The House of Favourite Newspapers

M/kiti wa Tume ya Uchaguzi, shemeji yake Lowassa

0

1.MwenyekitiwaTumeyaTaifayaUchaguziJajiDamianLubuvaakizungumzanawanahabarihawapopichani..JPGMwenyekiti wa Nec, Jaji mstaafu Damian Lubuva

Na Waandishi Wetu

Wakati Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) chini ya Mwenyekiti Mwenza, Freeman Mbowe wakilalamikia uteuzi wa makamishna wapya wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), baadhi ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) nao wamelalamika kuwa Mwenyekiti wa Nec, Jaji mstaafu Damian Lubuva ni shemeji wa Mgombea Urais wa Chadema, Edward Lowassa.

mama reginaMke wa Mgombea Urais wa Chadema, Edward Lowassa, mama Regina Lowassa.

Hali hiyo imezua sintofahamu baina ya vyama hivyo viwili vinavyoonekana kuwa vikuu katika kampeni za urais za mwaka huu ambazo zimebakiza siku 23 tu kabla ya Watanzania kupiga kura kumchagua rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Chanzo chetu makini kimelieleza gazeti hili hivi karibuni kuwa Jaji Lubuva ni shemeji wa Lowassa kwa sababu mkewe Regina, ni motto wa damu wa ndugu yake na mwenyekiti huyo wa Nec.

lowassa na mkewe
Lowassa akiambatana na mkewe.

“Hawa ni ndugu na tuna wasiwasi kwamba anaweza kuweka undugu mbele na kusababisha CCM kukosa ushindi, hili ni jambo linalowezekana,” kilisema chanzo ndani ya CCM.

Wakati chanzo chetu ndani ya makada wa CCM kikidai hivyo, Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila alipohojiwa juzi kama anafahamu kuhusu uhusiano wa watu hao, alipigilia msumari na kudai kuwa anamfahamu Jaji Lubuva na kwamba Regina ni mtoto wa kaka yake, hivyo Lowassa ni mkwewe.

“Hii siyo siri na siyo dhambi, Regina na Lubuva ni mtu na mwanaye, yule ni mtoto wa kaka yake, hivyo Lowassa ni mkwe wake,” alidai Mtikila.

Wakati chanzo hicho

kikilalamikia udugu wa Jaji Lubuva na mke wa Lowassa, Ukawa wamelalamika kuwa uteuzi mpya wa makamishna wa NEC una walakini kwani Rais Jakaya Kikwete ameufanya zikiwa zimebaki siku chache kufanyika uchaguzi mkuu.

Walioteuliwa kushika nyadhifa hizo ni Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mary Longway na Wakili wa Kujitegemea, Asina A. Omari, uteuzi huo ulifanyika siku 52 tangu amteue Mkurugenzi Mpya wa NEC, Kailima Ramadhan Kobwey, Julai 25, mwaka huu.

Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe alitoa tuhuma nzito akimhusisha Rais Kikwete na kile alichoita hujuma zinazoendelea ndani ya Nec.

Mbowe alimtuhumu Rais Kikwete kwa kuwaengua kwa kimizengwe watendaji wakuu wa tume hiyo na kuwapachika wanajeshi pamoja na watu wa Idara ya Usalama wa Taifa kuwa watendaji wakuu.

Alidai kuwa ndani ya miezi miwili iliyopita, Rais Kikwete amevuruga utendaji wa tume hiyo kwa kupachika watu wa kuilinda CCM na wizi wa kura.

“Kwa maana hiyo, Chadema

na Ukawa hawatathubutu kukubaliana na mizengwe yoyote ile itakayotokea kipindi cha uchaguzi na hatutakubali matokeo yanayotia shaka ya aina yoyote ile,” alisema Mbowe hivi karibuni.

Katika mahojiano na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana mara baada ya kikao baina ya NEC na wahariri wa vyombo vya habari, Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema kwamba yeye na Regina Lowassa wanatoka sehemu moja, Kondoa mkoani Dodoma lakini akashindwa kukubali wala kukanusha kuhusu taarifa hizo kwamba wana undugu.

Hata hivyo, alisema hata kama wangekuwa na nasaba, kamwe undugu wao hauwezi kumshawishi akakiuka sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi ili ampendelee Lowassa.

“Wote tunatoka Kondoa lakini nataka niwaambie hawa wanasiasa wenye hofu kwamba hata angekuwa ndugu yangu, kamwe siwezi kupindisha sheria ili nimpendelee mumewe… Tume hii ni huru, kwanza inawezekana vipi niwashawishi makamishna wote hawa eti wafanye upendeleo kwa ajili ya ndugu yangu? Kwa faida ya nani?” alihoji Jaji Lubuva.

Jaji Lubuva alionya kwamba, tuhuma kama hizo ni mbaya katika kipindi hiki cha uchaguzi kwa kuwa zinaweza kujenga chuki kwa jamii kwa kuwa hata kama hazina ukweli, baadhi ya wananchi wanaweza kuziamini, jambo ambalo ni la hatari.

Alisema uchaguzi unaofanyika ni wa Watanzania wote na hauwezi kuharibiwa kwa namna yoyote, ama kwa shinikizo la udugu.

Akizungumza wakati wa mkutano baina ya NEC na wahariri kuhusu tuhuma zilizotolewa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kwamba tume hiyo imejaa maofisa Usalama wa Taifa walioteuliwa hivi karibuni na Rais Kikwete maalum kwa kuchakachua matokeo, Jaji Lubuva alisema tuhuma hizo hazina msingi na ni za kupuuzwa kwa sababu uteuzi uliofanywa ni wa kawaida na hauhusishi agenda zozote kama wanavyodai wapinzani.

Jaji Lubuva alisema, Rais Kikwete alifanya mabadiliko ya kawaida ikiwemo kujaza baadhi ya nafasi kwenye tume, huku akimtaja aliyekuwa Mkurugenzi wa Tume, Jaji Julius Benedicto Mallaba, kwamba uteuzi wake kama Jaji wa Mahakama Kuu ulikuwa umefika na isingekuwa busara kuiacha nafasi hiyo ambayo hutokea mara chache.

Aliwataka wanasiasa kunadi sera zao na kama wameishiwa sera, hawalazimishwi kuendelea na kampeni, bali wasubiri Oktoba 25, wakapige kura kuliko kuchochea.

Aidha, aliwataka Watanzania wapuuze kauli zilizotolewa na wanasiasa kwamba kuna chama ambacho kimeapa kuingia madarakani hata kwa kutumia ‘goli la mkono’.

“Hakuna goli la mkono wala hakuna short-cut (njia ya mkato). Sisi hatulijui goli la mkono, lazima wanasiasa walielewe hili na wasiwapotoshe wananchi,” alionya.

Jaji huyo mstaafu alisema kwamba, taarifa zinazotolewa na wanasiasa, hasa wapinzani, kwamba kuna njama za kuiba kura ni za upotoshaji na zinaashiria kujenga chuki kwa wananchi ambao wanaweza kuamini yanayosemwa na wanasiasa hao na kuamua kususa kupiga kura.

“Wao wanadhani wanajenga, lakini wanajiharibia hata wenyewe kwa sababu wapo wananchi ambao wanaweza kuamini maneno yao na kuamua kutokwenda kupiga kura kwa kuona hakuna haja tena ikiwa kura zinaibiwa, jambo ambalo linaweza kuwaathiri hata wao wenyewe,” alisema.

Hata hivyo, amewataka wanasiasa hao wanaodai kuna wizi wa kura kwenye tume waende wakaonesha dirisha linalotumika kuibia kura na wao wataliziba kwa nondo na saruji.

Leave A Reply