The House of Favourite Newspapers

Kwenda kununua vitafunio huku unapiga mswaki

0

Man-brushes-teeth-on-tubeKuna mijitu bwana ni ya ajabu sana, wakati mwingine unaweza kusema bora hata Mungu asingewaleta hapa duniani. Wanafanya mambo ya ajabu tena ya kukera ambayo siyo ya kiuungwana na kwa kuwa ada yangu ni kunena, sina budi kufanya hivyo.

Kama unafuatilia hii safu, utakumbuka wiki iliyopita niliwapasha wale wanaume wenye tabia za kutoka ndaniĀ  wakiwa wamevalia nguo za ndani almaarufu kwa jina la boksa.

Niseme tu kwamba huo si uungwana na wale wenye tabia hiyo naamini wamenielewa na wataacha mara moja.

neemLakini leo naomba niwazungumzie hawa watu ambao asubuni wanatoka majumbani mwao na mswaki mdomoni kwenda kununua vitafunio. Yaani unakutana na mtu mzima na akili zake, kashika kibakuli au sahani anaenda kununua maandazi au mihogo mtaa wa pili lakini wakati huo huo anapiga mswaki, jamani huu ni uungwana kweli?

Ni ili iweje sasa? Unashindwa nini kutulia kama ni bafuni kwako au uani mwa nyumba unayoishi na kumaliza kupiga mswaki kisha ndiyo uendelee na mambo mengine?

Mbaya zaidi unapotembea huku unapiga mswaki halafu unatematema mate njia nzima, aah jamani! Huu siyo uungwana hata kidogo na ni tabia inayokera mpaka basi.

Hivi kama wewe ndiyo unauza maandazi au vitumbua vyako halafu anakuja mtu huku anapiga mswaki kisha anatema mate pembeni mwa biashara yako, utajisikiaje? Na wateja nao watajisikiaje kama siyo wataona kinyaa na kushindwa hata kununua wanachokitaka?

Naomba niseme kwamba, kuna mambo unapoyafanya ufikirie na wenzako unawaathiri vipi. Sawa unapiga mswaki ili kujiweka nadhifu lakini kuna ulazima gani kutembea huku unafanya hivyo? Unawatia kinyaa wenzako na kama hujui wanakudharau sana.

Siyo uungwana hata kidogo. Busara iko hivi; kama umeamka asubuhi, piga mswaki ukiwa umetulia sehemu moja, jisafishe vizuri kisha ndipo kama unataka kwenda kununua vitafunio uende.

Hili la kwenda mtaa wa pili huku unaswaki, watu watakuona mshamba ambaye unataka watu waone kwamba na wewe huwa unapiga mswaki. Au ndiyo lengo lako? Acha mambo yako bwana! Huo siyo uungwana hata kidogo.

Leave A Reply