The House of Favourite Newspapers

Magufuli, Lissu Uamuzi Mgumu

0

 

MOTO wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, umeendelea kukolea na kuwaacha wananchi katika wakati mgumu wa kutafakari mgombea watakayempatia ushindi ifikapo Oktoba 28 mwaka huu, UWAZI linachambua.

 

Hayo yanajiri wakati wagombea wa nafasi ya urais, Dk. John Magufuli (CCM) na Tundu Lissu (Chadema) wakizidi kuoneshana umwamba wa kipekee katika kipindi cha wiki mbili za kampeni tangu pazia lifunguliwe na Tume ya Taifa ya Uchaguzi Agosti 26 mwaka huu.

 

CCM ilizindua kampeni zake Agosti 29 katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, ilhali Chadema nao wakizindua kampeni zao Agosti 28 katika uwanja wa Zhakem Mbagala jijini Dar es Salaam.

 

Tayari wagombea hao wawili wamefanikiwa kuzunguka maeneo mbalimbali hususani kanda ya ziwa, kanda ya kati na Kusini na kujaza nyomi ya watu.

 

Katika uchaguzi huu, CCM na Chadema ndivyo vinavyopewa nafasi kubwa ya ushindi hasa baada ya mgombea urais kupitia ACT Wazalendo, kuonekana kulegalega, huku wenziye yaani Lissu na Dk. Magufuli, wakizidi kuchanja mbuga.

 

MAGUFULI

Mojawapo ya kete muhimu ambayo mgombea wa CCM amekuwa akijinasibu nayo, ni kufafanua ahadi alizotekeleza katika kipindi cha miaka mitano tangu alipoingia madarakani Novemba 5, 2015.

Kete hiyo amekuwa akiitumia katika hotuba zake pindi anapozungumza na wananchi katika maeneo mbalimbali kwa kuwahakikishia kuwa, ataendeleza pale alipoishia.

 

“Yale niliyowaahidi hata yale ambayo hatukuwaahidi, tutayatekeleza kwa spidi kubwa. Tumekuwa na historia ya kuwaachia viongozi kufanya yale waliyopanga, Baba wa taifa mlimpa miaka zaidi ya 20, Mzee Mwinyi, Mkapa na Kikwete mliwapa miaka 10 kila mmoja, mimi nimetumikia miaka mitano, msinipime kwa miaka mitano, naomba mnipime kwa miaka 10.

 

“Ndiyo maana nawaomba kura zenu ili tuweze kutengeneza Tanzania mpya. Katika kipindi cha miaka mitano, Tanzania imekuwa nchi ya uchumi wa kati, sasa tutaenda uchumi wa katikati,” alisema Magufuli alipokuwa akihutubia wananchi Mwanza.

 

LISSU

Wakati Magufuli akijinasibu kwa yale aliyotekeleza, kwa upande wake mgombea wa Chadema, Tundu Lissu amejikita kuelezea sera zake na kuzikosoa sera za Magufuli katika kipindi cha miaka mitano aliyokuwa madarakani.

 

Awali alipoanza kampeni, Lissu alijikita kuelezea wananchi kile kilichompata Septemba 7 mwaka 2017, kwamba madhila aliyofanyiwa na watu wasiojulikana kwa kujeruhiwa kwa risasi 16.

 

Wachambuzi wa mambo ya siasa, walitafsiri hotuba zake kuwa anaelezea hayo ili kupata kura za huruma kwa wananchi, jambo ambalo pia ni zuri kete kisiasa, lakini katika mikutano iliyofuata aliendelea kujikita kufafanua sera za ilani ya chama chake.

 

Mbali na sera hizo, pia Lissu amejikita katika kuzungumza matatizo yanayowagusa wananchi moja kwa moja, jambo ambalo linamuongezea uwingi wa wananchi katika mikutano yake sawa sawa na Dk. Magufuli.

 

“Mkinichagua kuwa Rais wa Tanzania, wakulima na wafugaji Serikali yangu itaangalia maslahi yao kwa upana na hakutakuwa na mkopo, ni mkono kwa mkono yaani nipe nikupe,” alisema akiwa Mwanza.

 

Akiwa mkoani Morogoro, alisema “Nikiwa Rais wa Tanzania na nikaunda Serikali, nawaahidi Mkoa wa Morogoro jambo la kwanza litakuwa kutaifisha mapande makubwa ya ardhi yaliyochukuliwa na Matajiri hapa Morogoro.

 

“Kila mtu akiwa mkubwa, anaona hapa Morogoro ndipo mahali pa kwenda kutajirikia kwa kuchukua ardhi, tutafanya mabadiliko makubwa ya mfumo wa ardhi Morogoro na sehemu nyingine nchini. Wananchi wanahangaika ardhi zinachukuliwa na wakubwa, wakulima na wafugaji hawatogombana tena.”

 

MTIHANI MGUMU KWA WAPIGA KURA

Wakati wagombea hao wakiendelea kutunishiana misuli, kwa kufafanua kwa kina sera na ilani za vyama vyao, kwa upande mwingine wananchi sasa wamebaki kuwa na mtihani mmoja tu wa kutafakari kwa kina na kumpa kura yule wanayemwamini.

 

Aidha, licha ya vipaumbele vya vyama hivyo kusheheni mambo ya msingi ambayo yanagusa changamoto za Watanzania, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa, wamebainisha mambo matatu ambayo yanawapa wapiga kura wakati mgumu katika kufanya maamuzi magumu.

 

ILANI TAMU

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. George Kahangwa, alisema ni dhahiri kuwa vyama vyote vina ilani nzuri ambazo zinaelezea kwa kina namna watakavyotekeleza ahadi zao. Aliongeza kuwa, hapo ndipo mtihani unapojitokeza kwa wananchi kuamua hasa ikizingatiwa kila chama kina ilani tamu.

 

HAKUNA ‘PERSONALITIES’

Aidha, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Muhidin Shangwe, anasema katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, kulikuwa na muktadha wake. “Siasa za wakati huo zilikuwa siasa za watu zaidi, zilichagizwa na makundi ndani ya CCM ambayo yalikuwa na vinara wake, kinara mkubwa alikuwa Lowassa, Magufuli hakuwepo kwa ukubwa.

 

“Baada ya hapo, Serikali ya Magufuli imekuwa ikijaribu kujiweka mbali na serikali zilizopita, unaweza kusema tumepata uhuru mwaka huo au chama kipya kimeingia madarakani, ni kwa sababu wanaCCM walikata tamaa hivi.

“Kwa hiyo, CCM imekuwa ikifanya kampeni zinazoelezea wamefanya nini na watafanya nini. Kwa kuwa wanatafuta kura, inabidi waseme watafanya nini,” alisema.

 

Alisema kwa upande wa upinzani, wanatumia lugha ya kisiasa kujaribu kuonesha mapungufu ya serikali ambayo inajisifu.

“Wanaonesha mashimo, ili wao waende sambamba na hali ya sasa. Lakini ili kuachana na dhana ya kwamba upinzani ni kulalamika tu bila kueleza watafanya nini, sasa kumekuwa na msukumo wa kueleza watafanya nini.

 

“Kufanya hivyo, ndiyo wataweza ku-‘deal’ na CCM. Wanalazimika kueleza wangekuwa wao madarakani wangefanyaje. Ili kuonesha wao ni mbadala, wanalazimika kueleza watu watafanya nini,” alisema.

 

Alisema muktadha huo unawapa wakati mgumu Watanzania kufanya uamuzi mgumu kwa sababu miaka yote walikuwa wanafuata watu badala ya masuala, lakini sasa kumekuwa na muako ambao watu wanafuatilia masuala.

 

KUTAFAKARI KWA KINA

Akizungumza na UWAZI, mmoja wa wachambuzi wa masuala ya siasa, Hebron Mwakagenda alifafanua kuwa uchaguzi wa mwaka huu, unawalazimu Watanzania kutafakari kwa kina kuhusu mgombea sahihi anayeweza kutatua changamoto zao.

GABRIEL MUSHI, UWAZI

 

Leave A Reply