The House of Favourite Newspapers

MAKONTENA YA MAKONDA YAMEKUA KAMA SINEMA

 

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

MAKONTENA 20 ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda yalitakiwa kupigwa mnada kwa agizo la Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango na baadhi ya watu walimpongeza waziri huyo kwa msimamo wake huo.  Sababu kuu ya kupongezwa ni kwamba alionekana ni kiongozi ambaye haangalii sura ya mtu na yupo kwa ajili ya kulinda na kukusanya mapato ya Serikali kwa haki, uaminifu wenye utiifu ndani yake kwa njia ya kodi. Wachache wakaona kama vile anajitafutia matatizo kwani wengine wakasema anamgusa asiyegusika.

Lakini wapo wengi waliompongeza Makonda alipotoa vitisho vya laana kwa atakayenunua makontena hayo akidai ni vifaa vya ofisi za walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ukiwa msaada kutoka kwa Watanzania waishio Marekani. Akiwa mkuu wa mkoa huo, alienda mbali zaidi kwa kusema; ‘hao TRA na huyo waziri wenu’ (Philip Mpango) wakitimiza wanachotaka (kupiga mnada kontena zake), angeshtaki kwa Rais Dk. John Magufuli.

Baada ya kauli hiyo Waziri Mpango akapigilia msumari kwamba kama mtu akinunua makontena atapata laana basi anatamani yeye angekuwa na pesa ili anunue yote. Watu walewale kwa umoja wao wakampongeza tena Dk.Mpango. Ilionekana kama utani kama siyo maajabu, lakini pia kwa nyakati hizi hakikuwa kitu cha ajabu kushuhudia mgongano wa kauli kwa viongozi wetu. Imetokea mara kadhaa mkuu wa wilaya kufanya kazi za TRA, au mkuu wa mkoa kufanya kazi inayotakiwa kufanywa na jeshi la polisi.

Lakini hili la waziri wa fedha kutishwa kwamba kuna laana itatokea kwa atakayenunua makontena likazua gumzo. Wapo waliodhani ni sinema inachezwa. Kumekuwa na mawazo kwamba kukiwa na jambo fulani zito, Serikali inaibua jambo la kupumbaza watu wasahau au wapuuze mengine. Ilikuwa rahisi watu wengine kuhisi hivyo. Ingawa siyo rasmi lakini ukweli ni kwamba waziri wa fedha ni mtu mzito sana. Hata kiprotokali unaweza kuanza na rais, makamu wake, waziri mkuu kisha akafuata waziri wa fedha. Wizara ya Fedha ni roho ya nchi yoyote duniani. Waziri na RC wote ni wateule wa rais. Lakini kila mmoja ana mpaka wake, yule ni waziri wa fedha utendaji wake ni wa nchi nzima, mwingine ni mtawala wa mkoa mmoja. Yule ni waziri na mbunge kwa wakati mmoja, hilo tu ni jawabu tosha kuwa yuko juu yake kwa kila kitu.

Kisheria waziri wa fedha ndiye mwenye idhini ya kupokea au kusaini misaada kutoka nje na siyo mkuu wa mkoa wala waziri mwingine yeyote, hii ni elimu kwa wasiojua. Naamini RC Makonda na watu wake wa karibu hawakugundua au kujua au walipuuza hilo. Hakuna msaada wa namna ile ukaja kwa jina la mtu binafsi. Makontena yamekuja kwa jina la paul Makonda, mwenye jina la Makonda anakana

kuwa siyo makontena ya Makonda, bali ya walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Kontena zingeingia kwa jina la mtu binafsi na siyo ofisi, hapo kuna tatizo. Yawezekana kweli ni vifaa lengwa kwa ajili ya ofisi za walimu, lakini kutaka sifa ziende kwake, Makonda akaamua liandikwe jina lake badala ya ofisi zinazopewa msaada husika. Najiuliza je, hakushauriwa?

Makonda na Waziri Mpango, ni watu ambao kwa nyakati tofauti wamewahi kusifiwa na rais kwa utendaji kazi wao.  Wakati Makonda akiteuliwa kutoka Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni mpaka RC Dar es Salaam, Waziri Mpango ndani ya mwezi mmoja alipandishwa kutoka Naibu Kamishna kuwa Kamishna Mkuu wa TRA, kisha Waziri wa Fedha. Huu ni mwaka wa tatu Waziri Mpango anasimamia bajeti ya Serikali ya Rais Magufuli. Yeye ndiye injini ya mambo yote ya bajeti ya uendeshaji wa Serikali ya awamu ya tano. Siyo mtu mdogo au wa kukurupuka tu kwenye maamuzi kama hayo.

Kwa maoni yangu, Makonda alikuwa na nafasi kubwa ya kuongea na waziri na mambo yasingefikia hapa.Rais asingetoa maelezo juu ya sakata hilo inawezekana bado kungekuwa na sintofahamu juu ya makontena hayo.

Inawezekana Makonda hakusoma alama za nyakati. Rais Magufuli siku zote anapenda kutumia neno ‘kwa mujibu wa sheria’ anapoelezea jambo. Sakata hili amelimaliza kwa maelezo ambayo ni ya kwa mujibu wa sheria. Walewale waliomshangilia Makonda kisha Waziri Mpango, ndiyo walioshangilia zaidi ufafanuzi wa rais.

Mnada wa makontena umeshindwa kuuza kwa mara ya pili sababu kubwa iliyoelezwa na mpiga mnada mama Scholastika Kivela ni watu kutofika bei elekezi kutoka TRA. Kwa nini hawafiki bei? Kuna uwezekano TRA wamekurupuka kukadiria kodi isiyoendana na thamani halisi ya mzigo uliopo kwenye makontena?

Waziri alikurupuka bila kutathmini mzigo na kiasi cha fedha kilichotajwa kama kilivyo? Hapa kuna mambo mengi ya kutafakari badala ya kushangilia kwa makofi na vigelegele matamko ya viongozi wetu.

STORI: ELVAN STAMBULI, UWAZI

Comments are closed.