The House of Favourite Newspapers

Msuva arejea Taifa Stars, aahidi kuwatungua Rwanda

0
Simon Msuva.

 

JUZI Alhamisi winga Simon Msuva hakushiriki mazoezi ya Taifa Stars na kuzua sintofahamu, lakini jana asubuhi alishiriki mazoezi hayo na kutamba kuifunga Rwanda, leo Jumamosi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa.

Taifa Stars chini ya Kocha Salum Mayanga, inacheza mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan), michuano hiyo itafanyika mwakani nchini Kenya.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Msuva alisema kuwa hakuonekana mazoezini juzi Alhamisi kwani alipewa mapumziko mafupi na kocha, ameshangaa uvumi uliozagaa wa kujiondoa kikosini.

“Siku ya Alhamisi ni kweli kabisa sikufika kwenye mazoezi ya timu ya taifa, lakini mimi nilipewa mapumziko na kocha, hivyo sina tatizo lolote na niko fiti kuipigania nchi yangu katika mchezo huu,” alisema Msuva anayechezea Klabu ya Yanga.

 

“Nipo vizuri kabisa kuweza kuivaa Rwanda na kutokana na maandalizi tuliyofanya, nina uhakika tutashinda mechi hii.”

Awali, Mayanga alipoulizwa kuhusu kukosekana kwa Msuva katika kikosi chake na mchezo ulio mbele yake, alisema kilichotokea ni moja ya mbinu za kuelekea mechi hiyo.

“Msuva hakuja mazoezini na hatuwezi kuwa tunasema kila kitu, nilimpa mapumziko ya kawaida na kesho (leo) atacheza mechi dhidi ya Rwanda kama kawaida,” alisema Mayanga.

 

JOHNSON JAMES | CHAMPIONI| Mwanza

Leave A Reply