The House of Favourite Newspapers

Kwa nini mimba hutoka mara kwa mara?

0

pregnant_2176694bKWA nini baadhi ya wanawake mimba zao hutoka mara kwa mara? Hili ni swali linaloulizwa na wanawake wengi wanaponipigia simu.

Jibu ni kwamba, mimba kutoka mara kwa mara ni tatizo linalotokea kwa wajawazito ambao mara zote wanakumbwa wakiwa na mimba yenye umri wa chini ya wiki 20 na zikawa zimetoka mara tatu au zaidi.

Mimba hizo kitaalam huitwa Recurrent Miscarriage au Recurrent Pregnancy loss. Karibu asilimia moja ya wanawake wenye uzazi hukumbwa na tatizo hili. Hatari ya tatizo hili huongezeka kadiri umri wa mwanamke unavyoongezeka.

SABABU ZA MIMBA KUTOKA

Kuna sababu nyingi sana za mimba kutoka mara kwa mara kama nitakavyoeleza hapa chini. Kwa mfano kama mwanamke ana matatizo ya mji wa mimba ya kuzaliwa nayo yaani Congenital Malformation. Kizazi huwa hakina umbo au nafasi ya kutosha kuruhusu mtoto akue mpaka kuzaliwa.

Sababu nyingine ni mjamzito kuwa na vivimbe vya mji wa uzazi ambavyo kitaalam huitwa Uterine Fibroids na shingo ya uzazi kulegea, nalo kitaalam huitwa Cervical Incompetence. Kadiri mimba inavyokua, shingo ya uzazi hushindwa kuhimili na hivyo kusababisha mimba kutoka.

Tatizo lingine ni kushikana kwa kuta za mji wa mimba kitalaam huitwa Asherman’s Syndrome au mjamzito kuwa na kisukari au kuwa na ugonjwa wa vivimbe vya Ovari Polycystic Ovarian Syndrome au kuwa na upungufu wa homoni ya tezi shingo Hypothyirodism na mjamzito kuwa na ugonjwa wa Thrombophilia.

DALILI:

Mara nyingi tatizo hili hutokea hasa mimba ikiwa bado changa, dalili zikijionesha wiki ya 10 au kuendelea kidogo. Mimba inayofuata kuharibika huwa katika wastani wa umri uleule wa mara ya kwanza au chini ya hapo kidogo.

Dalili kuu huwa huwa ni kutokwa na damu ukeni, mjamzito kusikia maumivu ya tumbo hasa chini ya kitovu na kiunoni na mara nyingine kutoa uchafu au sehemu ya mimba iliyoharibika.

Wakati mwingine homa na kutapika vinaweza kuambatana na dalili hizo.

Unapopata dalili zinazoashiria tatizo hili wahi uonane na daktari ambaye atakufanyia uchunguzi na vipimo ili kuweza kugundua chanzo cha tatizo hili, ingawa mara nyingine inakuwa ni ngumu kujua chanzo halisi.

MATIBABU

Tatizo hili huleta msongo wa mawazo na kukatisha tamaa kwa wenza walioamua kupata mtoto. Ni muhimu kushirikiana na kutiana moyo kwa karibu.

Karibu robo tatu ya wanawake wanaopata tatizo hili hupata ujauzito wa kawaida bila matibabu yoyote.

Baada ya vipimo na uchunguzi na chanzo cha tatizo kujulikana, basi linaweza kutibiwa kisha tatizo likaisha. Matibabu yanaweza kuhusisha dawa, upasuaji au kushona shingo ya uzazi kama imelegea, kitaalam huitwa Cervical Cerclage.

Wiki ijayo tutakuelezea ni mimba zipi zenye hatari ya kuharibika. Usikose nakala ya gazeti hili.

Dk. Marise anapatikana Marise Dispensary, njia panda ya Mabibo mkabala na kituo cha mafuta.

Leave A Reply