The House of Favourite Newspapers

Kwa Hili,Tumuombee Jini Kabula!

0

KAMA kiumbe mwenye vinasaba na utoshelezi wa binadamu kamili, hakika nilizipokea kwa masikitiko makubwa mno taarifa za kuugua kwa msanii wa filamu wa muda mrefu, Miriam Nyafulwa Jolwa maarufu kwa jina la Jini Kabula.

Kabula ni miongoni mwa wasanii, wenye mchango mkubwa katika tasnia ya sanaa ya maigizo nchini, huwezi kuitaja tamthiliya iliyotikisha na pengine kuweka rekodi ogopeshi ya Jumba la Dhahabu, bila kumtaja Jini Kabula ambaye kwa hakika ndiye aliibeba.

Katika hili la ugonjwa wa Jini Kabula, ingawa hatujui ni nini haswa kinamsumbua maana tayari watu wameshaanza kujivalisha majoho ya udaktari na kuanza kuutangazia umma aina ya ugonjwa wa msanii huyu nguli, jambo ambalo linakosa uungwana, tusizibe masikio na kuona kama mwenye kustahili ugonjwa na tabu hiyo ni Kabula pekee!

Wito na tarumbeta yangu juu ya hili, Watanzania wote bila kujali utofauti wa kazi zetu, dini, makabila na mambo mengine, tuunganeni kwa imani zetu zote kumuombea Kabula kwa Mungu aweze kupona.

Shetani hajawahi kupendezwa na utimilifu wa afya ya binadamu, hivyo mateso ya kiulimwengu kwetu sisi kama wanadamu, humaanisha raha na kicheko kwake. Mungu ndiye mtetezi wetu dhidi ya muovu huyu ibilisi, mwenzetu Kabula yuko kwenye mahangaiko ya kidunia, tumuombeeni jamani.

Maisha ya binadamu ni kama saa ya mshale, kwamba namba zote zilizoko kwenye saa hufikiwa na mishale yote mitatu, kama si ule wa saa, dakika basi ni ule wa sekunde. Vivyo hivyo kwa binadamu, shida, raha, matatizo, mateso na mahangaiko ni kama mishale ya saa na sisi ni zile namba, lazima tutafikiwa kwa zamu na hakuna mwenye ujanja wa kukwepa uhalisia huo katika uumbaji.YangaMiriam Jolwa ‘Jini Kabula’ na Kocha wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm.

Pole sana Jini Kabula, binafsi naungana na wenzangu kwa imani yangu, kupiga goti na kukuombea kwa Mungu, akupe wepesi na janga hilo la kidunia.

Kwa imani ni kwamba utapona na kurejewa na afya yako tengemi. Wewe si mtu wa kwanza kuugua, haijalishi unaumwa nini, hakuna jipya juu ya ugonjwa wako. Jiamini kwamba wewe ni binadamu na kuugua ni sehemu ya maisha yetu. Je, tupate yaliyo mema tu kutoka kwa Mungu na hata mabaya yasitupate? Hapana Miriam. Unapitia kipindi ambacho kila binadamu mwenye utimilifu wa utu, lazima apite.

Nihitimishe makala haya kwa kuweka kumbukumbu sawa kuwa, hakuna jambo jema ambalo humfurahisha sana Mungu kama kuwajali wenye masumbuko na mateso ya kimwili kama ilivyo kwa Jini Kabula. Tujitokezeni kumjali Jini Kabula, hata kama huna pesa mfukoni, kitendo cha kutenga muda na kwenda kumjulia hali ni zaidi ya kumpa pesa mkononi ambazo kwa kipindi hiki hazina msaada kwake.

Na BRIGHTON MASALU| IJUMAA

UGUA POLE MIRIAM JOLWA, POLE SANA JINI KABULA. TUNA-KUOMBEA KWA WIMO WA MOYO. GET WELL SOON!

Leave A Reply