nataka kuwa mfugaji mkubwa lakini sina mtaji.”

“Kama shilingi ngapi?” aliniuliza mmoja wao ambaye si yule wa kwanza aliyekuwa akizungumza na mimi.
Niliwaza haraharaka kisha nikaropoka.
“Shilingi milioni kumi na tano.”

Palepale, yule aliyeniuliza aliinua mkono wake wa kushoto juu. Ukaganda kwa dakika kama moja. Kufumba na kufumbua, mkononi mwake kukawa na mfuko mkubwa kama wa rambo lakini wenyewe mgumu sana. mweupe!
Akanitupia mapajani mwangu. Nilipoangalia ndani nikakutana na noti mpya tupu! Tena zilitoa hadi harufu ya pesa.
“Mnazipata wapi hizi pesa wakati nyie huku hamna viwanda?” niliwauliza.

Waliangaliana kisha mmoja wao akaja na kunishika mkono akanisimamisha. Alianza kutembea na mimi na kuniambia sasa napelekwa kwenye chumba maalum cha kuapishwa na swali langu la wanapata wapi pesa walilipuuza.
Alifungua mlango mmoja, akaingia ndani na mimi nikaingia. Mle ndani mlikuwa na mwanamke au naweza kusema mrembo. Ni mrembo kwa namna alivyokuwa amevaa, sura na rangi yake ya ngozi. Tulikutanisha sura, akaachia tabasamu na kunikaribisha.

“Huyu ana safari ya kwenda kusimikwa. Lakini kabla ya kwenda kule namba 666, hebu msimulie kuhusu maisha yetu na yao duniani maana ameuliza tunapata wapi pesa?” alisema yule mwanamke huku akitoka.
Ni wanawake tupu lakini cha ajabu mambo yao yote yalionesha wanajiamini kupita maelezo. Yaani sijamwona hata mmoja mwenye uso wa wasiwasi wala wa kukata tamaa.

“Karibu ukae,” yule dada alinikaribisha. Akaniuliza:
“Wewe ni mwanamke au mwanaume?”
Nilimshangaa sana.
“Ina maana hata ndevu zangu huzioni?” nilimjibu kwa swali.

“Mimi sijawahi kuona mwanamke wala mwanaume. Ila wote najua wapo. Kuna wengine nimewasaidia bila kujua ni wanawake au wanaume mpaka waliponiambia wenyewe.”
“Haya! Mimi ni mwanaume,” nilisema.
Palepale alisimama na kuzunguka kiti, akaja kunikumbatia na kunibusu huku akilazimisha ulimi wake kuingia kwenye kinywa changu.

“Kuna nini kwani?” nilimuuliza kwa sauti ya wasiwasi.
“Jamni wakija wanaume huku kidogo na mimi naridhika. Wenzangu huwa wanafaidi kidogo maana mara nyingi huwa wanakuja kule duniani,” alisema yule jini mrembo.

“Kwa hiyo unataka nini?” nilimuuliza huku nikiwa nampangua kutoka mwilini mwangu.
“Penzi jamani!” alisema huku akinivutia kwenye kiti chake.
“Kubali kulala na mimi nitakupa siri kubwa ya huku na hutadhurika. Lakini ukikataa lazima madhara yatakupata,” alisema huku akiwa amenikumbatia upya.

Je, unajua nini kilitokea? Usikose kusoma wiki ijayo kwenye gazeti hilihili.

Leave A Reply