The House of Favourite Newspapers

Wananchi wazidi kuibana Tigo

0

tigoMwandisi wetu

KUFUATIA utetezi wa kampuni ya simu za mikononi ya Tigo, juu ya kushindwa kutoa huduma kwa wateja wake siku nzima ya Jumapili iliyopita, wananchi wamezidi kuibana baada ya kauli iliyotolewa na shirika la umma la TTCL kukanusha sababu zilizotolewa na Tigo.

Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu kwa vyombo vya habari, Tigo iliwaomba radhi wateja wake kwa usumbufu uliotokea, wakisema ulisababishwa na kukatika kwa mkongo wa taifa katika sehemu tofauti.

Katika mahojiano na kituo kimoja cha redio jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki, TTCL ilisema kuwa kukosekana kwa huduma za Tigo siku hiyo hakukutokana na kukatika kwa mkongo wa taifa, kwani kama ingekuwa hivyo, mitandao mingine yote nayo ingesumbua, kwani yote hutumia mkongo huo wa taifa.

“Tigo waseme ukweli wa nini kilitokea siku ile, wana matatizo yao ambayo hawataki kuyaweka wazi, kwa sababu suala la kusumbua kwa huduma zao ni la kila mara, sasa kama mkongo ni mmoja na watumiaji ni kampuni zote, kwa nini wao tu ndiyo wawasumbue wateja wao? Waseme kweli juu ya tatizo lao tujue,” alisema mmoja wa wateja waliopiga simu chumba cha habari, Tedds Wane wa Kibamba.

Mwishoni mwa wiki iliyopita watumiaji wa Mtandao wa Tigo walipata shida kubwa baada ya huduma hizo kutopatikana tangu Jumapili asubuhi hadi alfajiri ya Jumatatu, jambo lililowafanya wateja wengi kutaka taasisi hiyo kuchukuliwa hatua na mamlaka za juu kwani ziliwapatia hasara.

Leave A Reply