The House of Favourite Newspapers

Waziri Aliyekuwa Mchawi -17

0

ILIPOISHIA WIKIENDA

Jambo hilo liliwashangaza sana. Polisi hao wakarudi ndani ya kituo na kwenda upande wa mahabusu walikotoka paka hao ili kujua walitokea wapi.
Walipochungulia ndani ya chumba cha mahabusu ambamo wale wazee wachawi walikuwa wamefungwa hawakuona mtu yeyote. Lango lilikuwa limefungwa vilevile lakini ndani hamkuwa na mtu yeyote.
SASA ENDELEA…

Walichungulia pia katika chumba cha mahabusu wanawake ambako Bi Shali alikuwa amewekwa. Humo pia hawakumkuta bibi huyo.

“Wale vijana walinipigia simu usiku uleule wakanijulisha kuhusu tukio hilo la kutoweka kwa mahabusu hao. Asubuhi hii nimefika na kuona kweli mahabusu hao ambao tulitarajia kuwapeleka mahakamani leo, hawapo,” afisa huyo wa polisi aliniambia.

Maelezo ya afisa huyo wa polisi hayakunishangaza kama alivyoshangaa yeye. Mimi nilikuwa ninajua kuwa wale wazee ni wachawi na ulikuwepo uwezekano wa kujigeuza paka na kutoweka usiku.
Lakini kwa mujibu wa maelezo ya afisa huyo wa polisi, awali aliingia paka mweusi ambaye aliwatoa wenzake. Sikuweza kutambua huyo paka mweusi alikuwa ni mchawi yupi.

“Lakini tutawatafuta,” afisa huyo wa polisi akaniambia.
“Mimi naona muwaache tu, mtasumbuka bure,” nikawaambia nikijua kuwa hata wakiwatafuta wasingewapata tena na wangejitafutia matatizo.

“Naamini wale watu walikuwa ni wachawi kweli,” akaniambia.
Sikutaka tuingie zaidi katika mazungumzo yale ya uchawi, nikamkatisha afisa huyo kwa kumwambia kuwa nilikuwa najiandaa kwa safari ya kurudi Dar.
“Asante mheshimiwa. Safari njema,” akaniambia.
“Asante.”

Nilipomaliza kuzungumza na afisa huyo wa polisi niliendelea kunywa chai. Nilipomaliza nikajiandaa na safari yangu ya kurudi Dar.Ile safari ya siku ile nilipata misukosuko mingi ambayo sikuitarajia.
Kwanza dereva wangu alimgonga mtu. Tukaenda kuripoti kituo cha polisi ambako tulipoteza muda mwingi. Tulipoanza tena safari, tairi moja ya mbele lilipata pancha. Ilikuwa nusura tupinduke.

Dereva wangu alibadili tairi akaweka tairi lingine la akiba. Muda ulikuwa ukizidi kuyoyoma.
Alipofanikiwa kubadili tairi hilo tukaanza tena safari. Tukiwa katikati ya safari yetu, dereva wangu alisimamisha gari ili kupisha msafara wa watu waliokuwa wanakwenda kuzika ambao walikuwa wanavuka barabara.
Mwili wa marehemu ulikuwa umeshikwa mikononi, jambo ambalo halikuwa la kawaida na ulikuwa umefungwa shuka nyeupe.

Hao watu walikuwa wengi ajabu kwani walikuwa hawamaliziki. Walikuwa wakitokea kwenye msitu, wanavuka barabara na kuingia katika msitu wa upande wa pili wa barabara. Tuliendelea kusubiri kwa karibu saa mbili! Watu walikuwa wanaendelea kuvuka barabara tu.
Watu hao walikuwa wanatoka wapi? Nikajiuliza.

Hapo hapo nikagutuka! Pale mahali hapakuwa na kijiji. Palikuwa ni katikati ya msitu. Haikuwezekana kuwe na msafara kama ule wa watu wanaokwenda kuzika.
Jambo jingine lililonishitua ni kuona ule mwili wa marehemu umetokea tena wakati ulishapitishwa. Nilipowaangalia vizuri wale watu walioubeba mwili huo nikashituka nilipomuona Bi Shali na Mzee Mgorozi.
Nikajua pale hapakuwa na watu bali palikuwa na mchezo tunachezewa na kina Bi Shali.
Nikamwambia dereva wangu.

“Unadhani hapa pana watu?”
“Kwani wale ni kina nani?”
“Watu wengi kiasi hiki wanatokea wapi na wanakwenda wapi wakati hapa hakuna kijiji karibu?”
“Hilo nalo ni jambo la kushangaza. Halafu watu wenyewe hawaishi.”
“Hapa tunaweza kukaa hadi kesho.”
“Sasa tufanye nini?”

“Pitisha gari katikati yao, twendezetu.”
“Tutawagonga!”
“Hapa hapana watu, ni miujiza tu. Pitisha gari katikati yao.”
“Unasema kweli.”

“Mimi najua, wewe pitisha gari.”
Dereva akatia gea na kuondoka kidogodogo ili wale watu wampe nafasi.
“Kanyaga mafuta. Pitisha gari palepale. Usiogope!” nikamfokea dereva wangu.
Dereva akanisikiliza. Alikanyaga mafuta na kuipitisha gari katikati ya lile kundi.
Hatukugonga hata mtu mmoja. Lile gari lilipoingia katika lile kundi la watu, kundi hilo lilitoweka ghafla. Hatukuliona tena.

“Alah! Wale watu wamepotelea wapi?” Dereva akaniuliza kwa mshangao wakati gari ikiwa katika kasi.
“Si nilikwambia pale hapakuwa na watu, ni maroroso matupu.”
“Ni kweli ulivyosema, umejuaje?”

“Sote tumezaliwa humuhumu, tutakosa kujua hulka zetu?”
Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda siku ya Jumatatu.

Leave A Reply