The House of Favourite Newspapers

Mabilionea Wasio na Huruma 78

1

DUNIA imepatwa na mshtuko mwingine baada ya mabaki ya Padri Silvanio na Sista Mariastela kukutwa ndani ya kisima chao huko Santa Marta, Columbia, watu akiwemo mpelelezi binafsi Denis Crapton aliyeacha uanasheria kwenda kusomea kazi hiyo ili aweze kuchunguza ilikuwaje watawa hao wakaachiwa utajiri mkubwa kiasi hicho uliokadiriwa kufikia dola bilioni mbili na Dk. Viola na nduguye Vanessa waliohukumiwa kifo kwa kudungwa sindano ya sumu.

Denis Crapton baada ya majibu ya DNA kutoka na kuthibitisha kwamba mifupa hiyo ilikuwa ni ya watu aliowaacha nchini Tanzania wakiwa hai, wamerithi utajiri aliotakiwa kurithi yeye baada ya kubadilisha nyaraka, anaamua kupanda ndege hadi Tanzania kuwafuatilia Padri Silvanio na Sista Mariastela bandia.

Anaingia jijini Dar es Salaam na kupanda boti iliyompeleka hadi kisiwani Bongoyo ambako alipewa taarifa ofisini kwa Padri Silvanio na Sista Mariastela kwamba watu hao walikuwa Hoteli ya Kilimanjaro kusaini mkataba wa kuuza kila kitu kabla hawajaondoka nchini Tanzania.

Alichokifanya ni kupanda boti tena na kurejea hadi mjini ambako alikodisha teksi iliyompeleka Kilimanjaro Hoteli, lengo lake likiwa ni kukutana na watu hao kabla hawajaondoka nchini.Je, nini kitaendelea? SONGA NAYO…

TEKSI ilipoegesha kwenye maegesho ya Hoteli ya Kilimanjaro, Denis Crapton alishuka haraka huku akihema kwa nguvu, akili na moyo wake vilikuwa vimejawa na hasira pamoja na chuki dhidi ya watu waliojiita Padri Silvanio na Sista Mariastela, alitaka kufahamu watu hao walikuwa ni akina nani wakati Padri na Sista walishakufa na kutupwa kisimani huko Santa Marta, Columbia.

Hakuna kitu alichotamani kukifahamu kama hicho, fikra zake zilimfanya aamini kulikuwa na utapeli wa aina fulani uliofanyika kwa lengo la kujipatia utajiri ulioachwa na Dk. Viola pamoja na nduguye Vanessa, ambao hata yeye na wakili mwenzake marehemu Mbwambo walishajaribu kutaka kuuchukua kwa dhuluma bila mafanikio, alitamani sana kukutana na hao waliojiita Padri Silvanio na Sista Mariastela.

“Leo ndiyo hatima yao!” aliwaza akitembea kwa kasi kuelekea kwenye mlango mkubwa wa kuingilia hotelini ambako iliwekwa mashine ya kuchunguzwa kwa watu wote walioingia kuona kama walikuwa wamebeba silaha yoyote au la! Akatoa vitu vyote alivyokuwa navyo mfukoni ikiwa ni pamoja na kufungua mkanda na kuviweka kwenye chombo alichopewa, vikapitishwa kwenye mashine na yeye akapita upande wa pili bila mlio wowote kuonyesha alikuwa na hatari.

Akafunga mkanda haraka kisha kuchukua vitu vyake vyote na kuanza kuingia ndani ya hoteli, baada tu ya kuupita mlango wa kufunguka na kujifunga wenyewe uliokuwa mbele ya hoteli, aliibukia kwenye ukumbi mkubwa, macho yake yakakiona kibao kilichoandikwa maandishi ‘Signing of Sale Agreement of Bongoyo Island, going on in the Tanzania conference room, first floor’ yaliyomaanisha kutiliana mkataba wa mauzo wa Kisiwa cha Bongoyo kunaendelea kwenye ukumbi wa mikutano uitwao Tanzania, ghorofa ya kwanza!

Mapigo ya moyo wa Crapton yakaenda mbio, akaisikia kabisa damu ilivyokuwa ikikimbia kwenye mishipa yake, hakutaka kuulizia mahali ilipokuwa lifti baada ya kuziona ngazi za kupandia juu, haraka alianza kukimbia mpaka ghorofa ya kwanza, akakutana na watu kwenye korido, kwa jinsi walivyobeba kamera nyingi alijua ni waandishi wa habari.

“Habari zenu?”
“Ni nzuri, mzima?”
“Mimi mzima tu, naulizia mahali ambako kuna mkataba unasainiwa!”
“Ulikuwa na shida na nani?”
“Padri Silvanio au Sista Mariastela.”
“Duh!”
“Mbona umeguna?”
“Una shida nao ya haraka? Maana unavyohema nahisi kuna jambo la muhimu sana.”
“Ndiyo.”

“Wamemaliza kusaini mkataba dakika ishirini zilizopita na wameondoka kuelekea uwanja wa ndege!”
“Uwanja wa ndege?”
“Ndiyo.”
“Wanasafiri?”
“Wameuza kila kitu na wanaondoka hapa nchini kwenda mahali ambako hawajataka kumweleza mtu yeyote.”

“Mungu wangu!”
“Kwani kuna nini?”
“Acha nijaribu kuwawahi huko uwanja wa ndege.”
“Walisema kwa sababu ya foleni wasingetumia gari, wameondoka na helikopta ya hoteli, kama unataka kuwawahi itabidi utumie helikopta pia.”
“Nitaipata wapi? Acha tu nijaribu,” Denis Crapton aliongea huku akikimbia kuelekea chini na kuwaacha waandishi wakimshangaa.

Alichokifanya baada ya kufika kwenye maegesho ni kuingia ndani ya gari na kumwamuru dereva aendeshe gari kwa kasi akipitia njia za mkato ili waweze kuwahi uwanja wa ndege kabla watu waliokuwa akiwasaka hawajaondoka, aliahidi kumwongezea dola mia moja kwenye malipo yake, dereva akachanganyikiwa kabisa na kuahidi kufika uwanja wa ndege ndani ya dakika ishirini na tano.
“Ishirini na tano?”

“Ndiyo.”
“Nyingi, fanya ishirini.”
“Acha tujaribu.”

Gari liligeuzwa kama limeibiwa na kuendeshwa hadi barabara ya Ohio kunyoosha kuelekea Barabara ya Bibi Titi, mbele kidogo kabla hawajafika Hoteli ya Serena, Denis Crapton aliliona jengo mkono wa kushoto mkabala na jengo la Makao Mkuu ya Posta, akapiga kelele akimwamuru dereva akate kona kuingia kwenye jengo hilo, ilikuwa kidogo tu wagongane na gari jingine, bila umahiri wa dereva huyo wangeweza kufa hapohapo kwani lori la mchanga lilikuwa likija kwa kasi kubwa.

“Subiri hapa.” Alimwambia dereva na kushuka kisha kukimbia hadi mapokezi.
“Vipi kaka mbona unahema?”
“Nina shida.”
“Na?”
“Mkuu wa Interpol hapa makao makuu ya jeshi la polisi.”
“Una ahadi naye?”
“Hapana.”

“Una shida gani?”
“Kuna hii barua nimepewa na polisi wa Columbia nimletee, ni muhimu sana!”
“Andika hapa kisha pandisha ghorofa ya sita, chumba namba 14.”
“Ahsante.”

Akatembea hadi mbele ambako alikuta watu wengi wamesimama kwenye lifti, ilipofunguka wote wakaingia na akawa mtu wa kwanza kubonyeza namba sita, kwa mwendo wa taratibu ikapanda na kusimama ghorofa ya sita, akashuka na kuwaacha wengine wakiendelea, haraka akakitafuta chumba alichoelekezwa na kukipata, hakuhitaji kugonga, alifungua mlango na kuzama ndani.

“Karibu baba.” Ilikuwa ni sauti ya Katibu Muhtasi ambaye alimweleza moja kwa moja sababu ya uwepo wake mahali pale, akanyanyua simu na kumpigia bosi wake,

ilichofuata baada ya simu kukatwa ni kuingizwa chumbani ambako alikutana na askari aliyevalia kiraia, ambaye alijitambulisha kwake kwa jina la Kamishina Hussein Rajab.
“Una uhakika na kilichoandikwa humu?” Kamishna Msaidizi Hussein aliuliza baada ya kusoma barua.

“Ndiyo, mimi ni mpelelezi binafsi, kitambulisho changu hiki hapa ingawa ni kweli nimewahi kufanya kazi ya uanasheria hapa nchini Tanzania miaka michache iliyopita.”
“Nakukumbuka, si ulikuwa unasimamia miradhi ya wale wanawake hatari waliodungwa sindano ya sumu?”

“Ndiyo, bado nafuatilia suala hilohilo, hawa waliokuja hapa na kurithi mali si Padri Silvanio na Sista Mariastela halisi, ni matapeli.”
“Kwa kilichoandikwa kwenye barua hii, ni lazima hawa watu tuwakamate mara moja na kuwafanyia uchunguzi, nifuate.”

JE, nini kitafuata? Watafanikiwa kuwakamata watu wanaojiita Padri Silvanio na Sista Mariastela? Fuatilia kesho katika Gazeti la Championi Jumamosi.

1 Comment
  1. ahady kidehele says

    pambana ijulikane mbivu aumbichi

Leave A Reply