The House of Favourite Newspapers

Mwenyekiti Kamati ya JPM ya Makinikia, Muhongo, Ngeleja Kitanzini

0
Spika wa Bunge Job Ndugai akizungumza jambo. Katikati ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson.

KAMATI ya Bunge iliyoundwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai kuchunguza biashara ya madini ya Almasi na Tanzanite imependekeza wajumbe wote wa bodi na waliohusika na kusimamia mgodi wa madini hayo, wahojiwe na ikibainika wamehusika na mapungufu wachukuliwe hatua.

Akisoma ripoti ya kamati hiyo ambayo imekabidhiwa kwa Spika wa Bunge Job Ndugai ambaye naye ameikabidhi kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, mwenyekiti wa kamati hiyo, Mussa Zungu amesema wamebaini madudu mengi.

Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo.

Madudu hayo ni pamoja na upotevu wa kodi, kutosimamiwa vyema kwa uchimbaji wa madini hayo, tofauti kubwa kati ya takwimu zinazotolewa na taasisi za Serikali juu ya kiasi kilichopatikana na kuuzwa cha madini hayo na udanganyifu kuhusu hali na gharama za mitambo.

“Serikali ihoji wajumbe wote wa bodi ya migodi hiyo na wote wanaohusika na ikibainika kuwa walihusika katika mapungufu waliyoyaona wachukuliwe hatua,” amesema.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Kwanza iliyofichua upotevu mkubwa wa mapato katika usafirishaji wa mchanga wa madini (makinikia) kwenda nje ya nchi, Prof. Abdulkarim Mruma (kushoto) akikabidhi ripoti kwa Rais Magufuli wakati Makamu wa Rais Samia Suluhu akishuhudia.

Zungu ameeleza kuwa, Profesa Abdulkarim Hamis Mruma aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya kwanza iliyoundwa na Rais Magufuli kuchunguza kiwango cha madini kwenye mchanga wa madini (Makinikia) anadaiwa kuisababishia serikali hasara kupitia Almasi na Tanzanite akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi wa Madini.

Amesema kuwa Mruma alikiri mbele ya kamati kuwa alishindwa kufuatilia madeni yaliyobambikwa kwa serikali ya Tanzania kwa sababu hakuwa na muda wa kusoma hivyo aliyapitisha madeni hayo kwani aliwaamini waliompelekea taarifa hizo (watendaji wa wizara).

Waziri wa Nishati na Madini wa zamani, William Ngeleja.

Aidha, Zungu amesema kuwa Kamati imebaini kuwa waliokuwa Mawaziri wa Nishati, Prof. Sospeter Muhongo na William Ngeleja walitoa leseni za madini kinyume na sheria huku Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Eng. Edwin Ngonyani akiwa STAMICO alishindwa kusimamia utekelezaji wa majukumu yake kwa ufasaha.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa kesho saa 4:30 asubuhi atamkabidhi Rais Magufuli ripoti mbili za uchunguzi wa biashara ya Almasi na Tanzanite alizokabidhiwa leo na Spika Ndugai.

FUATILIA TUKIO HILO

Leave A Reply