The House of Favourite Newspapers

Gazeti Jipya la Michezo, ‘Spoti Xtra’ Lazinduliwa Dar, Mtaani Kila Jumapili- (Video)

Mhariri Mtendaji wa Global Publishers, Saleh Ally, akizungumza na wanahabari.

KAMPUNI ya Global Publishers Ltd wachapishaji wa magazeti ya Amani, Ijumaa, Uwazi, Risasi na Championi imezindua Gazeti  Jipya na Bora la Michezo na Burudani nchini Tanzania linalotambulika kwa jina Spoti Xtra ambalo litakuwa linaingia mtaani kila Jumapili.

 

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhariri Mtendaji wa Global Publishers, Saleh Ally, ameeleza kuwa lengo kubwa la kuanzisha Gazeti la Spoti Xtra ni kukidhi kiu ya wasomaji wa magazeti ya michezo kwani ikizingatiwa Jumapili kunakuwa hakuna Gazeti la Michezo hapa nchini, hivyo wao kama Kampuni wameona ni vyema kuwajali wasomaji wao kwa kuwapelekea Gazeti Bora kila Jumapili ili wasikose kile wanachokihitaji wasomaji tena kwa wakati muafaka.

Mhariri Mkuu wa Spoti Xtra, Michael Momburi.

“Tumefanya tafiti nyingi ili kuona nini kinakosekana kwenye michezo siku ya Jumapili, tukaona ni vyema kuwapelekea Gazeti zuri na bora wasomaji wetu, gazeti litakalokata kiu yao ya michezo. Hivyo tulichofanya, tumeongeza timu ya watu walio bora kwenye upande wa michezo, na ndiyo watakuwa wanaliongoza hilo Gazeti.

 

“Vitu vitakavyokuwa vinaandikwa kwenye Spoti Xtra ni tofauti kabisa na vitu vingine walivyozoea, Spoti Xtra itakuwa ni zaidi ya kile walichokizoea. Tumejipanga vizuri na Gazeti hili litafika hadi vijijini ambako magazeti mengine hayafiki,” alisema Saleh.

Meneja Masoko wa Global Publishers, Franco Ruhinda, akizungumza na wanahabri.

Kwa upande wake Mhariri Mkuu wa Spoti Xtra, Michael Momburi amesema:

“Sisi tumejipanga vizuri kwa upande wa timu, unapotaka kuingiza bidhaa sokoni lazima ufanye tafiti na kubaini nini kinakosekana, hayo tumeyafanya na tumebaini kitu gani kina-miss kwenye soko, wasomaji na wadau wanataka nini siku ya Jumapili. Tumekuja na Gazeti ambalo ni tofauti kabisa na yaliyoko sokoni, tutaleta vitu tofauti.

 

“Tutagusa kila eneo katika tasnia ya michezo, tutaleta wachambuzi mahiri na waliobobea watalichambua soka kwa makini. Takwimu zote za soka kuanzia Ulaya, Afrika na Tanzania zitakuwepo tena kwa ubunifu wa hali ya juu,” alisema Moburi.

Gazeti la Spoti Xtra litakuwa mtaani kila Jumapili, na litaanza rasmi kutoka kuanzia keshokutwa Jumapili, Desemba 17, 2017. Kaa mkao wa kula! Spoti Xtra, Hapa ni Uhondo Tu!

Comments are closed.