The House of Favourite Newspapers

Madai: Askofu Afunguka Kutoka na Lulu

0

Askofu-na-LuluStori: Waandishi Wetu, Risasi Jumamosi

DAR ES SALAAM: Ukweli ni huu! Askofu, Mtume na Nabii wa Kanisa la Living Water Center, maarufu kwa jina la ‘Makuti Kawe’ la jijini Dar es Salaam, Onesmo Ndegi amezima uvumi kwamba, amekuwa akitoka na nyota wa filamu za Bongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ akisema kuwa, hayo ni maneno ya watu kwani yeye ni mtumishi wa Mungu aliye hai, Risasi Jumamosi limefanya mahojiano naye.

Akizungumza na gazeti hili ndani ya ofisi ya kanisa lake lililopo Kawe, Dar, Jumanne iliyopita, Askofu Ndegi alisema anamfahamu Lulu kama muumini wake na ndiyo maana hata alipotajwa kushiriki Tuzo za African Magic Viewers Choice (AMVCA) 2016 zilizofanyika Machi, mwaka huu nchini Nigeria, yeye na waumini wake walimfanyia maombi ashinde.

LENGO LA RISASI JUMAMOSI

Lengo kuu ya gazeti hili kumsaka Askofu Ndegi lilikuwa kumuuliza pamoja na ishu ya Lulu, pia madai kwamba, baadhi ya watumishi wa Mungu nchini (Wakristo kwa Waislam) wamekuwa wakitumia mwanya wa kupewa msamaha wa kodi wa serikali (Tax Exemption) kuingiza kutoka nje, vifaa vya nyumba za ibada lakini matokeo yake wamekuwa wakiingiza mali zao binafsi na hivyo kuhesabiwa kwamba, wanakwepa ushuru.

ILIKUWA HIVI

Risasi Jumamosi lilifika kwenye kanisa hilo na kuomba kuonana na Askofu Ndegi ambapo wasaidizi wake waliwasiliana naye na kuruhusu.

BAADA YA SALAMU NA UTAMBULISHO

Ndani ya ofisi yake, Risasi Jumamosi lilijitambulisha kwa mtumishi huyo wa Mungu na mahojiano yalianza hivi…

Risasi Jumamosi: Baba askofu, kumekuwa na madai kwamba, baadhi ya watumishi wa Mungu nchini wamekuwa wakitumia msamaha wa kodi unaotolewa na  serikali kwa taasisi za dini kuweza kupitisha bure vifaa vya makanisa na misikiti kama vile magari madogo, mabasi, malori, spika nakadhalika, kujiingizia vitu vyao binafsi na kujitajirisha wao. Hili unasemaje baba askofu?

Askofu: Ni kweli, wapo baadhi ya watumishi wa Mungu wanafanya hivyo, baadhi, lakini mimi hapa sijawahi. Nimekuwa nikitumia msamaha huo kwa serikali kuingiza vitu vya kanisa tu (akaonesha magari ya watumishi wake).

KUHUSU LULU

Risasi Jumamosi: Oke, vizuri sana. Unamjua Elizabeth Michael au Lulu?

Askofu: (akiwa katika utulivu) ndiyo, namjua.

Risasi Jumamosi: Unamjua kama nani?

Askofu: Ni muumini wangu, amekuwa akisali hapa.

Risasi Jumamosi: Sasa kuna madai yalifika ofisini kwetu kwamba, eti wewe unatoka na Lulu. Inadaiwa kwamba, umekuwa ukimfanyia maombi hapa ofisini kwako, lakini kuna siku mkeo kwa vile alishajua alipokukuta naye akataka ufafanuzi kutoka kwako kwani alishawahi kusikia kuhusu madai hayo. Ukweli ni upi baba askofu?

MKE AITWA MBELE YA RISASI JUMAMOSI

Askofu: (anatabasamu, anamuita msaidizi wake. Anafika, anamtuma akamuitie mkewe, mara mke anafika)…

“Huyu ni mke wangu, anaitwa Lilian Ndegi. Hebu ninyi waandishi muulizeni hilo swali lenu.”

Baada ya kusikia madai hayo, mama askofu naye alifunguka hivi:

“Hee! Siyo kweli mbona. Wala mimi sijawahi kukutana na hali hiyo. Lulu ni muumini wetu hapa, mimi niko naye na namlea kiroho. Nani aliwaambia habari hiyo? Hakuna kitu kama hicho.”

ASKOFU ASHIKA USUKANI

Askofu: (akiwaangalia waandishi). Huyu ni mke wangu. Nataka kuwaambia kitu kimoja, mimi nina miaka 51 sasa, mke wangu 47. Binti wetu wa kwanza ana umri wa miaka 28, yupo hapo Chuo Kikuu (Mlimani) anasomea sheria, hata Lulu ni mdogo kwake (Lulu ana miaka 20). Mpaka kufikia hapa mimi na mke wangu hatujawahi kusuluhishwa na mtu kwa kisa cha mambo kama hayo.

UPENDO ZAIDI

Katika kuonesha upendo wake kwa mkewe Lilian, Ndegi alikwenda mbele zaidi ambapo alilionesha Risasi Jumamosi kutoka kwenye simu yake, picha yao wakiwa katika pozi la upendo lakini alitahadharisha isipigwe picha (Risasi Jumamosi likaomba picha hiyo, akacheka).

ATOBOA SIRI YA USHINDI WA LULU

Kama vile haitoshi, Askofu Ndegi alisema kuwa, ushindi wa Lulu kwenye tuzo kule Nigeria, maombi ya kanisa hilo yalichangia.

“Lulu alipotajwa tu kuwa mmoja wa washiriki katika kile kinyang’anyiro, mimi na waumini wangu tulimfanyia maombi maalum, akashinda. Na aliporejea alikuja hapa na tuzo yake kwa ajili ya kulishukuru kanisa, hata Makonda (Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaaam alikuwepo),” alisema askofu huyo kwa kujiamini huku mkewe akitingisha kichwa kuashiria kwamba anakubaliana na mume wake.

AWATAJA MASTAA WENGINE

Askofu huyo alisema si Lulu tu, wapo nyota wengine wanaosali kwenye kanisa lake linalosifika kwa maombi ya kufungua watu wenye matatizo mbalimbali.

“Ukiachana na Lulu, kuna wasanii wengine wanaosali hapa. Mfano, Ray (Vincent Kigosi), Mainda (Ruth Suka, zamani Mwanaidi), Pastor Myamba (Emanuel Myamba),” alisema askofu huyo licha ya kwamba, Risasi Jumamosi linafahamu hata Makonda ni muumini wa kanisa hilo.

MUUMINI WA KANISA

Muumini wa kanisa hilo ambaye aliomba hifadhi ya jina, akizungumzia madai hayo alisema: “Mimi namjua Ndegi, yuko safi. Ila sema tu kuna watu hawapendi kuona au kukomaa au kukua kwa kanisa hili. Kanisa lilianza kidogokidogo, na kila siku linakua mpaka unavyoliona sasa. Sasa wale wasiopenda huduma ya Mungu kukua au kuendelea mbele, wanamnenea hayo mambo.”

LULU SASA

Siku hiyohiyo ya Jumanne, Risasi Jumamosi lilimtafuta Lulu mwenyewe ambapo alipatikana kwa njia ya simu na kusomewa madai hayo mwanzo mwisho, jibu lake lilikuwa hili:

“Muulize huyohuyo aliyekwambia. Mimi sitaki kuulizwa vitu ambavyo sijasema. Kitu nikikiongea mimi mwenyewe ndiyo niulizwe…” (akakata simu).

Imeandikwa: Issa Mnally, Richard Bukos na Mayasa Mariwata

Leave A Reply