The House of Favourite Newspapers

JPM Aagiza Wananchi Walime Eneo Lililotengwa Makaburi ya Marais na Mawaziri

Rais John Magufuli ameagiza ardhi ya Iyumbu mjini Dodoma iliyotengwa kwa ajili ya kuzikwa viongozi wakuu wa nchi, (marais, mawaziri na viongozi wengine) ianze kulimwa na wananchi kwa kuwa kila kiongozi anataka kuzikwa nyumbani kwao.

 

Rais ametoa agizo hilo leo Desemba 13, 2017 alipokuwa akizindua Mradi wa Nyumba za NHC, Iyumbu mjini Dodoma.

 

“Ardhi ambayo ilitengwa kwa mujibu wa sheria namba 1 ya mwaka 2006, zilikuwa ekari 129. Kwamba patakuwa na eneo la kuzikiwa viongozi, wakati sheria ikipitishwa nilikuwa Waziri wa Ardhi. Viongozi tuliowalenga ni marais, mawaziri na viongozi wengine. Wakati huo sikujua kama nitakuwa Rais, nilisema nitaenda kuzikwa Chato alikozikwa baba.

 

“Nilipowauliza wengine marais wastaafu wakakataa, kila mmoja akasema ataenda kuzikwa kwao, sasa hapa mtamzika nani? Nimeshatoa maagizo hiyo sheria tuibadilishe, wakati tunasubiri kubadili hiyo sheria, natamka hapa kuwa ardhi tuwarudishie wananchi wenyewe. Hivyo wananchi wa Iyumbu anzeni kuilima hiyo ardhi, jengeni nyumba, watakaoitaka waje wawalipe fidia,” alisem Magufuli.

 

Aidha Rais Magufuli amelitaka Shirika la Nyumba (NHC) kuwa makini katika matumizi yao kwani yamekuwa juu sana licha ya kufanya kazi nzuri ya kuboresha makazi na kujenga nyumba za kisasa na zenye ubora.

“NHC jengeni nyumba kila mahali lakini angalieni matumizi yenu. Serikali ya sasa hivi haitoi garantii ya hovyo hovyo. Nataka Shirika la Nyumba (NHC) litimize wajibu wake kwa manufaa ya Watanzania. Ifike mahali baadhi ya hizi nyumba mnazoziuza ziguse maslahi ya Watanzania,” alisema Magufuli.

 

MSIKIE HAPA JPM AKIFUNGUKA

Comments are closed.