The House of Favourite Newspapers

MABONDIA WA NJE WATUA, KUKIWASHA DAR LIVE

0

 

ZIMEBAKIA siku saba kabla ya kufanyika kwa Mapambano ya Kimataifa ya Ubingwa wa Global TV, Afrika Mashariki na Kati yatakayopigwa Julai 22, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem jijini Dar. Hii ni vita ya aina yake itakayowakutanisha wakali watatu wa Tanzania dhidi ya wageni kutoka katika mataifa ya Malawi, Zambia na DR Congo watakapokuwa wakiwania mikanda ya ubingwa huo ambao umeanza kuvuta hisia za mashabiki wengi wa mchezo huo wanaosubiri kwa hamu kushuhudia mapambano hayo.

Katika mapambano hayo ya kimataifa, yaliyoandaliwa na kampuni ya kupromoti mchezo wa ngumi za kulipwa nchini, Solid Rock Tanzania ambayo yatasimamiwa na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO) chini ya rais wake, Yassin Abdallah ‘Ustaadh’ huku yakirushwa mubashara na Kituo cha Global TV Online.

 

Tanzania itawakilishwa na Francis Miyeyusho ‘Chichi Mawe’, atakayezichapadhidi ya Israel Kamwamba kutoka nchini Malawi, Nasibu Ramadhani anatarajia kuonyeshana umwamba ndani ya ulingo na Mzambia, Benard Mwango huku Idd Pialali akitarajia kupeana vitasa vya aina yake na Regin Champion raia wa DR Congo. Mabondia kutoka njewanatarajia kuingia nchini wakati wowote kwa ajili ya kumalizia maandalizi yao ya mwisho kabla ya kupanda ulingoni kuweza kuwania mikanda hiyo ya Ubingwa wa Global TV, Afrika Mashariki na Kati ambapo mapambano yote yatarushwa mubashara kupitia kituo hicho kinachofuatiliwa na maelfu ya watu duniani kote katika Mtandao wa YouTube.

 

Risasi Jumamosi limefanya mahojiano maalum na Rais wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO), Yassin Abdallah ‘Ustaadh’ ambaye amefunguka kuwa maandalizi kuelekea katika vita hiyo itakayowakutanisha wanaume watatu kutoka katika ardhi ya Tanzania na wenzao kutoka Malawi, Zambia na DR Congo yanakwenda vizuri.

 

“Niwatoe wasiwasi mashabiki wa mchezo wa ngumi hapa nchini na duniani kwa jumla kuwa kila kitu kinakwenda kama kilivyopangwa hasa upande wa maandalizi ya ndani chini ya kamisheni ambayo inaongozwa na mimi mwenyewe.

 

“Mabondia wetu wapo katika kambi zao wakiendelea na mazoezi makali ya kuhakikisha wanafanya vizuri katika mapambano hayo kwa sababu hao ndiyo wawakilishi wa chini yetu, nimeambiwa kati yao wamekuwa wakifanya mbio ndefu katika Jiji la Dar, wanatoka kwenye maeneo ya kambi zao hadi Kariakoo, Ilala na Buguruni kwa lengo la kuongeza pumzi. “Wengine wamekuwa wakikimbia katika fukwe mbalimbali za jijini Dar wakiwa na lengo la kuongeza pumzi na stamina kwa sababu siku zote bondia bora ni yule ambaye anakubalika kujitoa kufanya mazoezi makali ili aweze kufanikiwa.

 

“Naamini hata mabondia waliokuja kutoka nje nao wamejiandaa vya kutosha kwa sababu hii ni mikanda mikubwa hivyo bondia yoyote atakayefanikiwa kushinda atakuwa amejiweka katika soko zuri la kibiashara nje ya Afrika. “Lakini pia haya yatasaidia kuongezea au kufanyika kwa mapambano mengine makubwa iwapo kila bondia atajua thamani yake siku hiyo na ndiyo maana yatakuwa live ili kutoa fursa kubwa kwa kila mtu, sehemu yoyote atakayokuwepo kuweza kuona bila ya kufika ukumbini kupitia website ya www.globaltvtz.com. “Shabiki anachotakiwa kufanya hivi sasa ili kuweza kuona mapambano hayo kwa njia ya simu au kompyuta tena bure, basi ahakikishe anajiunga (SUBSCRIBE) na YouTube Channel ya Global TV Online sasa hivi.

 

Yaani anatakiwa kuingia YouTube halafu anatafuta GLOBAL TV ONLINE kisha abonyeze neno subscribe pia abonyeze kikengele kidogo kilichopo pembeni yake ambacho kitamkukumbusha kuangalia pambano hilo mara tu litakapoanza. “Kama utakuwa umeshajiunga, basi hakikisha pia umebonyeza kikengele ili usipitwe na kila kinachoendelea Global TV. Pia unaweza kutupata kupitia mtandao wa www. globaltvtz.com , jiunge sasa na Global TV ili uwe wa kwanza kuona ndondi za kimataifa.

 

Kajiunge sasa kwa kuingia www.youtube. com /user/ uwazi1,” anasema Ustaadh. Katika hatua nyingine, meneja wa mabondia hao, Stephen Mawenzi, Raia wa Malawi amefunguka kuwa mabondia wake wako katika hali nzuri kuelekea katika mapambano hayo baada ya maandalizi makali waliyokuwa wakiyafanya katika kambi zao.

 

“Tumeamua kufika mapema hapa ili kuweza kumalizia maandalizi yetu kwa uhakika ikiwa ni pamoja na kuzoea hali ya hewa ya hapa ili iwe rahisi kwa mabondia wangu kutimiza majukumu yao kwa wepesi. “Lakini kwa upande mwingine nipongeze wadhamini Global TV Online kwa kitendo chao cha kuamua kurusha live maana tayari mashabiki wa mabondia wangu wameshapata links wanasubiria tu siku ifike ili waweze kuona kitu ambacho hakikuwahi kufanyika huko nyuma,” anasema Mawenzi.

Licha ya ukubwa wa mapambano hayo, hayatakuwa na kiingilio na mashabiki wataweza kushuhudia mubashara kupitia simu zao za mkononi tu, kwani litaoneshwa na Global TV pekee. Wadau na mashabiki watakaopata nafasi ya kuingia ukumbini wataingia kwa kadi maalum za mwaliko tu.

Leave A Reply