The House of Favourite Newspapers

Kwa Mwanangu Nitakayemzaa 26

0

Alile alikuwa bado mitaani akimtafuta dada yake Abikanile akisaidiana na rafiki yake Max Dean, miezi tisa ilipita bila mafanikio yoyote ya kumpata wala kusikia fununu za wapi alikuwa, wakakata tamaa, lakini jambo la kushangaza siku ambayo waliamua kuahirisha rasmi kumtafuta, wakiwa mtaani waliliona kundi la watu, waliposogea kushuhudia nini kilikuwa kimetokea Alile alipigwa butwaa alipomuona msichana mwenye ulemavu wa ngozi akiwa amelala chini hajitambui, akamdondokea na kumkumbatia, watu wote waliokuwa mahali pale walibaki midomo wazi.

TAMBAA NAYO…

BAADA ya Abikanile kuumiza kichwa kwa muda mrefu alipata mawazo ya kuandika barua ili kama ikitokea akajifungua na kupoteza maisha uwe urithi pekee atakaomuachia mwanaye duniani.

Baada ya kutafuta karatasi na kalamu kwa shida na kuvipata msichana huyo alianza kuandika barua huku machozi mengi yakimbubujika ambapo hadi anamaliza kuiandika barua hiyo, uso wake wote ulikuwa umelowana kwa machozi.

Abikanile aliipitia tena barua hiyo zaidi ya mara tatu, maandishi aliyokuwa ameyaandika ndani yake yalikuwa ni ya kuhuzunisha sana, aliamua kufanya hivyo ili kumfikishia ujumbe mwanaye ambaye angemzaa aliyefahamu hakukuwa na mtu mwingine ambaye angeweza kumueleza juu ya historia yake na jinsi alivyopatikana.

Baada ya kuhakikisha kila kitu kiko sawa, aliikunja karatasi hiyo vizuri kisha akaiviringisha kwenye karatasi nyingine aliyoiandika juu yake, ‘Kwa mwanangu nitakayemzaa’.

Akaibusu kwa mapenzi ya dhati, kisha akaiweka kwenye kifua chake ndani ya sidiria.

Kwa tabu Abikanile alijiinua huku akihisi kizunguzungu kisha akaanza kupiga hatua za taratibu kuelekea barabani.

Aliendelea kupiga hatua hadi akafika kwenye makutano ya barabara kubwa iliyokuwa inakwenda kwenye kituo cha treni, lakini tayari alikuwa ameshaishiwa nguvu.

Alishindwa kabisa kuendelea, akadondoka chini jambo lililopelekea watu kujaa baada ya muda mfupi.

***

Alile alizidi kulia kwa uchungu huku akipiga kelele kuwa huyo aliyekuwa amelala mahali hapo alikuwa ndiye dada yake Abikanile ambaye walikuwa wamefanya kazi ya kumtafuta kwa muda wa miezi tisa.

“Una uhakika?” Max Dean aliuliza.

“Ndiyo.” Alile alimjibu.

“Kivipi?”

“Max sihitaji maswali zaidi, ni yeye!”

“Nataka kuhakiki tusipatwe hatia.”

“Ondoa shaka, huyu ni Abikanile.

Max Dean hakupenda kuwa mbishi, aliwaomba msaada watu waliokuwa wamekusanyika eneo hilo kutoa msaada ili kumpeleka Abikanile hospitali.

Bila kupoteza wakati watu walishirikiana na kumkimbiza Abikanile katika Hospitali ya Leiden Medical Center (LMC) alikopokelewa na madaktari ambao kwa haraka walimuingiza kwenye chumba kilichoandikwa mlangoni ICU (Intensive Care Unit) na kuanza kumhudumia.

Lakini hali ya msichana huyo ilikuwa mbaya sana, madaktari walijitahidi kwa juhudi zao zote kuhakikisha wanayaokoa maisha yake lakini walichoambulia ni kufanikiwa kumtoa mtoto, Abikanile  alifariki dunia muda mfupi tu baada ya kumalizika kwa zoezi hilo.

Baada ya kupewa taarifa hizo Alile alilia sana, kwa juhudi alizofanya za kumtafuta dada yake huyo, mtoto wa baba yake mkubwa hakupenda kuamini kuwa huo ndiyo ulikuwa mwisho wake.

Lakini ukweli ni kwamba hakuwa na njia yoyote ile ya kuubadili ukweli, aliamua kuwapa taarifa pia wazazi wake walezi, bwana na bibi Johannes ambao walisafiri hadi katika mji huo wa Rotterdam kwa ajili ya mazishi.

“Hatimaye umeondoka dada, Mungu ailaze roho yako mahala pema peponi. ”

Hayo ndiyo maneno pekee aliyomudu kuyatamka Alile katikati ya simanzi kubwa siku ya mazishi ya Abikanile yaliyofanyikia kwenye makaburi ya familia ya Bwana Davis Dean.

Huo ndiyo ukawa mwisho wa safari ya maisha ya Abikanile duniani. Msichana aliyeipigania mno roho yake na mpambanaji ambaye alikuwa anapinga vikali masuala ya ubaguzi na unyanyasaji wa walemavu wa ngozi (Maalbino) lakini akishindwa kutimiza azma yake baada ya kujiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya.

Baada ya mazishi, familia hizo mbili zilikaa kikao kujadiliana kwa namana gani wangemsaidia mtoto huyo wa kiume aliyeachwa na marehemu, Bwana Johannes na mkewe walijitolea kumlea huku wakimpa jina la Mtima kama barua aliyokutwa nayo Abikanile ilivyoeleza.

Barua hiyo alikabidhiwa Alile, ambaye aliapa kuitunza mpaka pale Mtima atakapokuwa mkubwa na siku moja kumpa ujumbe kutoka kwa mama yake.

Mtoto huyo wa kizungu mwenye chembechembe za ualbino alikuwa anafanana sana na marehemu Abikanile mama yake mzazi.

Baada ya siku arobaini kupita tangu Abikanile azikwe, Alile na walezi wake pamoja na mtoto mchanga Mtima walisafiri hadi Amsterdam yalipokuwa makazi ya bwana na bibi Johannes kwenda kundelea na maisha kama kawaida.

Mtima alitafutiwa mlezi aliyebobea katika masuala ya malezi kwa watoto ili kumuangalia kwa ukaribu zaidi hadi pale ambapo angefikisha umri wa miaka mitatu na Alile aliendelea na masomo yake kama kawaida.

Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia wiki ijayo.

Leave A Reply