The House of Favourite Newspapers

Kwani kuna gharama gani mke akimtii mumewe?

0

blackcouple-bedsmileAMANI ya Bwana iwe nanyi watu wa Mungu. Jumamosi nyingine tunakutana katika kilinge chetu, kupeana elimu katika masuala mbalimbali ya uhusiano. Karibuni marafiki tujifunze pamoja!

Jumamosi iliyopita nilieleza kwa kirefu kuhusu suala la usaliti katika uhusiano. Nilisema, madhara ya usaliti huwa ni makubwa kwa aliyesalitiwa. Nikashauri ni bora usisaliti kabisa maana kovu la usaliti huwa ni gumu kufutika katika akili ya aliyesalitiwa.

Nilisema ni vyema kila mmoja akawa na mtu sahihi, aridhike naye na wajenge familia. Kovu la usaliti lina gharama kubwa kufutika. Unaweza ukaomba radhi na mwenzako akakuelewa lakini asirudishe imani kwako.

Kila wakati atakuwa na wasiwasi na wewe. Anajiuliza kama alikuwa anakuwa anakupa kila kitu na ukamsaliti, kipi cha ziada atakachokufanyia na wewe usimsaliti? Maswali kichwani mwake yatakuwa mengi kuliko majibu hivyo ili kuepusha hayo yote yasitokee, bora usithubutu kabisa kusaliti.

Tukirudi kwenye mada iliyopo mezani, kuna kasumba ambayo baadhi ya wanawake wanayo. Utandawazi umewakolea kwelikweli. Wanataka kuona wanawapanda vichwani wanaume zao. Eti mwanaume ammnyenyekee, amuogope. Amtii.

Anamjibu mwanaume kadiri anavyojisikia. Hataki kuona anazidiwa kitu na mwanaume. Mwanaume akikasirika, akafoka kuhusu jambo fulani, naye anafoka. Anaonesha kwamba hamuogopi, anaweza kumfanya lolote atakalo.

Kujishusha kwake ni mwiko. Anaendesha mapambano na mumewe utafikiri akishinda kuna kombe anapewa. Anataka kuhakikisha mumewe ‘anaufyata’ kwake. Anamjibu kwa nyodo mumewe mbele ya majirani au marafiki zake bila hofu wala woga wa aina yoyote.

Marafiki zangu, hapa suala la msingi ni kujiuliza, kwani kuna gharama gani mke akimtii mumewe? Mke akipamba na mumewe anafikiria nini? Hata kama ni ushindi, ukishamshinda mumeo, halafu nini kitafuata? Wewe uwe mkubwa zaidi ya mumeo?

Ukijishusha, ukimheshimu mume mbona ina maana kubwa zaidi kuliko kutomtii. Itakuwa na faidia ya kiasili lakini pia utakuwa umeenda sanjari na mpango wa Mungu.

Sisemi kwamba mwanaume hapaswi kumheshimu mkewe lakini mke anapaswa kumheshimu zaidi mumewe.

Maandiko matakatifu yanasema, mwanaume atawaacha wazazi wake, naye ataambana na mkewe. Inafahamika kwamba mwanaume ni kichwa cha familia. Anaondoka kwenda kuanzisha familia. Ndiyo maana Biblia imemtaja mwanaume na si mwanamke. Mwanaume ndiye anayeoa na si mwanamke kuoa.

Wewe mwanamke usiyetaka kumtii mumeo unafikiri ni nani zaidi unayepaswa kumtii? Mume ndiyo mtu wako wa karibu baada ya kukuondoa kwa wazazi.

Ndiyo mwenza aliyekutoa nyumbani kwenu na kwenda kuanzisha makao mapya. Ndiye baba atakayelea watoto, hata kama hana uwezo wa kiuchumi lakini ndiye ambaye maandiko au asili ya binadamu inamtaka awe kichwa.

Hata kama kuna sauala la haki sawa lakini linapokuja suala la utii, utapungukiwa nini ukimtii mumeo? Unataka akutii wewe utajisikiaje? Kwa maana nyingine, mtu ambaye ni kichwa, ndiye anayejua mustakabali mzima wa maisha yenu. Mtakula na kuvaa nini, mwanaume ndiye tegemeo.

Ukimtii huyo utakuwa umefanya kosa? Kosa kumtii mtu ambaye ndiye kila kitu katika maisha yako? Ndiye mashine ya kuzalisha kila kitu katika familia. Hakuna gharama yoyote utakayoingia endapo utamtii mumeo. Sanasana utakuwa umetimiza mpango wa Mungu unaosema:

“Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo.

Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno.”-Waefeso 5:21-25.

Leave A Reply