The House of Favourite Newspapers

Makambo Arejea Kuipa Ugumu Simba SC

HUENDA ikawa habari njema kwa Yanga na mbaya kwa mashabiki wa Simba. Ni baada ya mshambuliaji wa Wanajangwani, Heritier Makambo kutarajiwa kuanza mazoezi na timu hiyo, akitokea kwenye majeraha.

 

Mshambuliaji huyo alipata maumivu ya misuli kwenye mchezo uliopita wa Kombe la Shirikisho Afrika wakati timu hiyo ilipocheza na Rayon Sports ambao ulimalizika kwa Yanga kufungwa bao 1-0, hivi karibuni. Katika mchezo huo, Makambo alishindwa kumalizia mechi hiyo na kutolewa dakika ya 69 baada ya kugongwa na goti kwenye sehemu ya msuli wa paja.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Zahera alisema mshambuliaji wake huyo tegemeo tayari amemaliza siku nne za mapumziko alizopewa na daktari wa timu hiyo, Edward Bavu. Zahera alisema, kwa kuanza atafanya mazoezi mepesi binafsi kwa muda wa siku mbili kabla ya kuanza magumu na wenzake siku ya tatu baada ya kuwafiti kwa asilimia 100.

 

Aliongeza kuwa, kurejea kwa mshambuliaji huyo kumempa matumaini ya kuendelea kupata ushindi katika michezo ijayo kutokana na umuhimu alionao mchezaji huyo kwenye safu yake ya ushambuliaji.

 

“Nilisikitika kuumia kwa Makambo kwenye mechi dhidi ya Rayon, beki wa Rayon alimgonga kwa makusudi kwa lengo la kumuumiza na ninaamini alifanya hivyo baada ya kumgundua ni mchezaji hatari.

 

“Sikutaka kumtoa katika mechi hiyo na nili_ kia maamuzi ya kumtoa kwa hofu ya kumuongezea maumivu zaidi, hivyo nikaona nimtoe kwani mchezo huo haukuwa na kitu cha kupoteza zaidi ya kukamilisha ratiba. Hivyo, Makambo amemaliza muda wa kupumzika alliopewa na daktari aliokuwa akiutumia kwa ajilli ya matibabu pekee,” alisema Zahera.

 

Makambo anatarajiwa kuwa mwiba mkali kwa Simba wakati watani hao wa jadi watakapokutana Septemba 30 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.

 

Wakati huohuo, Juma Abdul na Juma Mahadhi wamerejea na wataanza mazoezi leo Jumatatu kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi. Juma alikuwa anasumbuliwa na enka alipoumia katika mechi dhidi ya Mtibwa, wakati Mahadhi alikuwa akisumbuliwa na goti baada ya kuumia katika mechi dhidi ya USM Alger.

 

Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Comments are closed.