The House of Favourite Newspapers

Madebe Aweka Rekodi Bongo Movies

0

NABII Mswahili siyo jina geni kwa wapenda Bongo Movies. Ni jina la kazi la muigizaji nyota wa filamu kwa sasa kutokana na ubunifu wa kutumia vizuri lugha ya Kiswahili kwa misemo ambayo imekuwa gumzo.

 

Jina halisi ni Madebe Lidai. Alianza rasmi sanaa ya filamu mwaka 2002 akiwa na Kundi la Shirikisho Msanii Afrika.

Jeneza ni filamu ya kwanza iliyomtambulisha Madebe kwa mashabiki zake. Amefahamika zaidi na filamu nyingine kama Mama Mwali, Chanuo, Nabii Mswahili, Kiberiti, Msungo na nyingine nyingi.

 

Gazeti la IJUMAA limefanya mahojiano maalum na Nabii Mswahili ambaye anafunguka mengi usiyoyafahamu;

IJUMAA: Kazi yako mpya ya Matusi inakimbiza YouTube kwa sasa, je, mapokeo yake yakoje?

 

MADEBE: Ninawashukuru sana mashabiki maana Matusi inafanya vizuri mtandaoni na inakaribia kufikisha watazamaji milioni moja, nitakuwa muigizaji wa kwanza Bongo Movies ambaye ameweka rekodi ya kupandisha filamu kwenye YouTube na kufikisha watazamaji wengi.

 

IJUMAA: Mashabiki wako walizoea kuona ukitumia mfumo wa CD au DVD, kwa nini mitandaoni sasa?

MADEBE: Kwanza niliamua kupitia mitandao yote (platforms) kwa sababu tasnia yetu ina ukakasi kidogo, hivyo tunajaribu kutafuta vyanzo vingine. Lakini pia iko hata kwenye mfumo wa DVD.

 

IJUMAA: Idea ya Matusi ilikujaje?

MADEBE: Kwanza nilivyoitengeneza ni kitu ambacho niliangalia vijana wanaweza kufuatilia.

IJUMAA: Neno lenyewe Matusi, halikukuletea shida katika masuala ya kimaadili?

 

MADEBE: Hii tamthiliya ilipita bodi ya filamu japo ikawa na ukakasi kidogo kwa sababu nimetohoa neno lenyewe kuwa siyo tusi. Hata bodi niliiomba kunihakikishia ndiyo ikaonekana siyo matusi kama watu wanavyotafsiri.

 

Hata kwenye filamu ya Nabii Mswahili, waumini wengi walihubiri makanisani na misikitini kuwa nataka kukufuru. Walivyoangalia na kukuta kitu kingine, waliona ni kitu kizuri.

 

IJUMAA: Umekuwa ukija na idea tofautitofauti ambazo zina fasihi kubwa ndani yake, mfano Nabii Mswahili, je, huwa unatoa wapi?

MADEBE: Huwa ninafanya sana utafiti na ndiyo sababu ninachelewa kutoa filamu, nasoma sana vitabu vya Kiswahili ndiyo sababu natumia fasihi kwenye filamu na hadithi zinazohusu maisha halisi ya Watanzania.

 

IJUMAA: Kwa nini uliamua kufanya utafiti kabla ya kutoa kazi zako?

MADEBE: Ni kutokana na kuhangaika, wasanii wengi wanatoka katika fani moja na kuingia kwenye sanaa ilihali hawaijui sanaa.

IJUMAA: Je, umesomea sanaa?

 

MADEBE: Nimesoma hizi kozi fupifupi ila sikusoma sanaa yenyewe kabisa. Ni kipaji ambacho kilikosa pesa ya kukiendeleza, hivyo nikapambana na kujisumbukia mwenyewe.

IJUMAA: Misemo na misamiati unayotumia kwenye filamu zako, umekuwa ukiitoa au kujifunza wapi?

 

MADEBE: Kwanza ninamshukuru Mungu amenipa kipaji cha kuunda semi na tungo. Naangalia watu wa hali ya chini wanavyoguswa, ni sawa na kukaa nao karibu na kusikiliza matakwa yao kwa kutafuta namna ya kufuatilia kazi zangu.

 

IJUMAA: Tangu umeanza kutumia mitandao kwenye kazi zako, unaona teknolojia imebadili kitu kwenye sanaa ya Bongo?

MADEBE: Teknolojia imebadili kwa namna moja na imerahisisha. Imefanya kitu kikubwa na kunakuwa na uwezo wa wasanii kutokuuza hati miliki maana mitandao inalipa miaka yote tofauti na mifumo iliyokuwa ikitumika zamani.

 

IJUMAA: Kukubalika kwako kwa mashabiki, unadhani una kitu cha tofauti na wasanii wengine?

MADEBE: Tofauti yangu na wasanii wengine, ninafikiria sana kabla ya kufanya, maana wengine wanatengeneza bila utafiti.

 

IJUMAA: Kupitia ubora wako umewahi kushiriki na kushinda tuzo za ndani na nje ya nchi?

MADEBE: Kwa hapa Tanzania nina tuzo mbili; moja ni ZIFF na nyingine ni ya Nyanda za Juu Kusini ya Muigizaji Bora. Kwa upande wa tuzo za nje niliingia kwenye tuzo za Kiswahili nchini Kenya ila janga la Corona likakwamisha.

 

IJUMAA: Kutokana na matumizi yako ya fasihi na misamiati, imewahi kukupa madili kwenye taasisi za Kiswahili?

MADEBE: Hizo dili bado sijapata.

IJUMAA: Kwa upande wako unauzungumziaje msemo wa tamthiliya zinalipa kuliko filamu?

 

MADEBE: Bado sijasambaza katika media kama zilivyo series nyingine, tamthiliya si kwamba zinalipa maana tumetoka hukohuko, ninaweza kusema kwa upande wangu kuna mafanikio.

IJUMAA: Naona mkeo pia ni muigizaji na umeigiza naye filamu nyingi, je, unamzungumziaje?

 

MADEBE: Kwanza mke wangu ana kipaji kikubwa cha kuigiza na ana ndoto za kuwa prodyuza ila nasimamia kipaji chake kwanza ili asije kupotea.

IJUMAA: Kuna mipaka ya mkeo kufanya kazi na wasanii wengine zaidi yako?

MADEBE: Anafanya kazi na wasanii wengine maana hela inaingia na tunagawana majukumu, kwa hilo simzuii.

 

IJUMAA: Je, katika aina ya scene za kuigiza huwa unampangia?

MADEBE: Katika kazi vitu vingine ni yeye mwenyewe kujiheshimu, anafanya scene yoyote maana najua haiwezi kuwa nje ya makubaliano na siwezi kumchunga maana misingi anayo yeye.

MAKALA: HAPPYNESS MASUNGA

Leave A Reply