The House of Favourite Newspapers

Madai Fumanizi! Mwalimu wa Kike Ajinyonga Nyumbani kwa Mwal. Mkuu

0
 Mwenyekiti wa Kijiji cha Changarawe akihojiwa na mwandishi wetu, ofiisini kwake.

MWALIMU wa kike katika shule Moja ya Msingi iliyopo Tarafa ya Mgeta Wilaya ya Mvomero Mkoa Morogoro, amezua gumzo baada ya kudaiwa kujinyonga kwenye nyumba ya Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mlali iliyopo kijiji cha Mlali Wilaya ya Mvomero.

 

Tukio hilo lilitokea April 29 Mwaka huu limezua utata kutokana na ndugu wa marehemu kudai aliuawa huku mashuhuda wakidai alijitoa uhai baada ya kufamaniwa akiwa na Mwalimu Mkuu huyo ambaye ni mume wa mtu.

 

TUKIO LILIVYOTOKEA.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo Wema Simba na Asha Juma kutoka katika Vijiji vya Changarawe na Mlali, walidai kuwa walikuwa wakimuona Mwalimu Mkuu kila mara akiingia na mwanamke huyo kwenye nyumba hiyo ambayo ni mali ya shule.

 

”Licha ya kupewa nyumba na uongozi wa shule hapa kijijini Mlali, Mwalimu Mkuu hakutaka kuhamishia familia yake hapa kijijini na badala yake familia yake inaishi Morogoro Mjini huku akiwa anaishi peke yake shuleni hapa.

 

”Tunashangaa shule zimefungwa kupisha Corona lakini huyu Mwalimu Mkuu kila baada ya siku tatu anatoka mjini anakuja hapa na baada ya muda utaona anakuja mwanamke na wanajifungia ndani zaidi ya masaa manne.

 

”Kutokana na hali hiyo wambea waliamua kumtonya mke wa Mwalimu Mkuu huyo ambaye anadaiwa alikodi bodaboda kutoka Mjini hadi Kijijini Mlali akiwa na wenzake ambao walivamia hiyo nyumba na kumkuta mumewe akiwa na mwanamke ndani.

Nyumba ya familia ya Shayo ambapo marehemu mkewe  amezikwa eneo la nyumba hiyo iliyopo Kijiji cha Changarawe Kata ya Mzumbe.

”Baada ya kuwafumania mume alifanikiwa kukimbia huku mwanamke akikamatwa na kupokea kichapo kitakatifu baadaye wakamvua nguo zote akabaki kama alivyozaliwa, wakamfungia mlango kwa nje huku wakimueleza kwamba wanakwenda kumfuata mumewe aje kumshuhudia mkewe alivyofumaniwa.

 

”Walimpigia simu mumewe lakini hakupatikana waliporudia na kufungua mlango wakakuta mwanamke huyo kajinyonga.  Huenda alichukua maamuzi hayo kukwepa aibu,”walisema mashuhuda hao.

Aidha m waliendelea kusema kuwa polisi walifika eneo la tukio na kuuchukua mwili wa marehemu wakaupeleka mochwari.

 

FAMILIA YA MAREHEMU WATOA NENO

Aidha mwandishi wa habari hizi alifika nyumbani kwa marehemu Kijiji Cha Changarawe Kata ya Mzumbe Wilaya ya Mvomero mkoani hapa na kuzungumza na mume wa marehemu aliyefahamika kwa jina la Joseph Shayo.

 

Hata hivyo Shayo ambaye ni Bwana Shamba wa Kata ya Mzumbe alikataa kuzungumza na badala yake msemaji wa familia hiyo, Filbert Shayo, alikiri kutokea kwa purukushani hiyo lakini alidai kuwa ndugu yao ameuawa.

 

”Ni kweli tukio hilo limetokea na ndugu yetu hatunaye tena hivyo sisi kama familia hatuwezi kusema chochote kwani suala hilo liko polisi pia hatuwezi kukupa picha ya marehemu au kukuruhusu upige picha kaburi mpaka tupate kibali cha Polisi kwa sababu kuna utata kuhusu tukio hili,” alisema.

 

Aidha Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Changarawe, Fred Matangalu, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

“Nakumbuka April 29, 2020, Mkuu wa Kituo cha Polisi Mzumbe alinitumia SMS kwamba wanampigia simu Bwana Shamba Wetu Shayo lakini hapatikani hivyo nimtafute niende naye kituoni maana mkewe amafariki katika kijiji cha jirani cha Mlali.

 

“Nilienda kwa Shayo nikamkuta sikumwambia taarifa hizo nilimueleza kwamba anaitwa kituo cha Polisi. Basi tukaongozana naye mpaka kituoni ndipo wakamueleza kwamba mkewe anadaiwa kujinyonga katika kijiji cha Mlali, hivyo kwa pamoja tukapanda gari la Polisi kuelekea eneo la tukio.

 

”Tulipofika Shayo aliibua utata akidai kwamba huenda mkewe hakujinyonga waliomfumania ndiyo waliomuua,”alisema mwenyekiti huyo na kuongeza:

“ Licha ya kupewa maelezo na Polisi,Shayo hakukubali mpaka Mkuu wa Polisi kutoka Wilaya ya Mvomero alipokuja na kumfafanulia vizuri.

 

Ndipo akukubali kuuchukua mwili wa marehemu na kuuzika Mei 4 kwenye eneo la nyumba yao iliyopo hapa Changarawe, ”alisema mwenyekiti huyo.

Mwandishi wa habari hizi alizungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa ambapo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuahidi kulitolea ufafanuzi zaidi baabaye.

 

Na Dustan Shekidele, Morogoro.

Leave A Reply