The House of Favourite Newspapers

Waziri Alipokiri Kuwa Mchawi-18

0

ILIPOISHIA WIKIENDA

Mke wangu akanicheka kwa kuona nilikuwa kigeugeu. 

Sasa tukawa tunakuza mimba ya mtoto wetu. Kila nilipoliona tumbo la mke wangu likizidi kukua nilikuwa nikifurahi. 

Laiti ningejua matatizo ambayo yangekuja kunitokea baada ya mtoto huyo kuzaliwa, katu nisingefurahia mke wangu kupata ujauzito. SASA ENDELEA…

Mwezi uleule ambao mke wangu aliniambia kuwa alikuwa na ujauzito nilimnunulia gari. Niliweza kununua gari hilo kutokana na akiba yangu niliyokuwa ninaiweka kila mwezi kutokana na mshahara wangu pamoja na posho niliyokuwa ninapata.

 Mke wangu alifurahi kupata gari hilo, akawa analitumia kwenda nalo kazini kwake kila siku. Mimi pia nilikuwa nikilitumia katika siku za Jumapili na katika safari zangu binafsi nyakati za jioni na usiku ambao nilikuwa situmii gari la serikali.

Mafanikio yaliyokuwa yamepatikana katika wizara yangu yalinipa jeuri ya kujiona kuwa ninaweza.

Sasa nikawa ninalilia wadhifa wa uwaziri mkuu. Siku zote nilikuwa natamani waziri mkuu huyo afukuzwe kazi niteuliwe mimi kushika nafasi yake. Ile tamaa ya kupata uwaziri mkuu ilikaa katika moyo wangu kwa muda mrefu. Nikafikiria kwamba naweza kutumia uchawi kumuondoa waziri mkuu katika cheo chake na kukipata mimi.

Kulikuwa na mizizi ya kichawi ambayo nilikuwa ninaihitaji na ilikuwa inapatikana kule kijijini kwetu Nzega. Jumamosi moja nikaondoka asubuhi kwenda Tabora kwa ndege. Nilipofika Tabora nikapanda basi lililonipeleka Nzega. Nilipangisha chumba katika hoteli moja ambako nilisubiri hadi usiku.

 Kabla ya kutoka usiku huo nilibadili mavazi yangu nikavaa kama mkulima na si kama waziri mwenye dhamana.

Nilikodi bodaboda iliyonipeleka kijijini kwetu Mbogwe. Nilipofika Mbogwe nilikwenda katika eneo moja la makaburi ambalo lilikuwa limejificha kidogo.

Pale nilitafuta huo mmea niliokuwa nautaka. Mmea huo ulitakiwa uote juu ya kaburi. Kwa kumulika na kitochi kilichokuwa kwenye simu yangu nikaliona kaburi moja lililokuwa limeota mmea huo.

Niliokuwa ninautaka ni mzizi wake. Mzizi wake unakuwa ni mmoja tu usio na matawi na huelekea chini sana.

Nikavua nguo zangu na kuziweka kando ya kaburi kwani mzizi huo ulikuwa na sharti unapouchimba lazima uwe uchi kama mnyama.

 Kwa vile mchanga wa kaburi hilo ulikuwa laini nikaufukua ule mmea kwa mikono.

 Nilipoung’oa ule mzizi sikuvaa nguo zangu, nilikuwa nahitaji kitu kingine, mzizi wa mti ulioota juu ya mti mwingine. Huo mti ulioota juu ya mwingine ulikuwepo kando ya yale makaburi.

Nikaenda kwenye huo mti nikiwa sina nguo. Niliumulikaka mti huo kwa kitochi nikaiona mizizi ya mti uliokuwa umeota juu yake.

Ilibidi nipande juu ili niweze kuing’oa mizizi niliyokuwa naitaka. Nikapanda juu ya ule mti. Wakati nikiwa juu nilitaka nikae kwenye panda iliyokuwa juu yangu ili niweze kuiong’oa vizuri ile mizizi.

Wakati napeleka mkono wangu juu katika ile panda nikaoona ninagusa kitu kama nyanya iliyokuwa inazizima. Nikashituka na kujiuliza nimegusa nini.

 Sikuweza kuona vyema kwa sababu ya kiza na pale sikuweza kuwasha kitochi ili nione. Nikapeleka tena mkono wangu na kuigusa tena. Safari hii niliiminyaminya ili nijue kilikuwa kitu gani.

Kumbe nilikuwa nimegusa nyeti za binaadamu aliyekuwa pale kwenye ile panda.

Nikaona mkono unanishika. Nikakiachia kile kitu nilichokuwa ninakiminya na kushusha mkono wangu.

“Nani wewe?” nikasikia sauti ikiniuliza tena sauti niliyoitambua.

Nikashuka kwenye ule mti haraka. Nilishika mzizi mmoja nikauvuta na kuung’oa.

 “Wewe nani?” sauti hiyo iliniuliza tena

Niliwasha kile kitochi cha simu yangu nikamulika  juu. Nikamuona mzee Mgorozi yuko uchi kama alivyozaliwa akiwa ameketi kwenye ile panda. Sikujua alikuwa akifanya nini.

 Kwa vile hakunitambua na nilikuwa nimeshapata ule mzizi nikaona niondoke haraka.

 Nikafuata nguo zangu nikaanza kuvaa suruali. Wakati navaa macho yangu yalikuwa kwenye ule mti. Nikamuona yule mzee anashuka.

 Nikawahi kuvaa ile suruali harakaharaka, shati nililiweka begani nikatimua mbio.

 “Hebu nisubiri,” Mzee Mgorozi akaniambia huku akinifuata.

Nikajitokomeza kwenye vichaka. Niliisikia sauti yake nyuma yangu ikisema;

“Yule atakuwa ni Meshack.”

Hapo alikuwa amemaanisha mimi. Nikazidi kwenda mbele hadi tukapotezana kabisa, ndipo nilipovaa shati langu.

Baada ya kuvaa shati nilitokea barabarani nikatembea kwa mwendo wa taratibu kuelekea zilipokuwa bodaboda.

Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda siku ya Jumatatu. 

Leave A Reply