The House of Favourite Newspapers

Kwa Mwanangu Nitakayemzaa

0

Historia juu ya maisha aliyoishi Abikanile, mama yake mzazi inamuumiza sana Mtima jambo lililomsababisha aivue roho ya ubinadamu aliyozaliwa nayo na kuvaa ya kinyama akiwa na azma ya kulipiza kisasi kwa kuwaangamiza binadamu kutokana na yale waliyomtendea.

Ili kuikamilisha azma hiyo, Mtima aliunda kundi la kigaidi pamoja na rafiki yake Abdulrahman, liitwalo War Against Blacks, wakaelekea Magadishu, Somalia walikoanza vitendo vyao vya kihalifu kwa kuvamia kwenye Kambi ya Jeshi la Umoja wa Mataifa (Amisom), walikofanya tukio la kutisha mno.

SONGA NAYO…

Taarifa za tukio hilo haraka sana zilifikishwa kwenye vituo vya usalama vilivyokuwa na vikosi vya kupambana na ujasusi, bila kupoteza wakati  wanajeshi na madaktari walimiminwa kwenye Kambi ya Amisom ambako tayari kina Abdulrahman walikuwa wamekwisha tokomea kusikojulikana.

Kambini hapo kulikuwa na maiti nyingi zilizosambaa kila kona pamoja na wanajeshi waliokuwa wameponea chupuchupu, wote walikusanywa, wakaanza kupewa tiba, maiti zilipelekwa kuhifadhiwa kwenye hospitali ya mkoa huo kwa ajili ya kuzisubiri taratibu zingine za mazishi.

Vyombo vingi vya habari viliripoti juu ya tukio hilo la kutisha, watu wakatahadharishwa kuacha kukaa katika makundimakundi pia ulinzi uliimarishwa kwenye maeneo muhimu kama vile hospitalini, shuleni, kwenye vituo vya biashara na usafiri pamoja na kwenye mipaka yote ya kuingia na kutoka Mogadishu.

“Hawa watakuwa Al-Shabaab!” Jinja Muse, kamanda mkuu wa Amisom aliwaambia wenzake.

“Hapana.” mmoja wao alimjibu.

“Kwa nini unakataa?”

“Kamanda lile ni kundi kubwa tofauti na hawa waliokuja wawili tu.”

“Au pengine ni kikundi kipya cha ujasusi?”

“Inawezekana kabisa.”

Mipango madhubuti ilianza kupangwa ili kuliangamiza kundi hilo jipya la ujasusi. Japo lilionekana na kuthibitishwa kuwa liliundwa na watu wawili, umoja wa Amisom haukupenda kulipuuzia maana ulifahamu kufanya kwao hivyo kungewaletea matatizo baadaye wakati litakapokuwa kubwa kiasi cha kuota mizizi kila pembe ya Somalia.

Lakini ukweli ni kwamba juhudi zote hizo hazikuweza kulizuia kundi hilo kuendelea kufanya matukio ya kutisha nchini hapo, kadiri siku zilivyozidi kusonga mbele ndivyo lilivyozidi kutikisa hasa kwa kuua watu wengi bila huruma katika sehemu tofautitofauti.

“Hapa kazi ndiyo imeanza,” siku moja Mtima alimwambia Abdulrahman.

“Kweli kabisa.”

“Damu ya mama yangu iliyomwagika lazima wailipe.”

“Haswaa!”

***

Nchini Uholanzi maisha yalikuwa yanasonga mbele pia huku Alile akimkumbuka na kumlilia Mtima kila siku maana alifahamu kijana huyo hakuwa na maisha marefu tena mbele yake, lakini hakuchoka kumuombea kwa Mungu siku moja abadilike na kuwa miongoni mwa vijana ambao wangekuwa mstari wa mbele kuhamasisha na kupigania haki za walemavu wa ngozi.

Kwa upande wa Destiny, hakuwa anaishi kwa amani baada ya Mtima kuondoka katika maisha yake kutokana na malengo makubwa waliyokuwa wameyapanga tangu utotoni kwao.

Tofauti na malengo hayo, Destiny alikuwa anampenda  sana kijana huyo na moyoni alikwishaweka nadhiri ya kufanya juu chini siku moja waoane na kuishi wakiwa mke na mume.

Mwanzoni baada ya Mtima kuacha shule, Destiny alijitahidi kuvumilia kuwa huenda angezoea kwa kupata marafiki wengine na kumsahau, lakini kadiri muda ulivyokuwa unakwenda ndivyo alivyozidi kugundua kuwa Mtima alikuwa na nafasi kubwa katika maisha yake ukizingatia ni yeye pekee aliyekuwa rafiki yake tangu akiwa mtoto mdogo hadi katika umri huo wa miaka ishirini na mbili.

Kutokana na kuishi maisha ya kipweke yaliyotawaliwa na msongo mzito wa mawazo, Destiny hakuuona tena umuhimu wa kuendelea na masomo, aliacha shule na kurudi nyumbani kwao Kenya kuituliza akili yake kwanza.

Siku, miezi na miaka vikazidi kusonga mbele hatimaye Destiny akaanza taratibu kumsahau Mtima hasa alipopata shughuli ya kufanya baada ya mama yake mzazi Bi Rukia Okelo, balozi wa Kenya nchini Afghanistan, kumfungulia kituo cha biashara kilichoitwa Destiny Supermarket, kilichopata umaarufu kila kulivyokucha.

Ilikuwa ni siku moja tulivu, kabla ya kufika Sikukuu ya Eid El Fitri, kwenye kituo cha biashara cha Destiny kulikuwa kumechanganya, watu wengi walikuwa wanafanya mahemezi kwa ajili ya sikukuu hiyo.

Destiny akiwa anaendelea kusimamia shughuli zake, mara milio ya risasi ilisikika kutoka nje ya supermarket hiyo, hali ya taharuki ikaibuka, watu wakaanza kukimbia ovyo huku wakipiga kelele za kuomba msaada, Destiny naye alitaharuki akatafuta mahali pa kujichimbia ili aiokoe roho yake.

Kufumba na kufumbua, watu wawili waliovaa mavazi mfano wa waasi wa Boko Haram waliingia huku wameshika bunduki mkononi na kuanza kuua watu bila huruma yoyote ile.

Akiwa amejificha Destiny alizidi kuwatazama watu hao kwa makini huku anatetemeka kutokana na uoga aliokuwa nao, bila kutegemea kuna kitu alikiona kwenye mkono wa mmoja wa maharamia hao kilichomshitua sana.

Je, nini kitaendelea? Usikose wiki ijayo.

Leave A Reply