The House of Favourite Newspapers

Maelfu Wajitokeza Kwenye Kilele cha Boomplay Campus Tour Jijini Mwanza

0
Msanii wa muziki wa Singeli nchini Tanzania, Khalid Mtumbuka al-maarufu Meja Kunta, akitoa burudani kwa wanafunzi wa jiji la Mwanza kupitia Tamasha la Boomplay Campus Tour lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Mt. Agustino (SAUT) jijini humo siku ya jana. Tamasha hilo lilihudhuriwa na wanafunzi zaidi ya elfu sita kutoka katika vyuo mbalimbali vya jiji hilo.

 

Boomplay, App inayoongoza katika utoaji wa huduma ya kusikiliza na kupakua muziki barani Afrika kwa kushirikiana na jukwaa la kuwezesha vijana la Benki ya NMB ‘Go na NMB’ ilileta burudani kwa wanafunzi wa vyuo vikuu mkoani Mwanza kupitia tamasha kubwa la Boomplay Campus Tour.

 

Tamasha hilo lilifanyika katika Chuo Kikuu cha Mt. Augustino Tanzania (SAUT) mkoani Mwanza siku ya tarehe 10 Desemba na kuhudhuriwa na zaidi ya wanafunzi 6,000.

 

Tamasha hilo kubwa lilianza kwa wanafunzi kushiriki katika michezo mbalimbali kama vile mechi za mpira wa miguu, Usajili wa akaunti na mashindano ya kuimba ambapo wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbalimbali mkoani Mwanza waliweza kushindana na kuwajengea utamaduni wa kucheza michezo na kukuza vipaji vyao.

 

Msanii wa Hip-hop nchini Tanzania, Awadhi Chami al-maarufu Moni Centrozone akitoa burudani kwa wanafunzi wa jiji la Mwanza kupitia Tamasha la Boomplay Campus Tour lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Mt. Agustino (SAUT) jijini humo siku ya jana. Tamasha hilo lilihudhuriwa na wanafunzi zaidi ya elfu sita kutoka katika vyuo mbalimbali vya jiji hilo.

 

Baada ya hapo hafla hiyo ilitawaliwa na mazungumzo kutoka kwa wadau mbalimbali ikiwemo timu kutoka ‘Go na NMB’ pamoja na Uongozi wa Chuo cha Mt. Agustino.

 

Wadau hao walizungumza na wanafunzi jinsi ya kujitambua na kukuza vipaji vyao, elimu ya matumizi sahihi ya fedha, fursa zilizopo kwenye soko la muziki hasa muziki kidijitali lakini pia jinsi ya kujiandaa baada ya kuhitimu masomo yao.

 

Mida ya usiku wasanii kadhaa walipanda jukwaani kutoa burudani akiwemo Stamina, Meja Kunta, Moni Centrozone na baadhi ya wasanii wa mkoani Mwanza walipata fursa ya kuonesha vipaji vyao na kuwapa mashabiki burudani nzuri. Stamina na Moni Centrozone walitoa burudani ya kuvutia kupitia ngoma zao za Hip-hop huku Meja Kunta akifanya maajabu kupitia nyimbo zake za muziki Singeli na kuhakikisha mashabiki wote wanaburudika bila kuchoka.

 

Msanii wa Hip-hop nchini Tanzania, Bonventure Kabogo al-maarufu Stamina akitoa burudani kwa wanafunzi wa jiji la Mwanza kupitia Tamasha la Boomplay Campus Tour lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Mt. Agustino (SAUT) jijini humo siku ya jana. Tamasha hilo lilihudhuriwa na wanafunzi zaidi ya elfu sita kutoka katika vyuo mbalimbali vya jiji hilo.

 

Katika taarifa iliyotuwa kwenye vyombo vya habari, Meneja Mkuu wa Boomplay Tanzania, Natasha Stambuli alisema:

 

“Ziara za Campus Tour zinalenga kuimarisha uhusiano kati ya Boomplay na wanafunzi wa vyuo vikuu kwani vijana ni mabalozi wazuri wa App ya Boomplay, hivyo maamuzi ya kufanya matamasha kama haya ni katika kuhakikisha tunawafikia vijana kwa kugusa vitu wanavyovipenda mfano ni kupitia matamasha kama haya.”

 

 

Kwa upande wake, Meneja Uhusiano-Wateja Binafsi wa Benki ya NMB, Robert Mtimba alisema, “Tunajivunia sana kuwa sehemu ya shughuli hii, kwa miaka mingi lengo letu limekuwa kuungana na vijana kuhakikisha tunagusa vitu wanavyovipenda.

 

Kama taasisi, tunaahidi kuendelea kusaidia vijana huku lengo kuu likiwa ni kuwapa vijana fursa nyingi za uwezeshaji, elimu ya kifedha pamoja na kuelewa matumizi na faida za huduma za kidijitali za benki hususani NMB Lipa Mkononi, Mshiko Fasta na NMB Pesa Wakala.

Leave A Reply