The House of Favourite Newspapers

Mafundi wa EFD Kizimbani Kwa Kuisababishia TRA Hasara ya Zaidi ya Mil 900

0

MAFUNDI wawili wa mashine za kielektroniki za EFD na mwanamke mmoja, wakazi wa jijini Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni wakikabiliwa na mashtaka saba likiwemo la utakatishaji na kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya Sh Milioni 954.5.
Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na wakili wa serikali Mwandamizi Emmanuel Medalakini akisaidiana na Wakili wa Serikali, Auni Chilamula imewataja washtakiwa hao kuwa ni Awadhi Mhavile na Ally Msesya maarufu kama Ally Yanga (37) mafundi wa mashine na Salma Ndauka (38) Msimamizi wa Gereji anayeishi Sinza.
Wakisomewa hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga inadaiwa washtakiwa wametenda makosa hayo kati ya Mei na Julai mwaka 2023 ndani ya jiji la Dar es Salaam.
Imeelezwa kuwa  kati ya Mei 17 na Julai 2023, katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam, washitakiwa wote kwa pamoja walitumia isivyohalali mashine za EFD zilizozuiwa kinyume na sheria kutengeneza risiti zisizo halali zilizopakiwa kwenye mfumo wa TRA ili kuboresha walipa kodi wengine kudai Kodi ya Ongezeko la Thamani ya Sh 954,596,372 na kumpotosha Kamishna wa mamlaka hiyo.
Pia washitakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kutumia isivyo halali mashine za EFD zilizokuwa zimefungiwa na kumdanganya Kamishna wa TRA kwa kutoa risiti zisizosahihi na kuwanufaisha walipa kodi wengine kudai Sh 954,596,372.
Aidha katika mashtaka matatu yanayomkabili Mhavile peke yake inadaiwa, Julai 8 mwaka huu, mshatakiwa huyo alikutwa na mashine za kielektroniki 22 zinazozaniwa kuwa za wizi au zimepatikana kwa njia isiyo halali.
Medalakini anaendelea kudai kuwa, Julai 19, mwaka huu maeneo ya Sinza A, Wilaya ya Kinondoni, Ndauka alikutwa na mashine 10 za EFD zidhaniwazo kuwa za wizi au kuchukuliwa kwa njia ya isivyohalali.
Mshtakiwa Mhavile, inadaiwa Julai 8 mwaka huu maeneo ya Lumumba mkoani Dar es Salaam, alikutwa na mashine 10 za EFD na kutoa risiti za kielektroniki kinyume na sheria.
Medalakini aliendelea kudai kuwa washitakiwa wote kwa pamoja kati ya Mei 13 na Julai mwaka huu mkoani Dar es Salaam, washitakiwa Mhavile, Ndauka na Msesya waliisababishia serikali (TRA) hasara ya Sh milioni 954.5.
Katika shtaka la utakatishaji fedha, inadaiwa kati ya Mei 13 na Julai mwaka huu, jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote kwa kutumia mashine hiyo walitoa risiti zisizohalali zilizotumiwa na walipakodi wengine kudai Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya Sh milioni 954.5 kwa TRA wakati wakijua kwamba fedha hizo ni zao la kosa la kuisababishia serikali hasara.
Hata hivyo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi ambazo kwa kawaida husikilizwa mahakama Kuu ama kwa kupewa kibali kutoka kwa DPP.
Hata hivyo, wakili wa utetezi Kesiel Kikoti, alidai kwa mujibu wa katiba washitakiwa hao kwa kuwa bado wana tuhuma, wana haki ya kupata dhamana hivyo aliomba mahakama hiyo kuwapa dhamana wakati wakisubiri upelelezi kukamilika
Akijibu hoja hiyo, Wakili Medalakini alidai makosa wanayoshtakiwa nayo washtakiwa hao hayana dhamana kwa mujibu wa kifungu cha 148(5)(a) hivyo maombi yao ya dhamana hayana mashiko.
Akitoa uamuzi mdogo, Hakimu Kiswaga alisema kwa mujibu wa sheria ikiwemo kifungu cha 148(5)(a) kinataja makosa ambayo hayapaswi kupewa dhamana ikiwemo utakatishaji fedha.
Akasema kwa msingi huo, washtakiwa wataendelea kukaa rumande hadi Agosti 21 mwaka huu kesi yao itakapoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Leave A Reply