The House of Favourite Newspapers

Madaktari Bongo wafunguka dawa 4 za kutibu Corona

0

DAR: Wakati maambukizi ya Virusi vya Corona yakizidi kushika kasi katika maeneo mbalimbali duniani, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeanzisha; ‘mpango mahsusi wa kuokoa maisha’ unaojumuisha nchi 10 katika kutafiti dawa nne za kutibu Ugonjwa wa COVID-19.

 

Juhudi hizo zinakuja katika kipindi ambacho hadi kufikia Aprili Mosi, tayari watu 860,166 walikuwa wameambukizwa Corona duniani, huku 42,344 wakifariki dunia kwa ugonjwa na 178,441 wakiwa wamepona.

 

Tayari janga hilo la Corona limeshaiathiri Tanzania ambayo hadi kufikia Aprili Mosi, mwaka huu, ilikuwa na wagonjwa 19 waliothibitika kuwa na Corona, ilhali mgonjwa mmoja akithibitika kufariki kwa COVID-19.

Idadi ya watu kuathirika na kufariki, duniani imeendelea kuongezeka kila kukicha huku ugonjwa huo ukiwa hauna tiba wala chanjo, jambo ambalo sasa madaktari kutoka sehemu mbalimbali duniani, wanafanya kazi ili kupunguza makali ya dalili za ugonjwa huo.

Kwa sababu hiyo, WHO imeanzisha mpango wa mshikamano ‘solidarity’ ambapo mataifa kumi yanafanyia uchunguzi jinsi dawa nne zinavyoweza kutibu Covid-19.

 

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk. Tedros Ghebreyesus alisema lengo la mpango huo ni kukusanya takwimu zaidi kwa wakati mfupi ili badala ya kuanza kutengeneza dawa mpya, mchakato unaoweza kuchukua miaka kadhaa, washiriki wa utafiti huo wataona iwapo dawa hizo zinazotumika kukabiliana na magonjwa mengine, zitaweza kuzuia makali ya virusi vya Corona.

Alisema ingawa baadhi ya dawa hizi zinapatikana sokoni, madaktari wanasisitiza kwamba hazifai kutumiwa bila ya ushauri wa mtaalamu.

 

Nchi za Argentina, Bahrain, Canada, Ufaransa, Iran, Norway, Afrika Kusini, Uhispania, Uswizi na Thailand ndizo zimejiunga kufanya utafiti huo ambapo wanatarajia kwamba wagonjwa wengi watashiriki.

Profesa wa takwimu za kibaiolojia kutoka Chuo Kikuu cha Carlifonia nchini Marekani, Dk. George Rutherford alisema umuhimu wa utafiti kama huu ni kwamba, unaweza kushirikisha wagonjwa kwa haraka.

 

MADAKTARI BONGO

Wakizungumza na IJUMAA, baadhi ya madaktari walisema kuwa tafiti hizo zinaweza kuonesha matumaini ndani ya kipindi cha muda mfupi kutokana na juhudi zinazoendelea.

Dk. Godfrey Chale kutoka Hospitali ya Wilaya ya Temeke, alisema kutokana na nguvu kubwa iliyoelekezwa na shirika hilo la afya duniani, upo uwezekano wa tiba hizo kupatikana ndani ya kipindi cha miezi sita.

 

“Kwa hiyo, kwa kuwa virusi hivi vilianza kusambaa Desemba mwaka jana, hadi Juni mwaka huu, tunaweza kupata tiba ya awali,” alisema.

Hoja hiyo iliungwa mkono pia na Dk. Sadick Sizya kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo alisema kwa kuwa virusi hivyo ni vipya, ni vema wananchi wakaendelea kuchukua tahadhari kujikinga navyo kwa kuwa tiba au chanjo yake inaweza kuchukua muda mrefu zaidi kupatikana.

 

Dk. Sizya alisema katika utafiti huo, muungano wa nchi hizo unatia matumaini kwa sababu utafiti huhitaji gharama kubwa, muda na mbinu mbalimbali za kupata majibu sahihi.

 

UTAFITI WA MATUMAINI

Ili kuanzisha utafiti huo, jopo la watalaam wa WHO lilichagua tiba nne ambazo wanazitathmini kuweza kukabiliana na virusi vya Corona.

Tiba hizo zina dawa mchanganyiko ambazo zimetumika kutibu ebola, malaria au HIV.

 

“Baada ya tiba kuanza, madaktari watachunguza jinsi wagonjwa wanavyoendelea, ikiwemo siku watakazoondoka hospitalini ama iwapo atashindwa kupona.”

Aidha, Dk. Rutherford alisema kwamba, katika tafiti kama hizi, lengo ni kuanzisha tiba katika awamu za kwanza za ugonjwa kabla ya mgonjwa kuingia katika chumba cha wagonjwa mahututi.

 

TIBA NNE

  1. Remdesivir:

Licha ya kutengenezwa ili kutibu Ebola, dawa ya Remdesivir haikuonekana kuwa nzuri. Hata hivyo, inaonekana kuwa na uwezo dhidi ya virusi vya Corona kulingana na vipimo vya seli zilizopandwa katika maabara.

Pia imekuwa na faida kubwa kwa wagonjwa wa Covid-19, lakini hiyo haitoshi kuthibitisha kuwa dawa hiyo ni nzuri.

Mkurugenzi wa mpango wa magonjwa ya kuambukiza katika Chuo Kikuu cha Columbia (EE), Stephen Morse alisema, ‘’Kati ya dawa zilizojumuishwa katika mradi huo wa pamoja, Remdesivir inaonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kukabiliana na virusi vya Corona katika vipimo vya maabara.”

 

2. CHLOROQUINE/ HIDROXICLOROQUINA

Chloroquine ilitumika kwa miaka mingi kutibu ugonjwa wa malaria hadi pale vimelea ambavyo husababisha ugonjwa huo vilipotengeneza usugu dhidi ya dawa hiyo.

“Iwapo inaweza kutibu, haimaanishi kuwa itafanya kazi dhidi ya Covid-19,” alisema Rutherford.

 

Dawa hii inaweza kutumika kupitia kinywa lakini pia hutoa athari za maumivu kama yale ya kuumwa na kichwa, kuhisi kizunguzungu, kupoteza hamu ya kula, kuumwa na tumbo, kuhara, kutapika na kutokwa na upele katika ngozi, kulingana na Maktaba ya Kitaifa ya Tiba nchini Marekani.

Hatari yake ni kwamba, ni rahisi kuipata na muonekano wake katika habari kuhusiana na virusi vya Corona umesababisha kesi za sumu kuripotiwa.

 

3. RITONAVIR NA LOPINAVIR

Mchanganyiko wa dawa hizi mbili, umetumika kwa matibabu ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Wataalam waliozungumza na IJUMAA wanakubali kwamba mchanganyiko huu, haujaonyesha matokeo ya kutia moyo dhidi ya virusi vya Corona.

“Lakini ni busara kujaribu tena,” anasema Rutherford.

 

4. RITONAVIR/LOPINAVIR

Tiba ya nne kupimwa na timu hiyo ya watafiti ni mchanganyiko wa Ritonavir, Lopinavir pamoja na Interferon-beta, Molekyuli ambayo husaidia kudhibiti uchochezi na imeonekana kuwa bora kwa wanyama walioambukizwa na ugonjwa wa kupumua wa Mashariki ya Kati (MERS).

 

Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa ni muhimu kuwa waangalifu wakati zinapotumika kwani; ikiwa zinatumika katika hatua za mwisho mwisho, zinaweza kukosa ufanisi au hata kusababisha madhara zaidi kuliko faida kwa mgonjwa.

 

Sasa ni suala la wakati gani matokeo hayo yatapatikana kwa mradi huo wa mshikamano, lakini kulingana na Morse ni “Hatua moja kubwa iliyopigwa.”

 

SH BILIONI 98.7 KUTUMIKA

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dk. Tedros Ghebreyesus aliongeza kuwa mfuko wa utafiti huo dhidi ya COVID-19 hadi sasa umeshakusanya zaidi ya dola milioni 43 (Tsh bilioni 98.7) kutoka kwa watu zaidi ya 173,000 na mashirika ikiwa ni siku chache tu tangu ulipozinduliwa.

 

“Haya ni mafanikio makubwa, tunawapongeza watafiti kote duniani ambao wamekuja pamoja ili kutathmini majaribio ya tiba.”

Aliongeza kuwa WHO na washirika wake wanaandaa utafiti katika nchi nyingi ambako baadhi ya nchi hizo dawa hizi ambazo hazijajaribiwa, zitalinganishwa.

Stori: GABRIEL MUSHI Ijumaa

Leave A Reply