The House of Favourite Newspapers

Kuzimu Na Duniani-7       

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

“Kubali kulala na mimi nitakupa siri kubwa ya huku na hutadhurika. Lakini ukikataa lazima madhara yatakupata,” alisema huku akiwa amenikumbatia upya.

SASA ENDELEA…

Nilimuuliza nifanye nini na yeye wakati anajua kwamba kuna mtu ameniingiza kwake. Je, akiniona itakuaje?

“Hilo niachie mimi. Kuna chumba changu hakuna anayeingia zaidi ya mimi mwenyewe,” alisema yule  msichana akionekana kuwa mrembo zaidi ya wale wengine. Hata kwa umri, yeye alionekana ni mdogo kwao. Kwa hiyo, angewezaje kunitunzia uhai wangu!

“Nadhani una wasiwasi na mimi, siyo?” aliniuliza.

“Sana.”

“Kuhusu nini hasa? Labda naweza kukusaidia.”

“Umesema kwamba kama nahitaji usalama wangu nilale na wewe ili wasinidhuru. Ina maana kuna mpango wa kunidhuru?”

“Siwezi kusema kama mpango huo upo au la! Ila nimekwambia lala na mimi ili nikueleze mengi zaidi. Kama hutaki basi tuendelee, nikuelekeze mambo fulani kuhusu duniani.”

Sasa hapo nikahisi kwamba kama kweli kuna mpango wa kunidhuru utaendelea. Kwa hiyo ikabidi nikubaliane naye ingawa pia niliwaza kuwa, huenda ilikuwa ni mtego wake wa kutaka kufanya mapenzi na mimi lakini asinisaidie lolote.

“Hebu tujadili kwanza la mwanzo,” nilisema.

“Lipi?”

“Kulala na wewe ili nisidhurike.”

“Lile lilishapita, basi tena. Kama mpango wa kukudhuru upo upo tu. Huna jinsi. Ilitakiwa palepale useme moja. Ndivyo tulivyoumbwa sisi. Tabia zetu si kama zenu kule duniani.”

Nilishindwa cha kufanya, ikabidi nitulie tu ili nione kinachoedelea. Akaendelea:

Haya sasa, mimi niko na wewe hapa. Tunachotaka sisi huku ni kuifanya dunia kuwa sehemu ya sisi. Wanadamu waishi kama wanadamu lakini maisha yenu yawe chini ya sisi.

Ukweli ni kwamba, dunia ina viumbe wanaonekana lakini pia wapo hao viumbe wakiwa hawaonekani. Wasioonekana ni wengi zaidi kuliko wanaoonekana.

Nilishtuka sana kusikia hivyo, kwamba kuna viumbe wanaoonekana na wasioonekana. Na kwamba wasioonekana ni wengi kuliko wanaoonekana. Mimi hilo nililikataa moyoni kwamba hakuna kitu kama hicho.

Hata kama hukubaliani na mimi lakini huo ndiyo ukweli. Sasa nakusimulia maisha yetu kule duniani. Kwa sasa tupo duniani kwa wingi wetu tukitenda kazi. Wenzetu wanaoishi kule hawana mchezo. Kwa bahati njema sana tumekuwa tukipata urahisi wa kuishi kule.

Imefika hatua tumejenga familia na zinaendelea kuishi. Nataka kukupa mfano mmoja. Kama maeneo unayoishi wewe kuna familia ambayo haina ushirikiano wowote na majirani, wao ni wao. Tambua hao ni sehemu ya sisi bila kujali ni weusi au weupe.

Aliposema hivyo nikakumbuka kwamba, maeneo ninayoishi kuna bwana mmoja anatambulika kwa jina la Myuropu! Huyu bwana Myuropu tulimpa jina kutokana na maisha yake yalivyo.

Ni yeye na familia yake tu, hakuna mtu mwingine. Ana mke na watoto wawili, basi. Hana cha hausigeli wala ndugu. Haendi kwenye misiba ya majirani zake wala hashiriki chochote na majirani hao.

Tumekuwa tukimsema kwamba, siku akifiwa na sisi hatutatokea kwenye msiba wake, akiumwa hatutakwenda kumjulia hali. Lakini hatujawahi kusikia kafiwa wala anaumwa, si yeye, si familia yake.

Asubuhi, mchana, jioni familia ipo ndani. Mara mojamoja sana kuiona inatoka kutembea kwa miguu. Hajulikani anafanya kazi gani wala anapataje pesa za kuendeshea maisha yake. Kwa staili hiyo ya maisha ndiyo maana akapewa jina la Myuropu.

Myuropu maana yake m-Ulaya. Yaani Mzungu. Tumezoea Wazungu ndiyo wana maisha ya wa nyumba ya pili asimjue wa nyumba ya tatu.

Basi, nikaanza kuhisi kwamba huenda Myuropu naye ni miongoni mwa viumbe vilivyoamua kuja kuishi duniani. Ila sasa yule mrembo akanikatisha na kuniambia kitu kingine ambacho kilinitoa kwenye fikra zangu za awali.

Alisema: Wale wanaoishi duniani wako kama nyie. Wanaugua kama nyie na wanakwenda hospitali zenu. Mnapanga nao foleni kama kawaida ili kumwona daktari.

Nilimkatisha kwa swali: Kwa hiyo hapo ina maana kwamba unazungumzia majini sasa?

Akanijibu: Ndiyo haswaa! Nazungumzia sisi mnaotuita majini.

 Akaendelea: Si hivyo tu. Kwa sasa wameenea mpaka imefika mahali wanafanya kazi za kijamii hivyo wanapanda mabasi ya usafiri wa abiria kama binadamu wengine. Hata wewe hapo kule Mlandege unakoishi, umeshawahi kupanda basi ukaa siti moja na jini.

Nilishtuka sana kusikia kauli hiyo. Sikuamini. Ikabidi nivute kumbukumbu nyuma kama nimewahi kupanda basi halafu nikakaa na mtu ambaye nilimtilia shaka, nikajiridhisha kwamba hakuna!

Akaendelea: Sina maana kwamba lazima umkumbuke mtu uliyewahi kukaa naye siti moja. Inawezekana hayupo unayemkumbuka lakini nakuhakikishia yupo uliyewahi kukaa naye. Je, hujawahi kupenda basi halafu ukakaa na mwanamke mmoja akawa anapiga chafya sana mpaka ukawa unakereka?

Aliposema hivyo tu nikalikumbuka hilo tukio. Niliwahi kupanda basi Kihesa kwenda Miyomboni. Ni kweli, kuna mama mmoja nilikaa naye akapiga chafya mara nyingi sana mpaka nikasikia kero, kidogo nimwambie.

Nikamjibu: Ni kweli, naikumbuka siku hiyo. Wewe umejuaje lakini?”

“Kwani unataka nikwambie mambo zaidi ya hapa?” aliniuliza huku akiwa amenitumbulia macho mpaka nikaanza kuogopa.

Je, unajua nini kilitokea? Usikose kusoma wiki ijayo kwenye gazeti hilihili.

Leave A Reply