The House of Favourite Newspapers

Lazima kieleweke

0

taifa stars_1TAIFA Stars kesho Jumapili inacheza na Malawi ‘The Flames’ kwenye Uwanja wa Kamuzu uliopo Chichiri jijini Blantyre nchini Malawi, ikiwa ni mechi ya marudiano kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2018, Kocha wa Taifa Stars, Charles Mkwasa, amesema: “Lazima kieleweke.”

Mkwasa na vijana wake wataingia uwanjani na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2-0 walioupata Jumatano iliyopita jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Taifa, mabao hayo yakifungwa na Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaochezea TP Mazembe ya DR Congo.

Kabla ya kuondoka jijini Dar es Salaam jana Ijumaa asubuhi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mkwasa aliyepewa mkataba wa miaka miwili kuinoa Taifa Stars, alisema: “Lazima kieleweke, kwani kila kitu kipo poa kuhakikisha tunaitoa Malawi.”

Mkwasa ameliambia Championi Jumamosi kuwa, haijalishi kama wanacheza ugenini kwani amerekebisha vitu mbalimbali katika kikosi chake ili wapate matokeo ya kusonga mbele.

“Washambuliaji wangu kuna kitu nimewaongezea, maana katika mchezo wetu wa kwanza uliona wakikosa mabao mengi kipindi cha pili, hata mabeki wangu yale makosa yao pia nimezungumza nao na sasa wapo vizuri.

“Ninachoahidi hapa ni matokeo yatakayoweza kutuvusha kwani lengo langu ni kusonga mbele bila kutazama matokeo yetu, Watanzania watulie na wajue tunakwenda kupambana kusonga mbele,” alisema Mkwasa.

Ili isonge mbele, Taifa Stars haitakiwi ifungwe zaidi ya bao 1-0 ambapo kama ikifanikiwa kusonga mbele itakutana na Algeria.

Nahodha wa Taifa Stars, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, alisema: “Tupo vizuri, nilivyoiona Malawi na maelekezo ya marekebisho aliyotupa kocha, Watanzania wategemee ushindi.”

Msafara wa Taifa Stars ukiwa na wachezaji 22 na viongozi saba, wakiwemo watu wa benchi la ufundi, uliondoka jana asubuhi kwenda Malawi tayari kwa mchezo wa kesho.

Mechi nyingine za kufuzu Kombe la Dunia 2018 kwa nchi za Afrika zitakazochezwa kesho Jumapili, Kenya itaivaa Mauritius na Ethiopia itacheza na Sao Tome & Princess. Leo Jumamosi, Afrika ya Kati itaivaa Madagascar, Chad vs Sierra Leone na Eritrea vs Botswana.

Leave A Reply