The House of Favourite Newspapers

Maiti ya baamedi yaokotwa mtaroni

0

Unyama! Maiti ya mhudumu wa baa moja iliyopo maeneo ya Mbagala-Misheni jijini Dar, Leah Amosi (24), mwenyeji wa mkoani Dodoma, imeokotwa kwenye mtaro katika Barabara ya Kilwa karibu na Kiwanda cha Nguo cha KTM-Mbagala na kuzua utata mkubwa kutokana na hali aliyokutwa nayo.

Habari kutoka eneo la tukio zilieleza kwamba, Leah ambaye alifika jijini Dar mapema mwaka huu, alianzia kufanya kazi kwenye Baa ya Yamoto kabla ya kuhamia kwenye baa hiyo iliyopo maeneo hayo ya Mbagala-Misheni ambapo maiti ya baamedi huyo ilikutwa na wapita njia Novemba 6, mwaka huu majira ya saa 11:00 alfajiri.

Kwa mujibu wa wafanyakazi wenzake, usiku wa kuamkia siku hiyo, Leah alikuwa kazini kama kawaida ambapo aliondoka bila taarifa majira ya saa 5:00 usiku na hakuonekana hadi maiti yake ilipookotwa.

Akizungumza na gazeti hili, rafiki wa Leah ambaye alikuwa akiishi naye kwenye chumba kimoja, Mariam Omary alisema kuwa mara kwa mara Leah alipokuwa akimaliza kazi usiku ilikuwa lazima ampitie kazini kwake kwenye baa nyingine kisha wote kurudi pamoja nyumbani.

Alisema kuwa, katika hali ya kutia shaka, siku ya tukio hakumpitia, jambo lililomfanya ahisi huenda aliamua kurudi nyumbani peke yake.

“Baada ya kuona kimya niliamua kukesha kazini kwa sababu kulikuwa na kazi nyingi. Ilipofika saa 12:00 alfajiri, kuna rafiki yetu mmoja akaja na pikipiki akaniambia kuna tatizo nyumbani, nikaondoka naye lakini tulipofika maeneo ya KTM ndiyo nikaona watu wengi barabarani, nilipoangalia mtaroni nikamuona Leah akiwa amekufa.

“Maiti yake ilikuwa imevunjika mkono wa kushoto na mguu wa kushoto na alikutwa na nguo ya ndani ‘taiti’ na brazia. Baadaye polisi walifika tukaenda nao hadi Hosipitali ya Temeke na kuanza taratibu za msiba,” alisema Mariam kwa huzuni.

Hata hivyo, ndugu wa Leah walionesha kushangazwa na ripoti ya uchunguzi juu ya kifo hicho iliyosema Leah amefariki dunia kwa kugongwa na gari jambo ambalo wanandugu hao walilipinga.

Katika msiba wa Leah uliotawaliwa na vilio, ulihudhuriwa na mabaamedi wenzake na wateja wa baa aliyokuwa akifanyia kazi ambao walishiriki kutoa michango ya mazishi na gharama za kusafirisha mwili wa marehemu kuelekea nyumbani kwao wilayani Kongwa, Dodoma ambapo alizikwa Novemba 8, mwaka huu.

Leave A Reply