The House of Favourite Newspapers

Majambazi Wanaswa Dar, Kamanda Wambura Atoa Kauli – Video

0

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Camilius Wambura, amesema jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa kadhaa wa matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha, wizi na ujambazi, katika oparesheni maalum iliyoanza Mei 21, 2021 jijini Dar es Salaam.

 

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Kamanda Wambura amesema jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa watano wa ujambazi, wakiwa na bunduki moja aina ya pump action katika eneo la Mwasonga, Kigamboni, siku chache baada ya kufanya kuvamia katika lindo lililokuwa likilindwa na askari wa Suma JKT na kupora silaha hiyo pamoja vitu vingine kadhaa na fedha.

 

Pia Kamanda Wambura amesema jeshi hilo limewakamata watuhumiwa wengine watano wa ujambazi, wanaokabiliwa na mashtaka ya mauaji ya mlinzi wa baa moja iliyopo Mikocheni, ambapo walivamia na kumshambulia kwa silaha za jadi mlinzi huyo kisha kupora vitu mbalimbali.

 

Kamanda Wambura ameongeza kuwa jeshi hilo linawashikiliwa watuhumiwa wengine wa watano kwa makosa ya uvunjaji wa nyumba na uporaji, sambamba na kukamata magari manne na pikipiki moja, vyote vikiwa ni vya wizi.

 

Amewaonya watu wote wanaojihusisha na matukio ya uhalifu, kuacha mara moja kwani jeshi hilo lipo imara kuhakikisha wakazi wa Dar es Salaam na mali zao wapo salama.

 

Leave A Reply