The House of Favourite Newspapers

Kwa nini Umtenge msichana wa kazi? Unajihatarisha

0

ASALAAM alaikum wapenzi wasomaji wangu wote, bila shaka mna afya njema, kwa wale wagonjwa nawaombea dua Mwenyezi Mungu awaponye inshallah.

Basi moja kwa moja, leo kwenye safu hii nimekuja na mada moto inayowahusu wasichana wetu wa ndani ambao tunaishi nao, wasichana ambao wana mchango mkubwa kwenye maisha yetu lakini tunawatenga, utakuta familia inamtengea chombo msichana wa kazi na kumkataza kukaa mezani kula nao.
Hivi nikuulize wewe unayefanya hivyo, je unafanya kazi au ni mama wa nyumbani tu, hata kama ni mama wa nyumbani basi hujui kuwa ule ni mwanzo wa kujihatarisha mwenyewe na kwa watoto wako?
Nasema haya ili niwakumbushe tu kuwa msichana wa kazi anatakiwa kuheshimiwa sana kwani moja kwa moja ndiye anayeendesha maisha yako nyumbani kwa kuwa karibu na wewe, kukupikia, kuwajali watoto wako kwa ujumla.
Nimeamua kuandika mada hii kwa sababu akina mama wengi wana tabia ya kuwatenga wafanyakazi wa ndani, unakuta mama anamwambia msichana asiguse kikombe chake wakati yeye ndiyo anakiosha mara kwa mara, hivi unajuaje ukiwa nje ya nyumba anakufanyia mangapi?
Tubadilike akina mama kwani msichana huyo anao uwezo wa kukuua pia kwa kero tu unazomfanyia.
Kisa hiki kimenifanya niandike haya, embu kisome..
Mama mmoja alinipigia simu na kunilalamikia kuwa amemkuta dada wa kazi na dawa ya kienyeji iliyosagwa kwenye begi lake la nguo alipoamua kumpekua baada ya kuona haelewi mienendo yake.
Anadai kuwa baada ya kumpiga sana yule dada wa kazi, akamwambia kuwa ile dawa alikuwa akiiweka kwenye chakula ili amchukue mume wa bosi wake huyo.
Hivi kwa mfano huu tu utakuwa umejifunza nini? Bila shaka utakuwa umegundua kuwa kuna kila sababu ya kumpenda dada wa kazi na kumfanya rafiki ili hata akitaka kukufanyia jambo baya akuonee huruma.
Wapo hata akina mama ambao hawawapi wasichana wa kazi mshahara wao, hii ni mbaya sana hivi unapomnyima hela na ameshakuwa mtu mzima, akipewa na mumeo je utasema kanisaliti wakati wewe ndiyo chanzo?

Kwa leo naishia hapa tuonane wiki ijayo kwa mada nyingine kali zaidi.

Leave A Reply