Kwa Mwanangu nitakayemzaa-23

Baada ya miezi mitatu kupita tangu Abikanile afanyiwe kitendo cha kinyama kwa kubakwa na kina Ruben pamoja na Lass anahisi kuwa ana kila dalili za ujauzito ambapo baada ya kumshirikisha rafiki yake Jesse wanakwenda hospitali alikofanyiwa vipimo na kugundulika kuwa alikuwa na ujauzito wa miezi mitatu.

Jambo hilo linamuumiza sana moyoni Abikanile ukizingatia hakuwa anamfahamu mtu aliyembebesha ujauzito huo, Jesse anamshauri wautoe kutokana na changamoto za maisha ya mitaani, Abikanile anakataa, anasema bora kufa lakini si kuteketeza kiumbe kisichokuwa na hatia yoyote ile.

TAMBAA NAYO…

UPANDE wa pili wa simulizi hii, Alile alikwishaianza kazi ya kumtafuta dada yake Abikanile mtoto wa baba yake mkubwa Aziba, kwa kuwa alikuwa katika likizo ya kufunga muhula wa pili wa mwisho wa mwaka, alipata wasaa mzuri wa kuzunguka mitaani akisaidiana na rafiki yake Max Dean, aliyefikia kwao baada ya kusafiri kutoka Amsterdam hadi Rotterdam kwa ajili ya kazi hiyo.

Kila siku walikuwa mitaani wakizunguka kila kona ya jiji hilo katika sehemu tofautitofauti walikoishi watu wasio na makazi walikofikiri wangeweza kumuona lakini hadi miezi mitatu baadaye, wakati ambao Alile alitakiwa kurudi shule kuendelea na masomo yake walikuwa bado hawajafanikiwa kumuona msichana huyo.

“Sidhani kama hili jambo litafanikiwa!” Max alimwambia Alile wakiwa wamepumzika baada ya kutembea muda mrefu.

“Kwa nini?”

“Tumejitahidi sana, miezi mitatu sasa, lakini bado hatujapata hata fununu yoyote ile!”

Ukweli ni kwamba kazi hiyo ilikuwa ni ngumu sana, ilihitaji moyo wa uvumilivu, Alile alijiapiza kuifanya bila kurudi nyuma na wakati huo aliamua hata kusimama masomo ili aendelee kumtafuta ndugu yake Abikanile.

Siku zikaendelea kusonga mbele, huku kila kukicha Alile na Max wakizunguka kwenye mitaa ya Jiji la Rotterdam wakimtafuta Abikanile lakini hatimaye miezi tisa ikakatika bila kufanikiwa kumpata msichana huyo, Alile akazidi kukata tamaa na wakati huo alikuwa amefikia katika kiwango chake cha mwisho kuamini kuwa ungetokea muujiza akamuona dada yake huyo.

“Hakuna uwezekano wa kumpata Abikanile,” Mzee Davis, baba yake Max aliwaambia siku moja.

Hakuna aliyemudu kuongeza neno lolote, Alile na Max wote waliinamisha vichwa chini, ni kweli walijituma sana kwa muda mrefu kumtafuta Abikanile lakini hakukuwa na matumaini tena na waliwaza kuwa huenda msichana huyo alikwishafariki.

“Max,” Alile aliita kwa sauti iliyojaa upole.

“Nambie Alile.”

“Naomba kesho tukajaribu kwa mara ya mwisho.”

“Bado tu huamini kuwa haiwezekani?”

“Ni vigumu kuamini, lakini naomba kesho tukamtafute kwa mara ya mwisho.”

“Sawa, ila kama tumeshindwa kumpata kwa miezi tisa sidhani kama muujiza unaweza kutokea kesho.”

Usiku huo ulipita Alile akiwa na mawazo mengi juu ya dada yake Abikanile, alikuwa anamuonea sana huruma, mara kwa mara alijiuliza maswali ni kwa nini alikuwa anateseka kiasi hicho lakini hakuweza kupata jibu.

Kulipokucha, kama walivyokuwa wamepanga Alile na Max walijiandaa na baada ya kupata kifungua kinywa walielekea mitaani kama ilivyokuwa kawaida yao na kuanza kuzunguka wakimtafuta Abikanile kila kona walikohisi wangemuona.

Waliendelea kutafuta kwa nguvu zote huku wakiulizia kila mahali walipopita lakini kadiri masaa yalivyokuwa yanayoyoma ndivyo taratibu matumaini yao ya kumpata Abikanile yalizidi kupotea.

“Dada yangu, uko wapi jamani!” Alile aliongea huku machozi yakimbubujika.

Hayo yalikuwa ni majira ya saa kumi za jioni na hakukuwa na dalili yoyote ile ya kufanikisha azma yao hiyo.

“Nyamaza Alile, inabidi tumuachie tu Mungu!”

“Jambo hili linaniuma sana Max.”

“Nafahamu lakini hii yote ni mipango ya Mungu.”

Hakukuwa na namna tena, ilibidi Alile na Max wainuke mahali hapo walipokuwa wamekaa wakipumzika ili waianze safari yao ya kurudi nyumbani.

Kwa mwendo wa taratibu walianza kuzipiga hatua katika mtaa huo wa Northnburg 50 block, kuelekea sehemu ambayo wangepanda treni na kurudi nyumbani kwao Max, wakiendelea kupiga hatua walifika mahali wakauona mkusanyiko wa watu wengi walioonekana kutawaliwa na hamaki kubwa.

“Kule kuna nini?” Alile alimuuliza Max.

“Sijui!”

“Tukashuhudie?”

“Sawa.”

Walielekea eneo hilo kwa mwendo wa harakaharaka hadi walipolifikia kundi lile la watu, wakajitahidi kupenya mpaka mbele yao kabisa kulipokuwa kuna mtu amelala akiwa hajitambui.

Mtu huyo alikuwa anaonekana ni mjamzito, tena alikuwa na mimba kubwa. Mwili wake ulikuwa unaonyesha kudhoofika kuliko kawaida pia nguo zake zilichakaa na kuchanikachanika, pia alikuwa ni mlemavu wa ngozi.

“Mungu wangu!” Alile alisema.

“Nini?” Max alimuuliza.

Lakini msichana huyo hakujibu neno lolote lile zaidi ya kuangua kilio, akapiga magoti na kumkumbatia mtu yule aliyekuwa hajitambui. Kila mtu aliyekuwa mahali pale alipigwa butwaa!

Je, nini kitaendelea? Huyo Alile aliyemuona ni Abikanile? Usikose kufuatilia Jumamosi ijayo.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!


Loading...

Toa comment