Mabilionea Wasio na Huruma 44

us-dollarsMABILIONEA wawili, Dk Viola na nduguye Vanessa, wanatafutwa kila kona ya dunia kwa mauaji ya watu wengi waliowaibia figo zao miilini na kuziuza kwa bei kubwa na mwisho wakaangusha ndege iliyokuwa imebeba abiria zaidi ya mia mbili, sitini na mbili wakiwa ni watoto yatima kutoka kwenye kituo cha watoto yatima kilichoanzishwa na Dk Viola.

Fidia yote ya watoto 62 ambayo ilikuwa ni dola milioni kumi kwa kila mtoto, ilikwenda mikononi mwa Dk Viola, kwani wiki mbili kabla ya ajali hiyo, aliwawekea watoto hao bima na kujitaja yeye kama mrithi wa mafao likitokea jambo lolote, kiasi hiki cha fedha kimewafanya wazidi kuwa matajiri kwa fedha haramu.

Uchunguzi ulipofanyika, ulibaini kuwa Vanessa ambaye alikuwa Mhandisi wa Ndege wa Shirika la Ndege la Brito Africa Airline iliyoanguka na kuua abiria hao wote, alitega vifaa vya mlipuko na kuviseti vilipuke ndege ikiwa imeruka kutoka Tanzania kurejea Uingereza, baada ya tukio hilo tu aliacha kazi na kurejea Afrika ambako yeye na ndugu yake wamepotea.

Inspekta Masala, mpelelezi maarufu duniani, amekabidhiwa jukumu la kuwatafuta Dk Viola na Vanessa popote duniani, amepewa pia jumla ya wapelelezi wanne wa kushirikiana naye lakini akiwa nchini Thailand katika Jiji la Bangkok, wapelelezi wote hao wameuawa katika mazingira ya utatanishi, si wao tu bali pia daktari aliyewafanyia Dk Viola na Vanessa upasuaji wa kuwabadili sura.

Picha inaonyesha wazi kuna mtu anafanya mauaji hayo na amembakiza Inspekta Masala peke yake ili amalize kazi, anachokihitaji kwa sasa hivi Inspekta Masala ni sura za Dk Viola na Vanessa baada ya kufanyiwa upasuaji, anazipata picha zao kwa mwanaume aliyebadilisha jinsia na kuwa mwanamke (Jen) ambaye hata hivyo amepigwa risasi Inspekta Masala akiwa bafuni.

Akiwa njiani kutoka nyumbani kwa Jen, Inspekta Masala anakuta barabara imezibwa kwa magari, akijua hiyo ni hatari alichomoa bastola yake na kujiweka tayari kwa mapambano, lakini kabla hajafanya lolote taa kali zilizokuwa zikimulika zilizimwa na kuanza kumulikwa kwa tochi akiwa bado yuko ndani ya gari.
Je, nini kitaendelea?SONGA NAYO…

“SHUKA!” ilikuwa ni sauti ya kukwaruza, Inspekta Masala akihisi mdomo wa bastola ukimgusa kwenye paji la uso.
“Ninyi ni akina nani?”
“Usiulize maswali!”

“Ni vizuri tufahamiane ndugu zangu.”
“Lete hiyo bastola, vinginevyo nakusambaratisha.”
Bila ubishi Inspekta Masala akielewa kabisa kanuni ya bastola kwamba mtu aliyesimama akiwa amekuonyesha bastola yake wewe uliyekaa, ya kwako hugeuka fimbo maana ukijaribu tu kuigusa kwa maana ya kutaka kushambulia, aliyesimama lazima atafyatua risasi na kukumaliza, akakabidhi bastola yake kwa mtu ambaye hata kwa sura alikuwa hawezi kumwona sababu ya mwanga mkali uliompiga usoni.

“Ishiii!” alitoa mlio huo baada ya kusikia kitu chenye ncha kali kama sindano kikizama mwilini mwake, akaelewa kabisa ilikuwa ni sindano, bila shaka ya kulevya ili alale usingizi, moyoni mwake akajua amekwisha.

Haukupita muda mrefu sana macho yake yakaanza kuingiwa na giza na baadaye kupoteza fahamu kabisa, hakujua tena kilichoendelea, jambo lililofanya iwe rahisi sana kwa watu waliomteka kumchukua na kumlaza kiti cha nyuma cha gari lake na mmoja wao akaketi kwenye usukani, safari kuelekea mahali walikofahamu wao ikaanza, Inspekta Masala akiwa usingizini.

“Tumemaliza…tunaelekea ufukweni kukamilisha kazi…amelala…valium siyo mchezo…tukimaliza tu kumtupa majini tutaelekea uwanja wa ndege moja kwa moja…ndiyo…ndiyo…kichwa lazima kiondolewe…sawa mkuu…” Alisikika akiongea kwa simu mwanaume mmoja aliyeketi kando ya dereva kwenye gari la Inspekta Masala, alionekana kuwa ndiye kiongozi wa zoezi hilo.

Simu ilipokatwa mwanaume huyo alitoa maelekezo kwa watu walioketi kiti cha nyuma akiwataka wakamilishe kazi aliyowapa ya kufanya kile alichokiita “Kuondoa ushahidi”, shughuli ikaanza kiti cha nyuma kwa muda wa karibu saa nzima ndipo walipompa taarifa kiongozi wao kwamba kila kitu kilikuwa sawa.

“Weka kwenye mfuko wenye jiwe, tutakitupa majini pamoja na mwili!”
“Sawa mkuu.”

“Huo mwili uwekeni kwenye mfuko wenye jiwe, ili iwe rahisi kuzama!”
“Sawa mkuu.”
Zoezi hilo liliendelea wakati safari ikienda kwa kasi nje kabisa ya Jiji la Bangkok katika kitongoji kiitwacho Patoyo, kilichoko ufukweni kabisa lakini eneo ambalo hakuna mwananchi yeyote aliyeishi. Saa saba na nusu usiku ndiyo waliegesha ufukweni, wote wakashuka na kuubeba mfuko ambao ndani yake kulikuwa na mwili wa binadamu na mtu mwingine akabeba mfuko uliokuwa na kichwa, vyote vikatupwa ndani ya maji na kuzama hadi chini.

“Awe chakula cha samaki,” aliongea kiongozi wao.
“Hakuna mtu atakayeelewa alielekea wapi.”
“Kabisa.”

“Anatakiwa akome kufuatilia mambo ya watu.”
“Ni kweli.”
Walipoona kazi yao imekamilika, waliingia ndani ya gari lao, wakiliacha gari la Inspekta Masala ufukweni, safari kurejea mjini ambako waliwasili baada ya saa tatu ikaanza. Kitu cha kwanza walichokifanya baada ya kuingia kwenye nyumba yao ni kufanya usafi wa gari, kubadilisha nguo na kuchoma kabisa walizokuwa nazo ambazo zilitapakaa damu ili kupoteza ushahidi maana walifahamu ni lazima polisi wangefuatilia tukio hilo.

Wakiwa sebuleni simu ya kiongozi wa zoezi hilo ambaye vijana wote walimwita Tim, mwanaume mrefu mwenye mwili mpana na ndevu nyingi, iliita, akaipokea na kuanza kuongea na mtu ambaye watu wote ndani ya chumba hawakumfahamu, alionekana akipokea maelekezo ya wapi pa kupeleka mzigo aliokuwa nao kwenye gari.
“Fuata anuani niliyokupa!”

“Sawa mkuu.”
“Ukifika kila kitu kitakuwa tayari, ila hakikisheni yupo katika hali ileile!”
“Hilo linafanyika kwa uangalifu wa hali ya juu!”
“Basi bwana Juan Lee, anawasubiri nyumbani kwake na ndege ipo tayari kukuleta wewe na mzigo mpaka Marekani kwa kutumia ndege yake binafsi!” aliongea mtu upande wa pili wa simu.

Alichokifanya Tim baada ya simu hiyo kukatika ni kuwaamuru wenzake wanyanyuke na wote wakaanza kutembea hadi nje ambako waliingia kwenye gari, safari kuelekea nyumbani kwa Juan Lee ikaanza. Aliishi nje ya Jiji la Bangkok, sehemu iliyoitwa Tampo, palikuwa ni mashambani ambako matajiri wachache sana walioaminika kujihusisha na biashara nyingi haramu waliishi.

Nyumbani kwa Lee, lango lilifunguliwa, gari likaingizwa ndani na kuongozwa moja kwa moja hadi sehemu ya nyuma kulikokuwa na uwanja mkubwa wa ndege na hapo paliegeshwa ndege kubwa aina ya Gulfstream 550GS, mali ya bwana Lee ambaye pia alikuwepo kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa.
“Mzigo uko wapi?”
“Kwenye gari.”

“Shusheni.”
Gari ikafunguliwa kwa nyuma na akabebwa mtu aliyeonekana kuwa katika usingizi mzito na kupandishwa mpaka ndani ya ndege ambako bwana Lee aliamuru achomwe tena sindano nyingine ya usingizi kabla ndege haijaruka! Zoezi hilo lilipokamilika watu wote walishuka, akabaki Tim na wafanyakazi ndani ya ndege hiyo, ikaiacha ardhi ya Thailand kuelekea Washington, wakiwa wamepanga kutua Amsterdam kwa ajili ya kujaza mafuta.
***
Mita Govan alikuwa ni mvuvi wa siku nyingi sana nchini Thailand, aliendesha maisha yake kwa kazi hiyo na kufanikiwa kusomesha watoto wake mpaka chuo kikuu. Utaratibu wake ulikuwa ni kutega mitego yake usiku na kurejea nyumbani, lakini alfajiri ilikuwa ni lazima arejee tena ufukweni kuangalia kama alikuwa amefanikiwa kunasa samaki yoyote.

Alifika ufukweni saa kumi kamili na kushtuka alipoona gari jeupe likiwa limeegeshwa chini ya miti, moyo wake ukaenda mbio, haikuwa kawaida kuona gari katika maeneo hayo. Haraka akarudi kinyumenyume kisha kwenda kujificha nyuma ya kichaka akijaribu kuangalia kama kuna mtu yeyote angeshuka au kupanda, haikuwa hivyo.

Sababu ya woga alibaki eneo hilo mpaka saa kumi na mbili asubuhi, mwanga wa jua ulipojitokeza ndipo naye akatembea taratibu mpaka kwenye gari hilo na kukuta liko tupu! Alipoangalia ardhini aliona alama za viatu zikielekea kwenye ukingo wa maji karibu kabisa na mahali ambako hutega nyavu zake, akaamua kuzipuuza na kuendelea na kazi yake.

Taratibu akaanza kuvuta nyavu lakini siku hiyo tofauti na nyingine zote alishangazwa na uzito, moyoni akajawa na furaha kuwa huenda alinasa samaki wengi kupindukia! Nguvu zake zote za kuvuta mtego zilishindwa, akaamua kusubiri mpaka wavuvi wengine walipokuja ndiyo wakamsaidia, wote walishtuka walipotoa mtego majini, ndani yake kukiwa na kiwiwili cha mtu bila kichwa.

“Mungu wangu! Inabidi tupige simu polisi!”
“Kabisa, huyu mtu kauawa halafu wamemtupa humu.”

JE, nini kitafuata? Fuatilia kesho katika Gazeti la Championi Jumamosi.


Loading...

Toa comment